Monday, May 29, 2017

MWANZA WATAKA VIWANDA VYA PEDI ZA KISASA.

Muuguzi Mkuu mkoani Mwanza Agness Hassan, akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani 2017, kimkoa Mwanza yakifanyika uwanja wa Nyamagana hii leo Mei 28,2017.


Wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali Jijini Mwanza wameiomba serikali kusaidia ujenzi wa viwanda vya pedi za kisasa vitakavyosaidia pedi hizo kuuzwa kwa beo nafuu.

Hayo yamesemwa kwenye risala yao iliyosomwa na mwanafunzi Edna Ignas kutoka shule ya msingi Malulu, kwenye maadhimisho ya Siku ya hedhi duniani yaliyofanyika jana katika uwanja wa mpira Nyamagana.

Aidha wameomba ujenzi wa viwanda hivyo vya pedi uendani na kupunguza ama kuondoa kabisa kodi kwenye mauzo ya kodi hizo, hatua ambayo itasaidia kuuzwa kwa bei nafuu na hivyo kuwafikia wasichana wote hususani wanaotoka kwenye kaya zenye uwezo mdogo wa kiuchumi.

Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Youth With New Hope in Life Organization (TAYONEHO) la Jijini Mwanza, Dkt.Iman Tinda, amesema suala la hedhi limekuwa na changamoto kubwa ikiwemo baadhi ya mabinti wanafunzi kukosa masomo wakati wa hedhi.

Amesema mabinti hupoteza vipindi darasani kati ya siku mbili hadi saba kwa mwezi, siku 86 kwa mwaka na hivyo kuwa kikwazo kwao kimasomo ambapo ni vyema wadau wa elimu wakaungana pamoja ili kuvunja ukimya juu ya suala la hedhi na hivyo kuwasaidia mabinti kuondokana na changamoto wanazokumbana nazo katika kipindi hicho.

Naye Mratibu wa Shirika la Plan International mkoani Mwanza, Emmanuel Asaph, amebainisha kwamba elimu ya hedhi tayari imewafikia wanafunzi 250 kutoka shule 10 za msingi Jijini Mwanza pamoja na waalimu wa kike na kiume 20 ambao wamefunzwa namna bora ya kuwa msaada wa kwanza kwa mabinti watakaokumbana na changamoto za hedhi wawapo shuleni.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Muuguzi Mkuu mkoani Mwanza Agness Hassan, amesema halmashauri zote mkoani Mwanza kwa kushiriakana na kamati za shule zinafanya juhudi za kuhakikisha mazingira yanakuwa salama ikiwemo upatikanaji wa maji safi ili kuwasaidia mabinti kujiweka nadhifu pindi wawapo kwenye hedhi.

Maadhimisho hayo mkoani Mwanza yameratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la TAYONEHO la Jijini Mwanza kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Plan International pamoja na lile la SVC Mwanza.

Lengo ni uvunja ukimya juu ya masuala ya hedhi ikiwemo kuondokana na dhana potofu kwamba hedhi ni ugonjwa pamoja na namna bora ya kuhakikisha mtoto wa kike anajiweka katika hali ya usafi ili abaki shuleni badala ya kukosa masoko kila apatapo hedhi.

Siku ya hedhi duniani ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 baada ya kuidhinishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa ambapo ni mara ya kwanza kuadhimishwa mwaka huu 2017 nchini Tanzania ikiwa na kauli mbiu isemayo "Elimu juu ya hedhi hubadili kila kitu".
Mkurugenzi wa Shirika la TAYONEHO, Dkt.Iman Tinda, akizungumza kwenye maadhimisho hayo
Mwanafunzi Edna Ignas kutoka shule ya Msingi Malulu Jijini Mwanza, akisoma Risala kwa niaba ya wnafunzi wenzake kwenye maadhimisho hayo
Wanafunzi wakiwa kwenye maadhimisho hayo
Tazama Video hapo chini

No comments:

Post a Comment