Thursday, April 27, 2017

WAZIRI LUKUVI AANZA KUBAINI WADAIWA WA KODI YA PANGO LA ARDHI


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mh. William Lukuvi amefanya ukaguzi wa mfumo wa kodi ya ardhi katika manispaa ya Musoma Mjini mkoa wa Mara ambapo amebaini wananchi 231 wanadaiwa Kodi ya Pango la Ardhi kiasi cha shilingi milioni 271.
Mhe Lukuvi amemtaka Afisa Ardhi wa manispaa ya Musoma bwana Joseph Kamonga kuwasilisha majina ya wadaiwa hao katika Mahakama ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupiga mnada majengo na mali zao kawa wakikaidi kulipa kodi hiyo.
“nimeagiza kesi za madai ya kodi zitolewe hukumu ndani ya siku moja tu ili wadaiwa waweze kuchukuliwa hatua ya kuuzwa kwa mali zao haraka” Mhe Lukuvi aliyasema hayo wakati alipo fanya ziara ya kukagua mfumo wa kodi wa manispaa ya Musoma mjini ili kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi nchini wanalipa kodi kwa hiari kabla ya hatua za kisheria hazijafuata dhidi yao.
Aidha, Waziri Lukuvi amefanya uzinduzi wa mpango kabambe (Master Plan) wa Manispaa ya Musoma na kuwapongeza viongozi na watendaji wa manispaa ya Musoma kwa kuwa manispaa ya kwanza nchini kuweza kuzindua mpango kabambe wa mji wao. Pia aliwapongeza kwa uzalendo wao wa kutumia kampuni za ndani katika utekelezaji wa mpango huo.
Manispaa ya Musoma ilitoa tenda kwa kampuni zalendo ijulikanayo kama CRM ambayo ilithibitisha uzalendo wake kwa kumaliza kazi waliyopewa kwa wakati. Kutokana na hilo, Mheshimiwa Waziri alizitaka manispaa zingine kutumia kampuni za ndani ya nchi ambazo zimesajiliwa na wizara.
Mbali na hayo, Mh. Lukuvi aliiagiza manispaa ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa mpango kabambe kwa kutumia wataalam wao (wa serikali) au Makampuni ya ndani. Pia, aliiagiza manispaa ya Musoma kutoa nakala za kutosha ili mpango huo uwafikie wadau wote, na kutaka mpango huo utafsiriwe kwa Kiswahili ili madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa waweze kuwafikishia wananchi kwa urahisi.
Maagizo mengine ni pamoja na kwataka viongozi wa manispaa zote nchini kusimamia suala la ujenzi unaofuata mipango miji na kupiga marufuku wananchi wanaojenga bila kupewa vibali vya ujenzi katika maeneo ambayo yamekamilisha mipango kabambe na kuagiza nyumba itakayojengwa bila kibali ivunjwe.

Pia aliwataka maafisa ardhi wa manispaa kutoa elimu ya masuala ya Ardhi kwa kwa maafisa watendaji wa Mitaa ili elimu na utekelezaji wa masuala ya ardhi ngazi ya wananchi uwe ni kwa urahisi na wenye kueleweka.

No comments:

Post a Comment