Wednesday, January 11, 2017

SERIKALI WILAYANI HANDENI YAPIGA MARUFUKU UUZAJI HOLELA WA MKAA

Mkurugenzi akionesha baadhi ya vibakuli vilivyokamatwa ambavyo vilitengenezwa na mti aina ya mkarambati tayari kwa kusafirisha kuelekea nchini Kenya kwa mauzo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe na wataalamu wakipata maelekezo mafupi juu ya moja ya kituo cha kuuzia mkaa cha Manga.
Meneja wa wakala wa Misitu Tanzania wa Wilaya ya Handeni akizungumza na wafanyabiashara wa mazao ya misitu ya Mkaa wakati wa Uzinduzi.
Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji Bw. William Makufwe na Meneja wa wakala wa Misitu wa Wilaya Bw. Elias Mwaijere wakitoka kuzindua kituo cha wauza mkaa cha Manga
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe akizungumza na wafanyabiashara wa mkaa wakati wa Uzinduzi . 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe akizungumza na wafanyabiashara wa Mkaa.


Serikali wilayani Handeni imepiga marufuku uuzaji holela wa mkaa ili kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za misitu NA kuwataka wananchi kutumia vituo rasmi kuuza na kununua mkaa. 

Marufuku hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alipokuwa akizindua vituo maalumu vilivyotengwa kwaajili ya kuuzia mkaa (mkaa centre) vinavyotarajiwa kuwa mazingira rafiki kwa vijana wanojihusisha na biashara za mikaa wilayani hapa. 

Mh Gondwe alisema "ni marufuku kuanzia sasa mtu yeyote kuuza mikaa kwenye maeneo ambayo sio vituo rasmi, mkaaa utauzwa na kununuliwa kwenye vituo vilivyopangwa atakayekiuka hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake”. Aliongeza kuwa lengo kuu la kuweka vituo vya kuuzia mkaa ni kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za misitu; Kulingana na sera ya ukusanyaji mapato,kwa kutumia vituo hivi serikali itaweza kupata mapato yake ambayo hapo awali kulikua na utoroshaji na ukwepaji wa kulipa kodi kwa wavunaji na wauzaji wa mikaa.

Mkuu wa wilaya aliwataka wavunaji wa mkaa kuunda vikundi ambavyo vitawatambulisha na kusaidia kuwa na umoja utakaopelekea kupata vibali halali vya uvunaji wa mazao ya misitu. Alisema kuwa utaratibu huo utasaidia kuwepo kwa uvunaji endelevu ambao utahusisha kupanda miti na kuvuna tofauti na ilivyokuwa awali watu wanavuna miti bila kupanda miti mingine ili kufidia ile iliyovunwa hali itakayoiepusha Handeni kuwa jangwa na kuharibu vyanzo vya maji.

Aliwaeleza wananchi kuwa vituo hivyo vitasaidia kuwa na bei elekezi ambayo itawanufaisha wafanyabiashara wote tofauti na awali ambapo kulikua na ushindani mkubwa uliopelekea wengine kujaza lumbesa ili kupata wateja kwa haraka. 

Aidha Mkurugenzi mtendaji wa Halmasahuri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe aliwataka wafanyabishara wa mkaa kusajili vikundi vinavyojihusisha na uuzaji wa mikaa ili, watambuliwe na waweze kupata mikopo itakayowasaidia kujiendeleza ikiwezekana kuacha biashara ya mkaa na kujikita kwenye shughuli nyingine za kilimo, ufugaji na biashara nyingine ndogo ndogo.

Aidha, alisema kuwa Mikopo hiyo itawawezesha kununua miche ya miti na kuipanda ili kusaidia uvunaji endelevu, ambapo mwezi wa tatu kutakuwepo na zoezi la upandaji miti ambalo litawahusisha wafanyabiashara hao moja kwa moja. Vituo hivi vitasaidia pia kuwatambua na kuratibu kiwango cha mkaa kitakachokuwa kinavunwa na kutolewa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

Wakati huohuo Mkurugenzi Mtendaji chini ya kamati ya mapato inefanikiwa kukamata vibakuli zaidi ya 500 vilivyo tengenezwa kwa mbao za mkarambati vyenye soko nchini Kenya na mbao 914 zenye thamani ya milioni 24 ambazo zimevunwa kinyume chavsheria na kukiuka katazo la uvunaji wa miti ya mikalambati ambayo ipo hatarini kutoweka. Watuhumiwa wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Aidha Meneja wa Misitu Wilaya Bw. Elias Mwaijere, Aliwaeleza wanafanyabiashara hao kwamba kuna shamba la miti lijulikanalo kama Korogwe Plantation ambapo kila mwaka miche 5000 hupandwa na kuhamasisha na wao kuwa na tabia ya kupanda miti.Alieleza pia Halmashauri ya Wilaya ya handeni inatarajia kupata miche 3000 ambapo itapandwa kwenye maadhimisho ya siku ya upandaji miti mwaka huu 2017.

Vituo vimetakiwa kuwa na umbali wa mita100 kutoka usawa wa barabara, ambapo vituo vilivyopangwa ni pamoja na Manga, Tengwe, Kwenkwale, Chang,ombe, Kabuku na Mailikumi.

Alda sadango 
Afisa habari 
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

No comments:

Post a Comment