Wednesday, December 2, 2015

TANAPA YAIMARISHA ULINZI WA TEMBO KWA KUWAFUNGA VIFAA MAALUM.

 Wataalam wa Uhifadhi wakiongozwa na Dk. Alfred Kikoti (wa kwanza kulia) wakiendelea na zoezi la uwekaji kola maalum kwa tembo zinazosaidia kudhibiti mienendo ya tembo ndani nan je ya hifadhi ya Mfumo wa Ikolojia wa Ruaha Rungwa.
 Zoezi la uvalishaji wa kola maalum kwa tembo katika hifadhi ya Ruaha likiendelea.
 Helikopta maalum inayotumiwa na madaktari kwa ajili ya kutambua na kupiga dawa ya usingizi kwa tembo kabla ya uvalishaji wa kola maalum.
 Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi (mwenye kofia) akishuhudia zoezi la uvalishaji kola maalum kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
 Daktari wa Wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI) akijiandaa kumdunga sindano ya kumzindua tembo baada ya kukamilika kwa zoezi la kumvalisha kola maalum.
 Picha ya pamoja ya wahifadhi walioshiriki zoezi la uzinduzi wa program maalum ya uvalishaji kola kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi (kulia) akiongea na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa wakati wa zoezi la uvalishaji kola kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.

(Na Jovina Bujulu-MAELEZO)
Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zinazoliingizia Taifa pato hasa fedha za kigeni zinazotolewa na watalii wanaofika nchini kwa shughuli mbali mbali ikiwemo kuangalia wanyama na vivutio vilivyopo katika hifadhi za taifa.

Sekta hii ya utalii inakumbana na tatizo kubwa la ujangili ambalo linaripotiwa kuiingizia taifa hasara kubwa kutokana na idadi kubwa ya wanyama pori hasa tembo kuuawa kila mwaka.

Hivi karibuni Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) limezindua programu maalam ya kuwavalisha tembo kifaa maalumu kijulikanacho kama “kola” au king’amuzi maalum shingoni mwa tembo hao kinachong’amua na kurekodi mienendo yao kwa kutumia mawasiliano ya satelaiti.

Program hiyo inatekelezwa katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha Rungwa ambapo tembo 30 wanaoongoza makundi 30 wamevalishwa kola hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Bwana Allan Kijazi alisema kuwa inalenga kuimarisha ulinzi wa tembo nchini. “Lengo kuu la program hii ni kupata taarifa za kina juu ya mienendo ya tembo katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha Rungwe zitakazosaidia kubainisha maeneo shorobo (njia za wanyama) na mitawanyiko yao kwa ajili ya ulinzi wa tembo” alisema Bwana Kijazi.

Aliendelea kusema kuwa teknolojia hiyo inawawezesha kujua mwenendo wa tembo ndani na nje ya hifadhi, kujua walipo, wanapopita, kasi yao, sehemu wanazojificha, wanapokunywa maji, ikiwa wamejeruhiwa, wanapopumzika, maeneo wanayokaa muda mrefu, kama wamekufa, kama wamehama  hifadhi moja hadi nyingine na taarifa nyingine nyingi, hivyo itakuwa rahisi kwa askari wa wanyamapori kufuatilia usalama wa tembo hao.

Akizungumzia uanzishwaji wa program hiyo, Bwana Kijazi alisema kuwa inafadhiliwa na taasisi ya Global Government Facility pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP); ambapo UNDP kwa kushirikiana na TANAPA na SPANET wametoa kandarasi ya kufanya kazi hiyo ya kufunga “kola” kwenye tembo kwa kituo cha kimataifa cha utafiti wa Tembo “WORLD ELEPHANT CENTRE “ kilichopo mkoani  Arusha.

Bwana Kijazi aliendelea kusema kuwa, pamoja na shughuli ya kuweka “kola” kwenye tembo, pia kituo hicho kina jukumu la kuongeza hali ya usalama wa tembo katika hifadhi za Taifa.

Kwa upande Mkurugenzi wa Kituo cha World Elephant Centre Dkt. Alfred Kikoti ambaye pia ni mtafiti wa tembo aliyebobea kwenye sayansi za wanyama hao alisema kuwa kituo hicho kilianza kazi ya kufunga “kola” kwenye tembo kuanzia mwaka 2005 ambapo hadi sasa wamekwisha fanya kazi hiyo maeneo ya ukanda wa kaskazini kuanzia Serengeti, Loliondo, Manyara, na Tarangire.
Maeneo mengine ni Wami Mbiki mkoani Morogoro, Mashariki mwa Serengeti, Ziwa Natron, Kilimanjaro Magharibi na Amboseli upande wa Kenya. 

Dkt. Kikoti alisema kuwa sehemu zote walizofanya kazi ya kufunga kola kwenye tembo, kifaa hicho kinafanya kazi  vizuri ya kufuatilia mienendo ya tembo kwa tija na ufanisi mkubwa.
Akizungumzia jinsi kifaa hicho kinavyofanya kazi, Dkt Kikoti alisema kuwa, kifaa hicho kina uzito wa kilogramu 5 ambacho huvalishwa kwenye shingo ya tembo na kinarekodi mwenendo wa tembo kwa njia ya satelaiti. 

“Kituo kinafuatilia mienendo ya tembo kwa kutumia kompyuta maalum ambazo zimeunganishwa na kifaa hicho, hivyo  tembo wanaonekana kwenye kompyuta hizo, na kila wanapokwenda na wanachofanya kinarekodiwa.” Alisema Dkt Kikoti.

Aidha, Dkt. Kikoti alisema kuwa kifaa hicho kinatumia betri maalum ambayo ina uwezo wa kukaa kwa miaka 3 hadi 5, kabla ya kuweka betri nyingine.

Alipoulizwa jinsi namna wanavyowavalisha tembo kola hiyo, Dkt Kikoti alisema kuwa wanatumia helikopta ambayo inakuwa umbali wa mita 30 hadi 40 kutoka ardhini kulingana na ukubwa wa pori walipo tembo hao, na kuongeza kuwa wanachagua tembo mmoja kutoka kwenye kundi la tembo wanayeona anafaa kufungwa kola hiyo. 

“Tembo anayechaguliwa ni yule ambaye anaonekana ni kijana mwenye umri wa miaka 20 hadi 35, na asiye na mtoto,wala majukumu,  hapo daktari wa wanyama anamchoma sindano kutoka kwenye helikopta ambayo inamfanya alale usingizi na tembo wengine kwenye kundi wanakimbia kutokana na mlio na kelele za helikopta na baada ya hapo wanateremka kwenye  helikopta na kumvalisha kola hiyo” alisema Dkt Kikoti.

Aliendelea kusema tembo huyo baada ya kuzinduka huwafuata tembo wenzake na waliokuwa naye kwenye kundi na hapo kifaa hicho huanza kuratibu na kufuatilia mwenendo wa kundi hilo la tembo.

Akizungumzia kupungua kwa idadi ya tembo katika hifadhi za taifa, Dkt. Kikoti alisema kuwa kwa sasa hali si nzuri  kwani kwa kawaida makundi ya tembo huwa na tembo 150 hadi 300 lakini kwa sasa makundi yaliyofungwa kola ni yenye tembo 15 kwa kundi dogo na 300 kwa kundi kubwa.

Katika kuendeleza jitihada za kulinda tembo, Dkt. Kikoti alisema kuwa kwa sasa kituo cha World Elephant Centre kinaandaa ujenzi wa kituo kikubwa zaidi cha kimataifa kitakachoonesha taarifa za tembo dunia nzima ikiwa ni kumuenzi hayati Mwalimu Nyerere.

Naye Meneja Mawasiliano wa TANAPA Bwana Paschal Shelulete alisema kuwa zoezi la kuwafunga kola tembo litasaidia kudhibiti mienendo ya tembo na hivyo kujua walipo ili kuimarisha ulinzi dhidi ya majangili.

Dkt. Kikoti alizungumzia mafanikio ya program hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa maaskari wa wanyamapori kwani wanaelewa wanyama walipo na kuimarisha doria sehemu hizo. 
Mafanikio mengine ni idara ya wanyamapori kufahamu mienendo ya tembo na hivyo kuwaelekeza watalii sehemu ambazo tembo wanakuwepo kwa wakati huo.

Aidha matumizi ya ardhi yameboreshwa kwani kutokana na satelaiti kola kutoa taarifa tembo walipo, watu wamefahamu sehemu zinazofaaa kwa wao kuishi na kuendesha shughuli za kilimo. Pia kutokana na kuwepo kwa ufuatiliaji wa taarifa za mienendo ya tembo, migongano isiyo ya lazima kati ya tembo na binadamu imepunguzwa.

Pamoja na jitihada za serikali za kulinda tembo, wadau mbalimbali wa wanyamapori wameunga mkono suala hilo kwa kuanzisha kampeni ya “OKOA TEMBO WA TANZANIA.” ambayo ina lengo la kuhamasisha watanzania kuhifadhi tembo.

Akizungumzia sababu za kuanzisha kampeni hiyo, Mratibu wa kampeni hiyo Bwana Shubeti Mwarabu alisema kuwa walihamasika kutokana na takwimu za sensa ya tembo zilizotolewa na Taasisi ya Wanyamapori (TAWIRI) inayoonesha kuwa tembo wamepungua kwa asilimia 60% kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

“Mwaka 2009 idadi ya tembo ilikuwa 109,000 na ilipofika 2014 takwimu hizo zilionesha tembo wamebaki 43,000 kwa nchi nzima” alisema Bwana Shubeti.

Bwana Shubeti aliendelea kusema kuwa kampeni hiyo imefanikiwa kutoa elimu iliyotolewa kwa Umma kwa njia mbalimbali kama vile ushiriki wa maonesho mbalimbali na matamasha ambapo husambaza vipeperushi vinavyoonesha madhara ya kuua tembo, kufanya matamasha mbalimbali yenye lengo la kuzuia kuua tembo.

Programu ya kufunga kola tembo itaendeshwa kwa miaka mitatu, na inawashirikisha wadau mbali mbali wakiwemo, World Elephant Centre, TANAPA, Taasisi ya utafiti wa wanyamapori (TAWIRI), Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya wanyamapori, na askari wa hifadhi ya taifa. 

No comments:

Post a Comment