NA BASHIR YAKUB -
WAPO mawakala na wapo wanaohitaji kuwa mawakala, Kwa sasa biashara ya uwakala ni kubwa mno, wapo mawakala mitandao ya simu kama tigo, Airtel, voda n.k, mawakala makampuni ya usafirishaji kama mabasi, malori n.k , na makampuni mengine mengi. Mtindo wa biashara ya uwakala umekua sana katika siku za hivi karibuni.
Ni kutokana na ongezeko la makampuni na kukua kwa biashara, Upo umuhimu mkubwa wa kuijua biashara ya uwakala kwa undani hasa katika misingi ya kisheria .
Hii itakusaidia kuzijua haki zako, usipozijua haki zako za kisheria katika biashara kama hii ni vigumu kunufaika. Hii ni kwasabbu hutojua unastahili nini na nini hustahili. Ili kuliepuka hili unajikuta katika ulazima wa kuzijua taratibu za kisheria zinazohusu uwakala. Usiingie katika biashara hii bila kujua japo mambo kidogo ya msingi ya kisheria yanayohusu uwakala.
1.WAKALA NI NANI.
Sura ya 345 kifungu cha 134 cha sheria ya mikataba kinaeleza nini maana ya wakala. Kinasema kuwa wakala ni mtu aliyeajiriwa kufanya kazi au kitu chochote kwa niaba ya mwingine au kumwakilisha mtu mwingine katika shughuli fulani. Kwahiyo wakala ni mtu anayesimama badala ya mtu mwingine.
Huyo mtu mwingine huitwa mhusika mkuu, Kwahiyo wakala hufanya kazi kwa niaba ya mhusika mkuu, Humwakilisha mhusika mkuu.
2. SIFA ZA KUWA WAKALA.
Vifungu vya 135 na 136 vinaeleza sifa za mtu kuwa wakala au kuwa mhusika mkuu, Vinaeleza kuwa mtu yeyote mwenye umri wa mtu mzima yaani mwenye umri wa miaka 18 na kwenda mbele anaweza kuwa wakala.
Lakini pia ni lazima awe na akili timamu, Kwa sifa hizi pia unaweza kuwa mhusika mkuu,,hata hivyo hizi ni sifa za jumla za kisheria, yamkini zipo sifa nyingine kutegemea na mhusika mkuu anahitaji wakala wa aina gani kwa ajili ya biashara zake.
3. MAMLAKA ALIYONAYO WAKALA.
Kwa mujibu wa kifungu cha 38 wakala anayo mamlaka makuu ya aina mbili, Kwanza mamlaka ya kutamkwa (expres) na pili mamlaka ya kumaanisha(implied). Mamlaka ya kutamkwa ni yale yote ambayo ameambiwa kwa mdomo au kwa maandishi kuyatekeleza .
Ni yale yaliyo katika mkataba wake alioingia na mhusika mkuu.
Pili ni mamlaka ya kumaanisha.
Haya hayapo katika mkataba wake na wala hakuambiwa na mhusika mkuu lakini ameyatekeleza. Haya ni yale ambayo wakala huyatekeleza kwa nia nzuri au kwa lengo la kuikoa biashara na jambo fulani ambalo limetokea ama kwa dharula au vinginevyo.
Ikiwa wakala amefanya jambo jema na kwa nia njema hata kama halipo katika makubaliano kati yake na mhusika mkuu basi jambo hilo huhesabika ni sehemu ya mamlaka yake na mhusika mkuu hawezi kukataa kuliwajibikia kwa kisingizio kuwa halipo katika makubaliano.
4. HAKI YA WAKALA KUZUIA MALIPO YA MHUSIKA MKUU.
Ikiwa wakala anafanya biashara ambayo anatakiwa kuwasilisha pesa za mauzo kwa mhusika mkuu na ikatokea kuwa hajalipwa malipo yake basi anaweza kuzuia malipo ya pesa hizo ili kufidia hela anayodai. Muhimu ni kuwa asizuie pesa nyingi zaidi kuliko kiasi anachodai.
Pamoja na hayo kifungu cha 172 kinasema hakutakuwa na malipo kwa wakala kwa kazi aliyoiharibu. Wakala anatakiwa kuwa mwangalifu, mtiifu kwa maelekezo ya mhusika mkuu, na kujiepusha na uzembe au kutojali. Hasara anayoisababisha kutokana na haya itakatwa katika malipo yake.
5. WAKALA KULIPWA PESA ISIYOKUWA KATIKA MAKUBALIANO.
Ikiwa wakala amefanya jambo jema na la faida kwa mhusika mkuu basi wakala anastahili malipo ya jambo hilo hata kama malipo hayo hayapo katika makubaliano. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 174 cha sheria ya mikataba.
6. FIDIA KWA KUJIONDOA KATIKA UWAKALA.
Yeyote kati ya mhusika mkuu au wakala anaweza kujiondoa katika uwakala. Yeyote atakayejiondoa katika uwakala kabla ya muda wa makubaliano kuisha basi atalazimika kumlipa fidia mwingine. Akijiondoa wakala fidia italipwa kwa mhusika mkuu halikadhalika mhusika mkuu akijiondoa fidia italipwa kwa wakala. Taarifa ya muda wa kutosha ni lazima itolewe kabla ya kujiondoa la sivyo aliyejiondoa atalazimika kulipa fidia nyingine zaidi kwa madhara yaliyotokana na kujiondoa kwake ghafla.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
Je kodi kwa serikali juu ya wakala ikoje?
ReplyDelete