Monday, September 21, 2015

TAMASHA LA FAHARI YA MWAFRIKA KUFANYIKA OKTOBA 3,2015 CLUB YA ESCAPE ONE MIKOCHENI JIJINI DAR

 Mmiliki na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Black Sensation, Lilliane Masuka (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu Tamasha la Fahari ya Mwafrika litakalofanyika viwanja vya Club ya Escape One, Oktoba 3, 2015 Mikocheni jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Gabriel Manyaga na Mkurugenzi wa Ubunifu wa kampuni hiyo, Charlotte Mwaigwisya. 
 Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni ya Black Sensation, Gabriel Manyaga (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Mmiliki na  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Lilliane Masuka. 
 Mkurugenzi wa Ubunifu wa kampuni hiyo, Charlotte Mwaigwisya akitoa ufafanuzi kwa waaandishi wa habari kuhusu tamasha hilo.
 Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.

Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya Black Sensation inatarajia kufanya tamasha lenye kutangaza utamaduni wa Mwafrika Oktoba 3 mwaka huu katika Club ya Escape One iliyopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam ambalo linatambulika  kama 'Fahari ya Mwafrika'.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Mmiliki na Mkurugenzi Mtendaji wa  Kampuni hiyo, Liliane Masuka alisema tamasha hilo ni la muhimu katika kuutangaza utamaduni wetu.

Masuka alisema tamasha hilo linatarajiwa kuonyesha vitu mbalimbali vya asili ya mwafrika na tamaduni zake litakuwa la aina yake kutokana na maandalizi pamoja na washiriki.

Mkurugenzi huyo alisema tamasha hilo litakuwa na lengo lake likiwa ni kuhamasisha utamaduni na kubadilishana kimawazo pamoja na kufanya maonesha ta tamaduni mbalimbali.

"Oktoba 3 mwaka huu tutakuwa na tamasha ambalo litatambulika kwa jina la 'Fahari ya Mwafrika' na tunatarajia kutakuwepo na vikundi mbalimbali ambavyo vitaonesha utamaduni wetu," alisema. 

Masuka alisema katika tamasha hilo kutakuwepo na muziki wa dansi, vichekesho, maigizo, ngoma na vitu mbalimbali ambavyo kwa pamoja vinatangaza utamaduni wa Tanzania.

Alisema pia kutakuwa na vikundi mbalimbali kutoka shule za Sekondari, wanamitindo na wabunifu wa ndani ambao wataonesha vitu vyenye kuakisi utamaduni wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Gabriel Manyaga alisema pamoja na kuanda tamasha hilo pia wanatarajia kutoa tuzo za Fahari ya Afrika kwa watu ambao wataonesha kuudumisha uafrika kupitia tamasha hilo kubwa na la aina yake.

Alisema tuzo zitatolewa kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali ambavyo kwa pamoja vitazingatia sifa husika na sio kuchaguana kishabiki kama tuzo zingine zinazotolewa.

Manyaga alisema wao kama Black Sensation wanaamini kuwa wataweza kukuza na kuibua vipaji vya wasanii wa hapa nchini ambao wameshindwa kuonekana na kutambulika kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wao.

Mkurugenzi wa Ubunifu wa Kampuni hiyo, Charlotte Mwaigwisya alisema kampuni hiyo ilibuni tamasha hilo ili kutoa fursa ya kuutangaza utamaduni wetu ambao kwa kiasi kikubwa umeanza kusahulika kutoka na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa kasi ya kuutangaza.
 (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com

No comments:

Post a Comment