Friday, July 31, 2015

SHEIN AANDAA MIPANGO NA SERA ZA KUSAIDIA VIJANA ZANZIBAR

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ( Pichani) amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa mipango na sera nzuri za kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri wenyewe hasa waliojiunga katika vikundi vya ushirika na SACCOS.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeanzisha Mfuko wa kuwawezesha Wananchi Kiuchumi na tayari watu kadhaa wameanza kufaidika na Mfuko huo sambamba na kuwapatia mafunzo ya kitaalamu pamoja na kuvipatia vikundi vya ushirika mbinu za kupata masoko na kuwawezesha kuwa wajasiriamali wazuri.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Dk. Shein Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum, Mhe. Haji Omar Kheir, aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa Jumuiya ya Watazania Wasio na Ajira (TUEPO) huko katika ukumbi wa afisi za Jumuiya hiyo Rahaleo, mjini Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa katika kuwasaidia vijana walioshindwa kuendelea na masomo yao, Serikali imeyaimarisha mafunzo ya elimu ya amali katika vituo vya amali vya Mwanakwerekwe na Mkokotoni Unguja na Vitongozi huko Pemba.

Dk. Shein alisema kuwa kituo cha kuwaandaa wajasiriamali katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume imeshaanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kupatiwa mikopo.

Alisema kuwa katika vyuo hivyo vijana hufunzwa ujuzi wa kazi mbali mbali kama vile ufundi umeme, ufundi magari, useremala, uhunzi, kutegengeneza mafriji na amali nyengine ambapo tayari vijana wengi wameweza kunufaika na kujiajiri wenyewe.

Aidha, aliwaeleza vijana hao kuwa mafunzo wanayotoa katika taasisi yao na taasisi nyengine binafsi ni kuongeza fursa za mafunzo ya elimu ya amali kwa vijana ili waweze kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.

Dk. Shein alisema kuwa ukosefu wa ajira nji tatizo linalozikabili nchi zote duniani hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapindyuzi ya Zanzibar zimekuwa zikichukua jitihada mbali mbali katika kukabiliana na tatizo hilo kwa kushirikiana na jumuiya za Kimataifa, sekta binafsi na jumuiya hiyo ya TUEPO.

“Hivyo kuwepo kwenu hapa ni hatua ya juhudi za pamoja ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote huwa inazishajihisha katika kukabiliana na tatizo la ajira hasa klwa vijana wetu”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua ukubwa wa tatizo la ajira kwa vijana kutokana na uchache wa fursa za ajira serikalini na kuwepo kwa ongezeko la vijana wanaomaliza masomo katika ngazi mbali mbnali kwa kila mwaka na kutegemea ajira ziliopo.

Alisema kuwa inatia moyo kuona hivi sasa, vijana wengi wasomi wameanza kushajihishana kuanzisha vikundi vya ushirika na kujiajiri wenyewe bila ya kuendelea kusubiri ajira Serikalinini.

Dk. Shein aliwanasihi vijana hao kuhakikisha kuwa mafunzo wanayotoa yazingatie ubora na hali ya mahitaji ya soko la ajira sambamba na kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Taasisi mbali mbali za Serikali kama vile Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali yenye dhamana ya kuhakikisha ubora wa elimu inayotolewa kwa wananchi.

 “Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya hii na taasisi zote zinazounga mkono mipango na jitihada mbali mbali za Serikali katika kuleta maendeleo na Ustawi wa wananchi wetu”,alisema Dk. Shein.

Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuzitumia vyema fursa zilizoandaliwa na Serikali pamoja na Taasisi binafsi katika kuwawezesha katika kukabiliana na tatizo la ajira hapa nchini.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya  ya Watanzania Wasio na Ajira (TUEPO) Ussi Said Suleiman alisema kuwa lengo la Jumuiya hiyo ni kuwandaa vijana kielimu kwa kufundisha fani mbali mbali pamoja na kuwatafutia fani mbali mbali ndani na nje ya nchi, ili kuondosha tatizo la ajira.

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa jumuiya inashirikiana na itashirikiana na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali katika kupunguza tatizo la ajira nchini ambapo tayari imeanisha chuo cha Tanzania star teachers college kwa lengo lam kwuasaidia wanachama wa jumuiya hiyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio ya Jumuiya hiyo pamoja na changamoto zilizopo, ambapo Waziri Kheir alichangia Tsh. milioni mbili kwa upande wake akiwa kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum.

Jumuiya hiyo imeenzishwa tarehe 23.4.2015 ikiwa na wanachama watano ambapo hadi sasa ina wanachama 210 .

No comments:

Post a Comment