Saturday, April 11, 2015

Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Limited Francis Nanai azindua asasi ya TAYL

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Francis Nanai akizungumza wakati akizindua asasi ya kuendeleza vijana katika masuala ya uongozi ijulikanayo kwa jina la Tanzania- Asia Young Leaders (TAYL).
Mjumbe wa Kamati Kuu na mmoja wa muasisi wa asasi ya TAYL, Ismail Biro akizungumzia historia na malengo ya asasi hiyo wakati wa uzinduzi uliofanyika kwenye hotel ya New Africa jijini.
Wajumbe na wanachama wa asasi hiyo walifuatilia uzinduzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Francis Nanai (Kulia) akiwa na mmoja wa waanzilishi na mkumbe wa kamati kuu ya asasi ya kuendeleza vijana katika masuala ya uongozi ijulikanayo kwa jina la Tanzania- Asia Young Leaders (TAYL) Rugambo Rodney. 

Na Mwandishi wetu
Vijana nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani ili kuweza kupata nafasi ya kuongoza taifa katika umri mdogo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Francis Nanai wakati wa uzinduzi wa asasi ya mpya ya kuendeleza vijana katika masuala ya uongozi ijulikanayo kwa jina la Tanzania- Asia Young Leaders (TAYL).

Nanai alisema kuwa vijana ndiyo taifa la sasa na lazima wajue kuwa nchi nyingi duniani zinawategemea vijana katika kuendeleza sekta mbalimbali mbali ya uongozi.
Alisema kuwa miezi michache ijayo, Tanzania itakuwa katika harakati za kupata viongozi wapya wa kuongoza taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano na kuwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo.

“Kuna mifano kibao ya viongozi vijana nchini ambao waliamua kuingia katika kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kuleta maendeleo, wengi wamethibutu kuingia katika mchakato na sasa ni mfano wa viongozi bora wa kuigwa hapa nchini,”

“Mfano Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa, Mbunge wa Chadema jimbo laUbungo John Mnyika na aliyekuwamMbunge wa jimbo Kigoma mjini, Zitto Kabwe, wote hao wameshika madaraka ya kuongoza nchi hii katika umri mdogo, naamini nanyi mna lanego hayo naomba mtimize ndoto zenu za kuwa viongozi bora katika nchi hii,” alisema Nanai.

Alisema kuwa sifa kubwa ya kufikia malengo na kuendeleza asasi hiyo ni kuwa na viongozi waadilifu, waaminifu, wenye moyo wa kujituma huku wanachama nao wakiwa na sifa hizo hizo.

“Huwezi kuwa na asasi yenye maendeleo mazuri kwa kuwa na viongozi na wanachama wasiokuwa na sifa ya uadilifu, wenye kujihusisha katika shughuli ovu na wezi, kwa kufanya hivyo mtakuwa mnarudi nyuma na matokeo kupotea katika ramani,” alisema.

Kwa mujibu wa Nanai, njia ya kupata au kufikia malengo yako katika maisha inatokana na misingi bora. “Nimefuraishwa na malengo yenu na mipango yenu, hivyo naomba mshirikiane ili kutumia fursa zilizopo, naamini hata washirika wenu wa bara la Asia nao wamevutiwa kutokana na misingo bora,” alisema.

Mmoja wa waasisi wa asasi hiyo, Ismail Biro alisema kuwa wamejipanga vyema kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kufikia malengo waliyojiwekea.

Biro alisema kuwa wanajua kuwa vijana wanakabiliwa na changamoyo mbalimbali ambazo wao wameziona na kuamua kuanzisha asasi hiyo kwa lengo la kuzitatua na kuwapa maendeleo kiungozi na kiuchumi.

Alisema kuwa kupitia asasi yao, vijana wataweza kupatiwa mafunzo mbalimbali ya uongozi, kuwasaidia na kuwawezesha vijana wa Tanzania na Asia katika kutumia fursa zilizopo. 

No comments:

Post a Comment