Tuesday, March 3, 2015

Yanga yaishukia bodi ya Ligi,yagomea mechi yao dhidi ya JKT Ruvu

Jerry MuroMsemaji wa Timu ya Yanga
Na Ripota wa Globu ya Jamii

Uongozi wa Klabu ya Yanga umeishukia bodi ya Ligi kwa kile walichodai kuwa wamechakachua kanuni kwa kuiruhusu Timu ya Simba kumtumia mchezaji Ibrahimu Hajibu na kuitaka sheria zichukue mkondo wake huku wakigomea mechi yao dhidi ya JKT Ruvu kusogezwa mbele.

Akizungumza kwenye Makao Makuu ya Klabu hiyo leo, Msemaji wa Yanga Jerry Muro amesema Bodi ya Ligi inayumbisha soka la Tanzania kwa kupindisha sheria na kitendo walichofanya ni cha ubabaishaji na hawawezi kukikalia kimya.

"Umeshaona wapi mtu anakosa, anakaa kujadili adhabu ya kupewa na mtoa adhabu, Tanzania ni ya kwanza, halafu eti tunataka soka letu lisonge mbele, litasonga mbele kwa stahili hii?"alisema kwa kuhoji.

Katika barua ya Februari 27 iliyosainiwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Fatuma Abdallah kwenda kwa katibu mkuu wa Simba Steven Ally ilisema "rejea barua yako ya Februari 25 yenye kumbukumbu namba SSC/29/2015/07/GS  kwa niaba ya bodi ya ligi tumezingatia maombi ya timu yako kutaka kwa mchezaji Ibrahimu Hajibu aruhusiwe kucheza mchezo wa Simba dhidi ya Prisons na Simba dhidi ya Yanga na asicheze mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Kwa kuzingatia mabadiliko ya katiba yaliyofanyika hivi karibuni, kwa barua hii mchezaji yuko huru kucheza katika mchezo wa Simba na Yanga." ilisema sehemu ya barua hiyo na nakala kutumwa kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Mkurugenzi wa Mashindano TFF, Kamati ya waamuzi, msimamizi wa kituo Dar es Salaam na Yanga.

Hata hivyo Yanga walidai kuwa hawawezi kukubaliana na jambo hilo kwa kuwa mabadiliko hayo ya katiba yalipendekezwa na bado hayajapata baraka ya mkutano mkuu.

Kwa mujibu wa kanuni ya 37 (4) ya Ligi kinachozungumzia udhibiti kwa wachezaji inasema 
klabu zinatakiwa zitunze kumbukumbu za wachezaji wake waliyoonyeshwa kadi. Klabu itakayomchezesha mchezaji mwenye kadi 3 za njano au kadi nyekundu itapoteza mchezo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu na  magoli 3, halikadhalika mchezaji anatakiwa atunze kumbukumbu zake za kadi na iwapo atacheza akiwa anatakiwa kutocheza kwa ajili ya kadi tatu za njano au kadi nyekundu timu yake itapoteza mchezo.

Wakati huo huo Yanga wamegomea mechi yao na JKT kusogezwa mbele na kudai kuwa Machi 11 hawatapeleka timu uwanjani kwa kuwa watakuwa wakijiandaa na mchezo wao na Plantiam ya Zimbabwe.

Katibu mkuu wa Simba Steven Ally alipoulizwa kuhusiana na suala la kuandika barua hiyo alisema "Ni kweli niliandika kama kupinga kanuni walitakiwa kupinga kwenye kikao cha bodi ya Ligi sio sasa, kanuni ilishapitishwa, na Yanga wanayo nakala tunashangaa sasa hivi wanavyopinga maamuzi ya TFF na bodi  ya Ligi basi waende Fifa."

Naye Katibu mkuu wa Simba Steven Ally alipoulizwa kuhusiana na suala la kuandika barua hiyo alisema "Ni kweli niliandika kama kupinga kanuni walitakiwa kupinga kwenye kikao cha bodi ya Ligi sio sasa, kanuni ilishapitishwa, na Yanga wanayo nakala tunashangaa sasa hivi wanavyopinga maamuzi ya TFF na bodi  ya Ligi basi waende Fifa."

"Tumejiandaa mechi yetu na JKT tunacheza kesho (leo), na Jumapili tunacheza na Simba, sasa bodi ya Ligi wanatuhujumu wanatupangiaje mechi tarehe 11 alafu tarehe 14 tucheze na Zimbabwe wanatutaka nini hao?" alihoji na kuongeza.

"Mkakati wetu ilikuwa tukimaliza mechi ya Jumapili akili yetu tunaelekeza kwa Zimbabwe, nasema tena Machi 11 hatupeleki timu tupo tayari kushuka daraja wakitaka waipeleke mbele zaidi tumalize na Zimbabwe."alisisitiza

No comments:

Post a Comment