Monday, March 9, 2015

APRM kuadhimisha miaka 12 ya mageuzi Afrika

Na Mwandishi Wetu

Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) Jumanne, Machi 10, 2015 unaadhimisha miaka 12 ya kuleta mageuzi ya utawala na utungaji wa sera bora barani Afrika.

Maadhimisho hayo yatafanyika kwa namna na staili mbalimbali Barani Afrika katika nchi wananchama wa Mpango huo ikiwemo Tanzania.

Hapa nchini kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa APRM, Mpango huo utaadhimisha siku hiyo kwa kufanya mjadala wa wazi kwenye Chuo Cha Diplomasia kilichopo Kurasini, Dar es Salaam utakaohudhuriwa na viongozi mbalimbali na wanadiplomasia.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni "Kuwawezesha Wanawake ili kuwa na Afrika yenye Amani na Fanaka". Kauli Mbiu hii inatoa fursa ya kuangazia mchango wa Wanawake katika ujenzi wa Tanzania iliyo bora zaidi, changamoto za usawa wa kijinsia na maoni ya nini kifanyike.

“Lazima sote tuendelee kupinga ukatili kwa binadamu wenzetu; ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia na  ukatili kwa watu wenye Albinism; na kuangalia njia za kuimarisha ushiriki wa Wanawake katika masuala ya Utawala bora, kuleta Amani na Maendeleo ya jamii kwa ajili ya Ustawi wa raia wote,” alisema Rehema.

APRM ni Mpango uliobuniwa na viongozi wa Afrika kwa ajili ya kufanya tathmini za utawala bora miongoni mwa nchi za Afrika kwa lengo la lkuchagiza utungaji wa sera, sharia na uchukuaji wa mambo ya kuigwa ili kila nchi iweze kujikosoa na kuboresha hali ya utawala na wananchi.

Tanzania ni miongoni mwa wananchi wa Mpango huu na tayari ilikamilisha hatua zote zinazotakiwa kwa kukamilisha ripoti yake ya tathmini na Rais Jakaya Kikwete aliiwasilisha mbele ya viongozi wenza Januari 26, 2013.

“Hii ni siku ambapo Serikali na wadau wa APRM kote Afrika wanakutana kutathmini kazi adhimu za Mpango huu wa mageuzi na kuangalia namna ya kuuboresha zaidi,” alisema Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib.

Katika nchi nyingi za Afrika zilizoamua kujiunga na Mpango huu, APRM imekuwa chachu ya maridhiano ambapo viongozi, wananchi wa kawaida na wadau wengine hukutana ili kubaini changamoto za kiutawala bora na kuainisha njia za pamoja za kuzitatua.

Katika miaka hii 12 pia APRM imekuwa kituo cha kuzuia migogoro ya kisiasa, raslimali na aina nyingine za migogoro kwa wadau kubaini viashiria vya mambo yanayoweza kuwa chanzo cha migogoro.

APRM pia imekuwa kioo cha kuchagiza mageuzi ya katiba, sharia na haki za binadamu na pale ambapo maonyo ya taarifa za APRM yalipopuuzwa Afrika ilipata fursa ya kujifunza. Kwa mfano kabla ya migogoro ya Kenya (2007/08) na vurugu za kibaguzi Afrika Kusini, ripoti za nchi hizo zilionya na kuainisha mambo ya kufanyiwakazi.

Pale viongozi wa nchi hizo wakati huo waliposhindwa kufanyiakazi viashiria hivyo vya vurugu kama vilivyokuwa vimebainishwa na ripoti za APRM, miezi kadhaa baadaye vurugu hizo hizo zilizotabiriwa ziliibuka na kuchafua Amani katika nchi hizo.

Akizungumza Januari 26, 2013 wakati akiwasilisha Ripoti ya Tanzania, Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi za APRM katika kulipa Bara la Afrika fursa ya kujitathmini na kujikosoa.

Alisema Tanzania imejiunga na APRM kwa sababu inaamini kuwa ni miongoni mwa nchi zinazoheshinmu utawala bora na kwamba inayo mengi ya kuipa mfano Afrika.

No comments:

Post a Comment