Monday, March 9, 2015

AFYA YA MAMA NA MTOTO NI AJENDA ENDELEVU - WADAU

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete katika picha hii ya maktaba anaonekana akimpa hongera mama ambaye amejifungua salama yeye na mtoto wake. Afya ya mama na mtoto ni moja ya ajenda ambayo inapewa umuhimu wa pekee katika duru ya Jumuiya ya Kimataifa. Tanzania na Canada kupitia wakilishi zao za Kudumu katika Umoja wa Mataifa zimeanzisha kundi la Nchi Marafiki kuhusu ajenda hiyo ya Afya ya Mama na Mtoto lengo kuu kuhakikisha kuwa mama na mtoto ni ajenda ambayo haifi.
Wawakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Canada katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Balozi Gillermo Rishechynski (pichani) mapema wiki iliyopita waliitisha kikao cha kwanza cha Nchi Marafiki kuhusu afya ya Mama na Mtoto, kikao hicho cha kwanza na ambacho kilifanyika katika uwakilishi wa Kudumu wa Canada, kilijadili pamoja na mambo mengine dhumuni la kuundwa kwa kundi hilo ambalo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba afya ya mama na mtoto inaendelea kupewa umuhimu katika malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015, pamoja na kushawishi uwajibikaji na uwekezaji katika eneo hilo. kundi hilo linaundwa na nchi 40 kutoka mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea.

Na Mwandishi Maalum, New York

Kundi la Nchi Marafiki kuhusu afya ya mama na mtoto limekutana na kufanya kikao chake cha kwanza na kukubaliana kwa kauli moja kwamba mama anapokuwa na afya njema anakuwa na uhakika wa maisha yake na maisha ya mtoto wake.

Kama hiyo haitoshi kundi hilo la nchi marafiki na ambalo limekutana nchi ya    uenyekiti- wenza wa Wakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Canada katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na Balozi Gillermo Rishchynski, limekubaliana haja na umuhimu wa kuhakikisha kuwa ajenda kuhusu afya ya mama na mtoto inaendelea na kubaki kuwa moja ya vipaumbele vya malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015.

Kundi la nchi hizo marafiki kuhusu afya ya mama na mtoto , linaundwa na wawakilishi kutoka nchi 40 zilizoendelea na zinazoendelea. Kikao hicho kwanza, kimehudhuriwa pia maafisa wa ngazi za juu kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwamo Bi. Amina Mohammed ambaye ni Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi na Mshauri wa Katibu Mkuu, kuhusu Mipango ya Maendeleo baada ya 2015.

Akizungumza mwanzoni mwa kikao hicho Balozi Tuvako Manongi amesemea, Tanzania imekubali na inajisikia fahari kuwa mwenyekit- wenza wa kundi hilo, kutokana na ukweli kwamba, Idadi kubwa ya vifo vya akina mama vitokavyo na matatizo ya uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga vinatokea Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“ Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara ni wadau wakubwa katika kulikabili tatizo hili kwa kushirikiana na wadau wengine, tumepiga hatua za kuridhisha katika kuhakikisha kwamba mama mjazito hapotezi maisha yake wakati wa kujifungua au mtoto mchanga hapotezi maisha yake mara tu baada ya kuzaliwa ingawa changamoto bado ni nyingi”.

Na kuongeza kuwa juhudi hizi zinahitaji pamoja na mambo mengine uwajibikaji wapamoja, uwezeshwaji wa raslimali fedha lakini kubwa zaidi utashi wa kisiasa na utimizwaji wa ahadi zinazotolewa na wadau mbalimbali.

Aidha Balozi Manongi amesisitiza pia umuhimu wa elimu kwa wanawake na hasa watoto wa kike kwa kile anachosema, mtoto wa kike akielimishwa kwa maana ya kupata fursa ya kwenda shule na kusoma, anakuwa na uelewa mpana wa mambo mbalimbali yakiwamo yanayohusu afya yake mwenyewe lakini pia afya ya mtoto wake.

“ Elimu kwa wanawake na watoto wa kike, ni jambo muhimu sana, na hasa ikizingatiwa wanawake ndio uti wa mgongo wa Bara la Afrika, mwanamke na mtoto wa kike anapopata fursa ya kupata elimu anao mchango mkubwa kwake mwenyewe, kwa familia yake na kwa jamii inayomzunguka” amesisitiza Balozi Manongi.

Naye Balozi wa Canada, Gillermo Rishchynski, pamoja na kusisitiza ushirikiano baina ya wadau mbalimbali katika jitihada hizi za kuimarisha kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto. Amesema serikali yake imetenga dola za kimarekani 3.5bn kwa pindi cha 2015-2020 kwaajili ya afya ya mama na mtoto.

Kundi la Nchi Marafiki kuhusu afya ya mama na mtoto litakuwa linakutana kila baada ya wiki sita au nane na litajielekeza Zaidi katika katika kufanya tathimini ya hali ya sasa ya utekelezaji wa malengo namba nne na tano ya maendeleo ya millennia mabayo utekelezaji wake unafikia ukingoni mwishoni mwa wamaka huu.

Kundi hili pia litakuwa na fursa ya kujadiliana, kubadilishana mawazo pamoja na kujiwekea mipango ya namna gani ya kuongozea jitihada za kusukuma mbele ajenda hii ya afya ya mama na mtoto kwa dhumuni la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.

Mwezi Mei mwaka 2014 Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Canada Stephen Harper ambao ni wenyeviti wenza wa Kamisheni ya Habari na Uwajibikaji kuhusu afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto waliongoza huko Toronto Canada, mkutano maalum wa wakuu wa nchi ambapo ilikubalika kwamba suala hilo lipewe kipaumbele katika kukalimisha Malengo ya Millennia yanayofikia ukiongoni mwaka huu.

Ni katika mkutano huo, ambapo ilikubalika kwamba Wawakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Canada katika Umoja wa Mataifa waunde kundi la nchi Marafiki kuhusu afya ya mama na mtoto.

No comments:

Post a Comment