Friday, July 18, 2014

ILI KUWA NA MAENDELEO ENDELEVU AFRIKA INAHITAJI UWEKEZAJI ZAIDI – BAN KI MOON


Na Mwandishi Maalum, New York
Wakati  ni jambo lisilopingika na linalokubalika na waafrika wenyewe na washirika wa maendeleo  kwamba   uchumi Afrika  unakua vizuri. Hata hivyo ukuaji huo unaelezwa bado haujaweza kupunguza au kuondoka changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazolikabili  bara hili na watu wake.
Na kwa sababu hiyo imeelezwa kwamba ili afrika iwe na maendeleo endelevu na  jumuishi basi  inahitaji kuongeza kasi ya kuvutia uwekezaji  na mitaji kutoka ndani ya Afrika yenyewe na nje.
Hata  hivyo suala  kubwa na ambalo limekuwa likiwafikirisha  waafrika wenyewe na wataalamu wa  masuala ya uchumi na maendeleo ni hili ,  je ni  aina gani ya  uwekezaji  na wenye tija ambao Afrika inauhitaji.
Katika siku nzima ya  Alhamisi Baraza kuu la Umoja wa Mataifa  lilikuwa na majadiliano  ya kina yaliyojikita katika eneo la Uwekezaji na umuhimu wake kwa maendeleo ya bara la Afrika na watu wake ni vile vile mchango wake  katika  mchakato mzima wa maendeleo endelevu baada ya  2015.
Mkutano huo  ulifunguliwa na  katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye katika hotuba yake, pamoja na kusifia namna Afrika ilivyopiga hatua nzuri katika ukuaji wa Uchumi,  akaeleza kuwa  kama kweli Afrika ilikuwa inataka maendeleo yamfikie kile mtu  basi  ilikuwa  inahitaji kufanya mambo matatu.
Kwa mujibu wa  Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa,  mambo hayo  ni  kujiwekea mazingira mazuri yatakayovutiwa wawekezaji , aina sahihi ya  miradi/ uwekezaji inayotakiwa  kuwekezwa na udhibiti mzuri wa  mapato yatokanayo na uwekezaji huo  ili  hatimaye yaweze kuhimili maendeleo endelevu.
Katika Mkutano huo na ambao washiriki mbalimbali walipata fursa ya kuchangia mawazo yao, Ban Ki Moon pamoja na  kuelezea maeneo hayo matatu,  alianisha pia mafanikio kadhaa na changamoto kadhaa ambazo anasema  Afrika inaendelea kukabilina nao, akazitaja baadhi ya change moto hizo kuwa ni  uwekezaji duni katika miundombinu, kilimo, ajira kwa vijana,  utaalam na teknolojia anuai na  tatizo kubwa la nishati ya uhakika na ambayo haiwafikii watu wengi.
 Katibu Mkuu alisifu mikakati na mipango mbalimbali ya kimaendeleo, kiuchumi na kijamii, ambayo ama Viongozi wa Afrika  tayari wameshaanza kutekeleza au  ilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Alipopata nafasi ya kuchangia maoni ya  Tanzania kuhusu umuhimu wa uwekezaji na  maendeleo kwa Afrika, Muwakilishi wa Kudumu wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi yeye alieleza kuwa pamoja na kwamba Tanzania ilikuwa inakubaliana na umuhimu wa uwekezaji kwa maendeleo,  uwekezaji huo  unahitaji ushirikiano wa pamoja,  uwazi na utawala bora.
Akaeleza kwamba kama ilivyoelezwa na  wazungumzaji wengine, sura ya Bara la Afrika imebadilika sana, Afrika ya sasa si ile iliyokuwa ikidharauliwa na kuonekana kama ni   bara lisilo na muelekeo wowote.
Akasema anakubaliana pia kwamba uchumi wa afrika  unakua vizuri na kuwa ukuaji huo umechangiwa na mambo mengi baadhi yake ni pamoja na  sera  na mipango mizuri ya kiuchumi,  uwepo wa  mazingira ya amani na usalama  katika maeneo mengi ya Afrika na  ukuaji ya kada ya watu wenye kipato cha kati pamoja na  wimbi kubwa la vijana ambao nao ni mtaji wa aina yake.
Balozi Manongi pia akagusia  umuhimu wa uwekezaji katika miundombinu,  afya, elimu na  kilimo kuwa ni   baadhi ya maeneo ambayo  kama yakiwafanyiwa kazi vizuri  yatasaidia  katika kuifanya Afrika isonge mbele.
Hata hivyo  Muwakilishi huyo wa Tanzania akasema  kasi ya ukuaji wa uchumi wa Afrika, pamoja na ule wa nchi moja moja na  jitihada  kubwa na nzuri zinazofanywa na  viongozi wakuu wa nchi na serikali pamoja wakishirikiana na wananchi wenyewe,  zinaweza kukwamishwa au zinakwamishwa na baadhi ya  na changamoto  kadhaa zinazohitaji ufumbuzi wa pamoja.
Moja ya  changamoto hizo na ambazo amesema ni  tatizo kubwa la linalochangia  kurudisha nyuma juhudi za nchi nyingi za  Afrika kujiletea maendeleo yao ni  tatizo la utoroshwaji wa fedha au biashara ya fedha haramu zinazofichwa nje ya  Afrika  na kusababisha ukwepaji mkubwa wa kodi.
Akasema  utoroshwanji huo wa fedha na ambazo hazilipiwi kodi  zinazinyima nchi zinazoendelea  mapato ambayo yangetumia kujenga hospitali, shule, barabara na  miradi mingineo ya maendeleo  pamoja na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millenia.
Changamoto nyingine alizosema zinarudisha nyuma maendeleo ya   Afrika ni pamoja na uvunuaji holela wa  maliasili,  biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na za kati na  rushwa.
Balozi  Manongi akasema ni  kwa sababu hiyo na nyingine nyingi ndiyo maana Tanzania imekuwa ikiunga mkono  malengo ya  maendeleo endelevu ambayo kwayo yatachangia  siyo tu  kuwahakikisha maendeleo  jumuishi kila mtu lakini pia yatakayoweza kukabiliana na changamoto alizozitaja.
Baadhi ya wawakilishi kutoka  mataifa yaliyoendelea waliozungumza katika   mkutano huo walijipambanua zaidi kwa kuelezea ni kwa namna gani nchi zao zimekuwa  zikichangia katika maendeleo ya Afrika kwa kutoa misaada mbalimbali ya  kimaendeleo yakiwamo pia masuala ya teknolojia.
Muwakilishi wa Marekani katika mkutano huyo naye pamoja na kuelezea  ushirikiano uliopo kati ya  Marekani na Bara la Afrika kwa maana ya maendeleo ya kiuchumi, alitangaza  katika mkutano huo kwamba,  Serikali ya  Rais Obama ilikuwa inaadaa mkutano  kati ya Marekani na Afrika. Mkutano huo utaojadili ushirikiano wa kibiashara na  unarajiwa kufanyika mwanzoni mwa wezi Agosti mwaka huu.



No comments:

Post a Comment