ABUJA,
Nigeria, May 8, 2014/ -- Rasilimali za Afrika zenye utajiri mwingi
zinatoa nafasi ya kipekee ya ufanisi katika uimarishaji wa maisha ya
raia wa Afrika, yasema ripoti mpya kubwa iliyozinduliwa leo na Kofi
Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, lakini mara nyingi
sana rasilimali hizi huporwa na maafisa wafisadi pamoja na wawekezaji wa
kigeni. Aidha, Ripoti hii inaonyesha kwamba kuongezeka kwa ukosefu wa
usawa vilevile kunaizuia Afrika isiikamate nafasi hii ya maendeleo.
Ripoti hii ya 2014 ya Jopo la Maendeleo ya Afrika (http://www.africaprogresspanel.org),
Nafaka, Samaki, Pesa: Kugharamia mageuzi ya Kijani kibichi na Samawati,
inawahimiza viongozi wa kisiasa wa Afrika kuchukua hatua hususa sasa
ili kupunguza ukosefu wa usawa kwa kuwekeza katika kilimo. Pia, inataka
hatua ya kimataifa kuchukuliwa ili kukomesha kile kinachotajwa kuwa
uporaji wa sekta za mbao na uvuvi.
“Baada
ya zaidi ya mwongo mmoja wa ukuzi, kuna mengi ya kushangilia,” Bwana
Annan atawaambia viongozi wa kisiasa na wa kibiashara, wakati wa
kuzinduliwa kwa ripoti hii katika mkutano wa Baraza la Kiuchumi la
Ulimwengu kwa Afrika (World Economic Forum for Africa). “Lakini ni
wakati wa kuuliza kwa nini ukuzi mkubwa wa jinsi hii haujasaidia hata
kidogo kuwainua watu kutoka katika umasikini na kwa nini utajiri mwingi
wa Afrika umeharibiwa kupitia mazoea ya ufisadi na uwekezaji usio
mnyoofu.”
“Afrika
ni bara lenye utajiri mwingi, kwa hivyo ni kwa nini fungu la Afrika
katika utapiamlo ulimwenguni, na idadi ya vifo vya watoto inaongezeka
haraka jinsi hii? Jibu ni kwamba ukosefu wa usawa unadhoofisha uhusiano
kati ya ukuzi wa kiuchumi na maendeleo katika hali ya maisha ya watu,”
alisema Bw. Annan.
Hata
ingawa wastani wa mapato umeongezeka kwa theluthi moja katika mwongo
uliopita, kuna Waafrika wengi zaidi sasa wanaoishi katika
umasikini-takriban milioni 45- zaidi ya waliokuwepo katika mwisho wa
miaka ya 1990. Malengo mapya ya kimaendeleo huenda yakajaribu kuodoa
umasikini Afrika kufikia mwaka wa 2030 - lakini kwa mkondo wa sasa,
Mwafrika mmoja kati ya Watano bado atakuwa akiishi katika umasikini
mwaka huo utakapofika.
Bw.
Annan, ambaye aliathiri kwa kiwango kikubwa Malengo ya Maendeleo ya
Milenia, asema: “ Mbali na kuahidi kutimiza malengo makuu, nchi
zinapojiunga na mfumo huu mpya wa kimaendeleo ulimwenguni zinapaswa
kuahidi pia kupunguza mapengo yasiyoweza kutetewa katika bara hili, kati
ya matajiri na masikini, maeneo ya vijijini na mijini, wanaume na
wanawake.”
Waandishi
wa ripoti hii wanatambulisha kilimo kuwa msingi wa ukuzi ambao
utapunguza umasikini. Wanadhihirisha kwamba masikini wengi wa Afrika
wanaishi na kufanya kazi katika maeneo ya vijijini, na kwa wingi ni
wakulima wadogo wadogo.
“Nchi
ambazo zimejengwa juu ya misingi ya sekta bora za kilimo - kama vile
Ethiopia na Rwanda- zimeonyesha kwamba maeneo ya vijijini yanaweza kuwa
kichocheo kikubwa cha ukuzi wa pamoja na upunguzaji wa umasikini,” Bw.
Annan atasema katika uzinduzi.
Ripoti
hii inahimiza kuwe na “mageuzi ya kijani kibichi ya Kiafrika,” ambayo
yanadondoa masomo kutoka kwa mageuzi ya bara la Asia na kubadilishwa ili
kufaa hali za Afrika.
Kwa
wakati huu, gharama ya uingizaji wa chakula kutoka nchi za nje ni dola
za kimarekani bilioni 35, kwa sababu kilimo cha ndani kimekumbwa na
uzalishaji wa kiwango cha chini, ukosefu wa uwekezaji, na ujitengaji wa
kimaeneo. Kuongezeka kwa uwekezaji katika miundombinu na utafiti
kunaweza kuinua kwa kiwango kikubwa mavuno ya eneo hili na mapato ya
wakulima. Kwa wakati huo huo, kuondoa vikwazo vya kibiashara ndani ya
Afrika kunaweza kufungua soko mpya.
Hata
ingawa ripoti hii inakosoa viongozi wa Afrika, Ripoti ya 2014 ya Jopo
la Maendeleo ya Afrika inaipa changamoto jamii ya kimataifa kuunga mkono
jitihada za kimaendeleo za Afrika. Inadhihirisha kwamba sekta za kilimo
na mbao ndizo sekta mbili muhimu zinazohitaji kuimarishwa ili kupambana
na uporaji wa rasilimali za asili.
Uvuvi
haramu, usiodhibitiwa na usioripotiwa umefikia kiwango cha juu
kupindukia katika maji ya pwani ya Afrika. Afrika Magharibi hupoteza
takriban dola za kimarekani bilioni 1.3 kila mwaka. Zaidi ya gharama za
kifedha, uporaji huu huangamiza jamii za kivuvi ambazo hupoteza nafasi
muhimu za uvuvi, utayarishaji na uuzaji wa samaki. Dola zingine bilioni
17 hupotezwa kupitia ukataji haramu wa miti.
“Uporaji
wa rasilimali ni wizi uliopangwa na unaofichwa kwa hila katika
biashara. Meli za biashara za uvuvi za kigeni, ambazo husajiliwa katika
nchi za Kiafrika kwa hila, na kupakua samaki katika bandari ambazo
hazirekodi mapato yao, hazina maadili,” alisema Bw. Annan, akiongeza
kwamba shughuli hizi haramu hukuza tatizo la ukwepaji wa kodi na kampuni
bandia. Ripoti ya 2014 ya Jopo la Maendeleo ya Afrika inahimiza kuwepo
kwa usimamizi wenye wahusika wengi wa sekta ya uvuvi ambao utatekeleza
vikwazo juu ya meli ambazo hazisajili na kuripoti mapato yao. Ripoti hii
aidha inazihimiza serikali ulimwenguni pote kuidhinisha Makubaliano ya
Port State Measures, mkataba ambao unalenga kuwazuia waporaji kupakua
mapato yao haramu katika bandari.
Viongozi
wa kisiasa wa Afrika wameshindwa kusimamia rasilimali za asili kwa
masilahi ya wanaozimiliki kihalisi- watu wa Afrika. Pamoja na kupoteza
pesa kupitia uporaji na usimamizi mbaya wa kifedha, Waafrika wanapoteza
pesa za kigeni, si ambapo wafadhili wanapokosa kuweka hadi zao tu, bali
pia wakati Waafrika wanaoishi katika nchi za kigeni wanapotuma pesa kwa
familia zao. Inakadiriwa kwamba kila mwaka bara hupoteza zaidi ya dola
za kimarekani bilioni 1.85 katika ada za kupindikia zinazotozwa kwa
huduma hizi.
Zikiwa
na mapato makubwa ya rasilimali, serikali za Afrika sasa zina nafasi ya
kutengeneza mifumo bora ya kodi – na kutumia pesa za umma vizurikwa
njia ya usawa, ripoti hii inaongeza. Kwa mfano, asilimia 3 ya pato la
jumla la eneo (GDP) kwa sasa huelekezwa kwa ruzuku za nishati ambazo kwa
sehemu kubwa huenda kwa watu wa tabaka la kati kati. Pesa hizo
zinapaswa kugeuzwa na kupelekwa kwa matumizi ya jamii ili kuwapa
masikini nafasi bora ya kutoroka mtego wa umasikini.
“Uwezo
wa Afrika wa kukabiliana na hali ngumu, na ubunifu ni mkubwa,” asema
Bw. Annan. “Tuna idadi kubwa ya vijana wenye nguvu. Wajasiriamali wetu
wanatumia teknolojia kubadilisha maisha ya watu. Tuna rasilimali za
kutosha kulisha si sisi tu bali na maeneo mengine pia. Ni wakati kwa
viongozi wa Afrika - na wawekezaji shirika wenye uwajibikaji - kuibua
uwezekano huu mkubwa.”
Distributed by APO (African Press Organization) on behalf of the Africa Progress Panel (APP).
Ikisimamiwa
na Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Jopo hili
lenye watu kumi hutetea, katika viwango vya juu sana, maendeleo endelevu
na yenye usawa barani Afrika. Jopo hili hutoa chapisho lake kuu, Ripoti
ya Maendeleo ya Afrika, kila mwaka mwezi Mei. (http://www.africaprogresspanel.org)
No comments:
Post a Comment