Afisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Swissport Tanzania Bw Gaudence Kilasara
Temu akizungumza na wanahisa wa kampuni hiyo wakati wa mkutano wao Mkuu
wa Mwaka uliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano jioni.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni ya Swissport Tanzania Jeroen de Clercqakizungumza
na wanahisa wa kampuni hiyo wakati wa mkutano wao Mkuu wa Mwaka
uliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano jioni. Wapili kushoto ni
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya hiyo Bw Gaudence Kilasara Temu
akifuatiwa na mmoja wa wakurugenzi wa bodi Bw. George Fumbuka.
Afisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Swissport Tanzania Bw. Gaudence Kilasara
Temu akizungumza na waandishi wa habari nje ya mkutano mkuu wa mwaka wa
kampuni yake uliyofanyika Jumatano jioni jijini Dar es Salaam.
Afisa Fedha Mkuu wa kampuni ya Swissport Tanzania Mrisho
Yassin akiwaongoza wanahisa kupitia ripoti ya mahesabu ya fedha ya
mwaka 2013, wakati wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa kampuni hiyo
uliyofanyika jijini Dar es Salaam Jumatano jioni. Wapili
kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya hiyo Bw Gaudence Kilasara
Temu akifuatiwa na mmoja wa wakurugenzi wa bodi Bw. George Fumbuka na
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bw. Jeroen de Clercq.
Mmoja
wa wanahisa wa kampuni ya Swissport Tanzania akichangia mada wakati wa
mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa kampuni hiyo uliyofanyika jijini
Dar es Salaam Jumatano jioni.
Swissport yapata ongezeko la faida kwa asilimia 17
· Pato la kila hisa lapanda kwa asilimia 11.5
· Yatenga Dola milioni 6.3 kujenga gala ya kisasa ya mizigo uwanja wa JNIA
Kampuni
ya Swissport Tanzania Plc imepata ongezeko la faida ya kabla ya kodi la
asilimia 17 la shilingi milioni 11,387 ikilinganishwa na shilingi
milioni 9,723 zilizopatikana katika mwaka wa fedha wa 2012, mafanikio
hayo yakitokana na maendeleo makubwa ya sekta ya usafiri wa anga
Tanzania.
Ongezeko
hilo la faida katika kampuni limewezesha pato la kila hisa kuongezeka
mpaka shilingi 208.22 ukilinganisha na shilingi 186.75 iliyoripotiwa
mwaka 2012, ikiwapatia wanahisa kila sababu za kutabasam baada ya kupata
ongezeko la asilimia 11.5 la hisa zao.
Haya
yalithibitishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Tanzania Plc Bw.
Gaudence Kilasara Temu katika taarifa yake kwa wanahisa wakati wa
Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika Jumatano jijini Dar es Salaam.
Bw.
Temu alisema kuwa ukuaji wa huduma za Fastjet, mwaka mzima wa
uendeshwaji wa shirika la Kenya Airways, uanzishwaji wa safari za ndege
kubwa kama Turkish Airlines na Qatar Airways katika uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro; na ongezeko la idadi za safari na mabadiliko
makubwa yaliyofanywa na Emirates, KLM, Ethiopian Airways, Qatar Airways,
South African Airways, Egypt Air na Rwanda Air yamesaidia kampuni ya
Swissport kufanya vizuri.
“Huu
ulikuwa mwaka wa mafanikio ambapo tumeweza kutanua shughuli zetu katika
viwanja vya ndege vya Mtwara na Songwe. Tumewekeza kikamilifu katika
vituo hivi vipya na tumeweza kufanikiwa. Vituo hivi viwili vinaumuhimu
mkubwa kutokana na kuwa katika maeneo mazuri kijeografia,” alisema
Temu.
Alisema
kwa mwaka 2013 kampuni iliweza kusimamia jumla ya safari 13,098 za
ndege ikiwa ni ongezeko la asilimia 13 uklilinganisha na safari 11,590
zilizosimamiwa na kampuni hiyo kwa mwaka 2012.
Abiria
waliohudumiwa na kampuni hiyo kwa mwaka 2013 walikuwa 905,347
ikilinganishwa na abiria 657,072 waliohudumiwa kwa mwaka 2012, ambalo ni
ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka 2012.
Mizigo
iliyosimamiwa kwa mwaka 2013 ilikuwa ni tani 25,126 ikiwa ni ongezeko
la asilimia 11 ikilinganishwa na tani 28,354 zilizosimamiwa mwaka 2012.
“Ongezeko
kubwa la safari zilizosimamiwa katika mwaka linaonyesha ukuaji wa pato
kwa asilimia 25 mpaka shilingi milioni 23,214 ikilinganishwa na shilingi
milioni 18,551 iliyopatikana mwaka jana. Pato litokanalo na mizigo nalo
limekuwa kwa asilimia 9.3 mpaka shilingi milioni 12,900 ikilinganishwa
na shilingi milioni 11,802 zilizopatikana mwaka 2012,” alisema.
Ofisa
Mtendaji Mkuu huyo aliongeza kuwa pato la jumla la kiuendeshaji la
kampuni kwa mwaka huo limeongezeka kwa asilimia 19 mpaka shilingi
milioni 36,115 ikilinganishwa na shilingi milion 30,353 zilizopatikana
katika mwaka 2012.
Alibainisha
kuwa gharama za jumla za kiuendeshaji za kampuni kwa mwaka zilikuwa ni
shilingi milioni 24,811 ambalo ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa
na shilingi milioni 20,683 zilizoripotiwa katika mwaka 2012.
“Kwa
upande mwingine mapato ya kabla ya riba, kodi, uchakavu na marejesho ya
kampuni yalikuwa ni shilingi milioni 13,677 ikilinganishwa na shilingi
milioni 11,598 iliyoripotiwa mwaka 2012, hii ikiwakilisha ongezeko la
asilimia 18. Mali za jumla za kampuni nazo zimekuwa kwa asilimia 18.4
kutoka shilingi 18,490 milioni katika 2012 mpaka shilingi 21, 895
milioni kwa mwishoni mwa mwaka 2013,” alisema.
Naye,
mwenyekiti wa Bodi ya Swissport, Juan José Andrés Alvez alibainisha kwa
wanahisa kuwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2013, kampuni ilianza ujenzi
wa gala la mizigo la kisasa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA), ambao utagharimu zaidi ya Dola za kimarekani
milioni 6.3.
“Gala
hili jipya la mizigo ya kutoka nje linategemea kuanza kufanyakazi
ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba 2014 baada ya hapo gala la zamani
litabadilishwa na kuwa eneo la mizigo inayokwenda nje, likiwa na kituo
cha kuhifathi bidhaa zinazoharibika kwa haraka likiwa na majokofu na
friji ili kuhifadhi bidhaa aina tofauti kama samaki, nyama, mbogamboga,
maua na madawa.
Eneo
hili jipya la bidhaa ziendazo nje linategemewa kurahisisha
usafirishwaji wa bidhaa nje ya nchi hususani bidhaa za jamii ya maua,
nyama na samaki,” alisema.
Mwenyekiti
aliongeza kuwa ikiwa ni kama mkakati wa kuboresha utoaji huduma kwa
wateja wao, shilingi 3,165 milioni ziliwekezwa kwa mwaka 2013
ukilinganisha na shilingi 2,434 milioni zilizowekezwa katika mwaka
2012.
“Sehemu
kubwa ya uwekezaji ilielekezwa katika vifaa vinavyosaidia shughuli za
ubebaji mizigo za ardhini ili kuwahudumia vizuri wateja wetu ambao ni
mashirika tofauti ya ndege,” alisema Bw. Alvez.
No comments:
Post a Comment