Saturday, April 26, 2014

Tanzania kufikia kipato cha kati ifikapo mwaka 2025

Na Greyson Mwase, Ujerumani

Tanzania inatarajiwa kuondoka kwenye kundi la nchi masikini na  kuhamia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akifungua  kongamano linaloendelea huko Berlin nchini Ujerumani  kama njia mojawapo ya kuadhimisha jubilee ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kongamano hilo  linakutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabalozi, wataalamu na wafanyabiashara mbalimbali ambapo  Profesa Muhongo alipata nafasi ya kuwasilisha mada kuhusiana na  fursa zilizopo katika  sekta ya  gesi, mafuta ikiwa ni pamoja na madini.

Profesa Muhongo alisema ili nchi ya Tanzania iweze kupiga hatua kimaendeleo inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye nishati ambayo ndiyo yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Akielezea juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na maisha  bora, Profesa Muhongo alisema kuwa serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza juhudi  za kupeleka umeme kwenye vijiji vyote kwa awamu tofauti tofauti.

“ Hatuwezi kusema kuwa nchi imeendelea wakati wananchi wa vijijini hawana umeme, na katika kutambua hilo serikali imeweka nguvu nyingi  kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inapatikana vijijini na kuchochea maendeleo.” Alisisisitiza Profesa Muhongo.

Profesa Muhongo aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa  nchi inapata umeme wa kutosha, serikali imekwishaanza mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la gesi linaloanzia Mtwara hadi jijini Dar es salaam.
Akizungumzia mradi huo, Profesa Muhongo alisema kuwa gesi itakayozalishwa itatumika majumbani, viwandani, kwenye magari ikiwa ni pamoja na kuzalisha umeme wa kutosheleza nchi na mwingine kuuzwa kwenye nchi za jirani na kuliingizia pato taifa.

“ Kwa mfano mara baada ya kuzalisha gesi ya kutosha na kuondokana na  changamoto ya upungufu wa umeme wa kutosha kulingana na mahitaji makubwa ya wananchi, umeme wa ziada utauzwa kwa nchi jirani kama Kenya na Ethiopia.” Aliongeza Profesa Muhongo.

Profesa Muhongo aliendelea kusema kuwa  kugundulika kwa gesi katika mikoa ya Lindi na Mtwara na kuanza kwa mradi wa bomba la gesi kumepelekea wawekezaji kujitokeza ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha sementi cha Dangotte kitakachokuwa kikubwa Afrika Mashariki.

Alisema kuwa mnamo Oktoba 25, mwaka jana serikali ilizindua vitalu saba vipya  katika maji ya kina kirefu cha bahari ya Hindi  na kitalu kimoja Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika vya utafutaji wa mafuta na gesi na kuwataka wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo ya kuomba vitalu kwa kufuata masharti yaliyowekwa kabla ya Mei 15, mwaka huu.

Profesa Muhongo aliongeza kuwa mbali na umeme wa maji na mafuta Wizara yake imeweka pia mkazo katika vyanzo vingine vya umeme kama makaa ya mawe, upepo, nishati jadidifu kama njia mojawapo ya kuongeza umeme.

“Kwa mfano  umeme wa upepo unazalishwa mkoani Singida, vyanzo hivi na vingine vinasaidia mikoa ambayo iko nje ya gridi ya taifa kupata umeme.” Alisisitiza Profesa Muhongo.

Profesa Muhongo aliwataka  wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania kupitia sekta  za gesi, mafuta na madini na kuwahakikishia kuwa  zipo sheria zinazotoa mwongozo juu ya usimamizi thabiti ikiwa ni pamoja na sheria ya petroli ya mwaka 2008, sheria ya umeme ya mwaka 2008, sera ya gesi asilia ya mwaka 2013, sheria ya gesi ambayo bado ipo katika maandalizi na mpango kabambe wa matumizi ya gesi asili ambao bado uko katika hatua za mwisho za maandalizi.

Profesa aliongeza kuwa miongozo mingine ni pamoja na sera ya nishati ya mwaka 2003, sheria  ya petroli (utafutaji na uzalishaji) ya mwaka 1980, sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na nyinginezo.

Akijibu swali lililoulizwa kuhusiana na wataalamu kwenye sekta mpya ya gesi Tanzania Profesa Muhongo alisema Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikipeleka wataalamu katika mafunzo ya muda mrefu katika shahada ya uzamili katika vyuo vikuu vilivyopo nje ya nchi kama Uingereza na Scotland.

Aidha Profesa Muhongo aliongeza kuwa  tayari  chuo kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na chuo kikuu cha Dodoma vimeanza kutoa kozi  ya masuala ya gesi na mafuta ili kuongeza watalamu katika sekta hiyo.

Profesa Muhongo alisema kuwa serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikidhamini wanafunzi wanaosomea masuala ya gesi na mafuta katika chuo kikuu cha Dodoma ikiwa ni pamoja na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha kuwa watalamu wa kati (technicians) hawaachwi nyuma, Chuo cha Madini kilichopo Dodoma kimeanza kutoa mafunzo hayo katika kiwango cha diploma.

“Juhudi zote zinafanywa na  serikali kuhakikisha kuwa inazalisha wataalamu wa kutosha kwani ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya teknolojia; bila utaalamu katika nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea kamwe, wanasayansi wanahitajika sana.” Alisisitiza Profesa Muhongo.

Akizungumzia kwa upande wa madini, Profesa Muhongo alisema kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini ya kila aina chini ya dunia na kuna maeneo mengi sana ambayo madini hayajachimbwa bado na kuwataka wawekezaji kuwekeza katika sekta hiyo.

Profesa Muhongo aliendelea kusema kuwa serikali imeandaa ramani za kijiolojia na kuwataka wawekezaji kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa hiyo.

Alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani  umekuwa ni wa muda mrefu na kusisitiza kuwa ushirikiano huo unatakiwa uimarishwe haswa katika uchumi ili kupiga hatua za kimaendeleo.

Aliongeza kuwa ili kuinua sekta ya madini serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha shirika la madini la taifa (STAMICO) na kuwawezesha wachimbaji wadogo.
“Kwa mfano hivi majuzi tumetoa ruzuku ya dola za kimarekani 500,000 kwa wachimbaji wadogo ambao tunaamini wana mchango mkubwa sana katika pato  la taifa.” Alisisitiza Profesa Muhongo.

Akijibu swali kuhusiana na mchango wa madini kwa taifa, Profesa Muhongo alisisitiza kuwa sekta ya  madini imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa kwa kujenga mashule kwenye maeneo ya migodi, mahospitali, ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na matumizi mengine.

Profesa Muhongo alisisitiza kuwa serikali inawakaribisha wawekezaji  kwa mikono miwili kuwekeza katika sekta hizo ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha ili kujenga uchumi na kudumisha uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani.

Alisema kuwa suala la rushwa halina nafasi katika uwekezaji na kuwataka wawekezaji hao kujitokeza na kuwekeza kwa kuwa fursa ni nyingi mno.

Alitaja sheria zinazosimamia sekta ya madini ni pamoja na sheria ya madini ya mwaka 2010, sheria ya ulipuaji baruti ya mwaka 1963, sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004, sheria ya kodi ya mwaka 2004 na nyinginezo.

No comments:

Post a Comment