Thursday, November 21, 2013

MAJARIBIO YA AWALI YA MATUMIZI YA "VIDEO CONFERENCE" YAFANYIKA KWA KUZIKUTANISHA OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA OFISI ZA MAKATIBU TAWALA NA WAKURUGENZI WA MAMLAKA YA SERIKALI ZA MITAA MIKOA YA RUKWA, LINDI, MARA, RUVUMA NA SHINYANGA

Pichani wajumbe mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa, Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri za Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo, Nkasi na Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia Mkutano wa kwanza wa majaribio ya huduma ya Video Conference leo katika ukumbi wa "Video Conference" uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Anayeonekana kwenye Luninga akiwasilisha mada ni Naibu Katibu Mkuu Utumishi Ndugu Hab Mkwizu ambao ndio walioandaa mkutano huo uliojadili mada mbalimbali.

........................................................
Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa Mikoa iliyowezeshwa kuwa na Miundombinu ya huduma ya "Video Conference" ambao unaratibiwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Huduma hii muhimu itasaidia sana katika kurahisisha mawasiliano Serikalini na hivyo kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji huduma kwa wananchi.

Katika majaribio ya awali Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imetoa mada mbalimbali kupitia mfumo huo kwa Makatibu Tawala pamoja na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mikoa ya Rukwa, Mara, Lindi, Ruvuma na Shinyanga.

Miongoni mwa mada hizo zilizowasilishwa zikifuatiwa na majadiliano ni Utekelezaji wa Mfumo wa "OPRAS" katika Utumishi wa Umma, Mwenendo wa utekelezaji wa masuala Anuai za jamii katika Utumishi wa Umma, Usimamizi na uzingatiaji wa Maadili ya Utumishi wa Umma na Mafanikio na Changamoto za utekelezaji wa Mfumo wa Taarifa za kiutumishi na Mishahara Serikalini.

Zoezi hili la majaribio limefanikiwa japo kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo kukatika kwa mawasiliano yanayounganisha picha na sauti sababu kubwa ikiwa ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kukosa huduma za Mkongo wa Taifa unaoratibiwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayanisi na Teknolojia.

Changamoto nyingine ni baadhi ya picha kuwa na muonekano hafifu, ambayo kwa mujibu wa Mchambuzi wa Mifumo ya Komputa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Ndugu Emmanuel Mwandiga inasababishwa pia na kasi ya huduma za mtandao kuwa chini pamoja na masafa ya mawasiliano kuwa hafifu.

Changamoto hizo zikifanyiwa kazi na Wizara husika ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ni wazi kuwa mfumo huo utakua njia sahihi zaidi na kisasa inayokwenda na wakati katika kurahisisha na kuboresha mawasiliano Serikali.
Wajumbe wakifuatilia mada kwa makini kupitia Luninga kubwa iliyopo mbele yao (Video Conferencing) Mambo yalikuwa yanakwenda "LIVE" ikiunganishwa Mikoa ya Rukwa, Lindi, Mara, Ruvuma, Shinyanga na Dar es Salaam ilipo Wizara ya UTUMISHI.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (wapili kushoto) nae alikuwepo kushuhudia Mkutano huo wa majaribio ambapo alipewa dakika kumi kuchangia juu ya mfumo huo ambapo alisema Serikali itaokoa fedha nyingi kuliko ilivyokuwa hapo awali ambapo wajumbe kutoka Mikoa mbalimbali walikuwa wakilazimika kusafiri kwa magari ya ofisi kuhudhuria vikao nje ya mikoa na maeneo yao ya kazi kwa gharama kubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya (kushoto) na Katibu Tawala Mkoa huo Alhaj Salum Mohammed Chima wakifuatilia moja ya mada iliyokuwa ikiwasilishwa kupitia mfumo huo mpya wa "Video Conferencing".
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Ndugu William Shimwela akichangia moja ya mada katika mkutano huo. Kulia ni Muhasibu Mkuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ndugu Sosthenes Mutarubukwa.
Wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali katika Mkutano huo.
Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa Ndugu Samson Mashalla akichangia moja ya mada katika mkutano huo. 
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada katika Mkutano huo.
(Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

No comments:

Post a Comment