Tuesday, October 1, 2013

Lindi na Mtwara wapata washirika kutoka Norway

Waziri wa nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akiwa katika majadiliano na Meya wa mji wa Hammerfest, Norway Alf Jakobsen. Pembeni ya Waziri, ni Balozi wa Norway nchini Tanzania Ingunn Klepsvik, pamoja na Ujumbe wa nchi zote mbili. Waziri na Ujumbe wake walitembelea nchini Norway hivi karibuni kujifunza namna serikali ya nchi hiyo ilivyofanikiwa kukuza uchumi wake kupitia sekta ya gesi na mafuta.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Meya wa mji wa Hammerfest ulioko Norway, Alf Jakobsen. Waziri aliongoza Ujumbe kutoka Tanzania katika ziara ya mafunzo nchini Norway hivi karibuni, kuhusu namna ambavyo sekta ya gesi inaweza kutumika kukuza uchumi wa nchi.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisalimiana na Meya wa mji wa Sandnessjoen nchini Norway, Bard Anders alipofika ofisini kwake kwa mazungumzo. Waziri na Ujumbe kutoka Tanzania walitembelea nchini humo hivi karibuni kwa ziara ya mafunzo kuhusiana na gesi asilia.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mwenye koti refu) akijadiliana jambo na Meya wa mji wa Sandnessjoen, Bard Anders (kulia kwa Waziri) na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ingunn Klepsvik (wa kwanza kushoto.) Waziri Muhongo na Ujumbe wake walikuwa katika ziara ya mafunzo ya gesi asilia nchini Norway hivi karibuni.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (mstari wa mbele-katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe ulioongozana naye katika ziara ya mafunzo kuhusu gesi asilia nchini Norway, pamoja na wenyeji wao mjini Sandnessjoen.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Idara ya Mafuta na Gesi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia kilichopo Trondheim Norway. Katikati ni Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ingunn Klepsvik. Waziri Muhongo alitembelea nchini Norway hivi karibuni akiongoza Ujumbe kutoka Tanzania kujifunza masuala yanayohusu sekta ya gesi asilia.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye tai) katika picha ya pamoja na wanafunzi Watanzania wanaosoma katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha nchini Norway, na Watanzania wanaofanya kazi nchini humo. Waziri aliwatembelea wanafunzi hao Chuoni kwao akiwa katika ziara ya mafunzo kuhusu sekta ya gesi asilia nchini Norway hivi karibuni.

Waziri wa nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo na viongozi wa miji miwili ya Hammerfest na Sandnessjoen iliyoko nchini Norway wamekubaliana kuanzisha ushirikiano baina ya miji hiyo na ile ya Lindi na Mtwara.

Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano baina ya viongozi wa miji hiyo na ujumbe wa wizara ya nishati na madini nchini Norway ambapo wamekubaliana kukutana mwezi ujao kuweka mikakati ya ushirikiano huo.

Katika makubaliano hayo viongozi kutoka pande zote wamekubaliana kuwa mji wa Harmmerfest utashirikiana na Lindi na ule wa Sandnessjoen utashirikiana na Mtwara, ushirikiano ambao unalenga kuzitumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza mara baada ya kufikia makubaliano hayo Waziri wa Nishati na Madini Profesa Muhongo amesema ili kuhakikisha mikoa ya kusini inanufaika na rasilimali zake, serikali imeamua kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kutimiza azma hiyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa wavuvi katika mji wa Sandnessjoen amesema uhusiano mzuri kati ya serikali na makampuni ya mafuta umechangia kubadilisha historia ya watu wa maeneo hayo ikiwemo kuwawezesha kukua kichumi na kuwasaidia kupata huduma mbalimbali za kijamii.

Akizungumzia umuhimu wa makampuni ya mafuta katita mji wa Sandnessjoen Meya wa mji huo Bard Anders Lango amesema, kwa kiasi kikubwa mapato ya mji huo yanatokana na mafuta.

Aidha Lango ameongeza kuwa asilimia Ishirini na mbili ya mapato yanayotokana na mafuta inatumika kutoa huduma muhimu za kijamii katika sekta za afya na elimu.

Naye Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Shirika la Mafuta la BP Olav Fjellsa amesema moja ya mbinu ambazo zimeliwezesha shirika hilo kujenga mahusiano mema na jamii ni kuhakikisha yanatoa misaada katika maeneo husika, kuwekeana mikataba mizuri pamoja na kujihusisha na ununuzi wa bidhaa za wazawa.

Kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya miji hiyo na mikoa ya kusini kutasaidia kufungua ukurasa mpya wa mahusiano na hiyvo kuwezesha wananchi kuwa sehemu ya mafanikio ya kuanzishwa kwa miradi ya umma katika maeneo yao.

Kabla ya ugunduzi wa gesi na mafuta miji hiyo miwili ilikuwa ikijishughulisha na uvuvi, kabla ya serikali ya Norway kuamua kuanzisha shughuli za uchimbaji wa gesi na mafuta baada ya kufikia makubaliano na wananchi wa maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment