Friday, September 20, 2013

GAWENI CHAKULA BURE NGORONGORO - WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaisimamia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuhakikisha kuwa wanagawa chakula cha bure kwa kaya 20,000 zinazoishi katika Tarafa ya Ngorongoro.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Septemba 19, 2013) wakati akizungumza na wakazi wa kata saba za Tarafa ya Ngorongoro katika mkutano wa hadhara uliofanyika Enduleni Madukani wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, kabla ya kuhutubia mkutano huo aliamua kukutana na Baraza la Wafugaji pamoja na wazee wa kimila (Malaigwanan) na kusikiliza kero kutoka kwa wazee hao.

Kero kubwa iliyowasilishwa kwenye kikao cha Malaigwanan na kwenye mkutano wa hadhara wa Endulen, ililenga kuiomba Serikali iwape ruhusa ya kuwa na mashamba madogo ya kujikimu kwenye maboma ya wafugaji wa Kimasai wanaoishi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro. Kero nyingine zilihusu ukosefu wa maji, ajira wa vijana, mitandao ya simu za mkononi na upatikanaji wa chakula cha msaada kwa haraka.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ambaye alitoa fursa kwa wakazi wawili wawili kutoka kila kata, wamuulize maswali na kutoa hoja zao katika mkutano huo, aliwakatalia ombi lao na kuwaeleza ugumu wa kulikubali ombi hilo kwa sababu linataka uchunguzi wa kina na halitaki kupatiwa jibu la papara kwa kuchelea madhara ambayo yanaweza kutokea endapo wakazi hao watapewa ruhusa ya kulima mashamba hayo ndani ya hifadhi.

Ili kukabiliana na tatizo la njaa linalowakabili wa tarafa hiyo, Waziri Mkuu aliagiza chakula kilichokuwa kimenunuliwa na NCAA kigawanywe haraka na tena bure badala ya kuwauzia wakazi hao ilhali wakijua hawana uwezo wa kununua chakula hicho.

Alifikia uamuzi huo baada ya kuelezwa na Mshauri wa Kisheria wa Baraza la Wafugaji, Bw. Eliamani Laotaika kwamba kuna chakula kiliagizwa na mamlaka hiyo kikaachwa hadi kikaharibika an kuchomwa moto.

Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Bw. Bruno Kawasange alipoitwa ajieleze ni kwa nini aliacha chakula kioze wakazi watu wana shida ya chakula, alikana tuhuma hizo na kusema si za kweli. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Enduleni, Bw. Julius Betei alipoitwa na Waziri Mkuu afafanue ukweli wa madai hayo, alisema hakuna chakula kilichoachwa kiharibike isipokuwa kilichopo kinauzwa kwa bei mbaya ambayo wananchi hawawezi kumudu.

Bw. Betei alisema debe moja la mahindi ya msaada kinauzwa kwa sh. 9,000/- wakati gunia moja linauzwa sh. 54,000/- ndiyo maana watu hawawezi kumudu bei hizo.

Wakati huo huo, Afisa Maendeleo ya Jamii anayeratibu masuala ya chakula katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Bw. Francis Kone alisema Julai 2012, mamlaka hiyo ilinunua magunia ya mahindi 7,000 na mpaka sasa imebakiwa na magunia 5,650 katika maghala yake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu aliwaomba radhi wakazi hao wa Ngorongoro kutokana na urasimu uliosababisha mahindi hayo yachelewe kuwafikia wananchi na kuahidi kufuatilia mahindi hayo yalikwama wapi na kwamba wangeanza kuyasambaza leo baada ya taratibu za kiofisi kukamilika.

Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka pamoja na Naibu Mawaziri wanne ili kuhakikisha kuwa tatizo la Ngorongoro linapatiwa ufumbuzi. Naibu Mawaziri hao ni Naibu Waziri wa OWM-TAMISEMI (Elimu), Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Naibu Waziri wa Maji pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mapema, Waziri Mku alizindua wodi ya wazazi kwenye kituo cha afya cha Enduleni wilayani Ngorongroro ambacho ujenzi wake umegharimu sh. milioni 185 pamoja na vifaa vyake.

Akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa kituo hicho, Dk. Flora Kessy alisema mbali ya wodi kituo hicho kimejenga nyumba wa kufikia wanawake wanaosubiri kujifungua yenye uwezo wa kuchukua wajawazito 30 kwa usiku mmoja.

“Tumeamua kujenga nyumba hii kwa sababu akinamama wengi wa tarafa hii hawawezi kufika hospitali kujifungua na baadhi yao wanatoka vijiji vya mbali. Tunawapokea akinamama wajawazito kuanzia miezi minane na huduma zitatolewa bure kama sehemu ya kuhamasisha na kuongeza idadi ya wanaojifungulia hospitali,” alisema.

Alisema kituo hicho kinahudumia wakazi 89,434 wa tarafa hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 27,240.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, SEPTEMBA 20, 2013.

No comments:

Post a Comment