Monday, September 16, 2013

Big Result Now; Tumechagua kutekeleza, si kutetereka tena

 Na Hassan Abbas
WAKATI dunia ikiingia muongo wa pili katika karne ya 21, yaani mwaka 2012, wanataaluma wawili waliandika maoni mawili kuonesha hisia zao mbili tofauti. Hawa hawakuwa wakitofautiana, bali wote walikuwa wakieleza na kuainisha hoja na haja ya kuonesha changamozo za msingi za kufanyiwakazi na dunia hii tuliyomo.
Mchumi mashuhuri duniani Joseph Stiglitz, aliaandika katika makala yake “The Year of Personal Pessimism” akionesha wasiwasi wake kuwa uchumi wa dunia ungedorora zaidi, lakini kwa upande wake aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair, yeye aliamini katika makala yake “Taking Faith Seriously” kuwa lazima tuendeleze mwafaka baina ya watu wa dini na tamaduni mbalimbali ili dunia iwe salama zaidi.
Wote hawa walikuwa wakizungumzia mambo wanayodhani katika mwaka huo yangeikwaza au kuisukuma dunia katika maendeleo zaidi. Walitofautiana juu ya nini kifanyike lakini walikuwa wanaungana juu ya umuhimu wa dunia kuwa salama zaidi kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Nimetanguliza nukuu hizo kuonesha sote tunavyoweza kuwa na maoni tofauti na katika namna tofauti lakini tukiwa sote tunakubaliana kuhusu jambo moja muhimu na adhimu-maendeleo na maisha ya watu.
Huu ndio mtazamo wangu wa kati baada ya kuzisoma makala mbili zilizojaa ufundi za hivi karibuni kuhusu maoni ya watu wawili adhimu-Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi wa Ikulu yetu ya Dar es Salaam na kwa upande wa pili mmoja wa wanahabari makini nchini, komredi Peter Nyanje.
Ingawa makala hizi ziliandikwa miezi kadhaa iliyopita kwa sababu bado uzito na umuhimu wake wa hoja zilizomo unaendelea kuwepo na kuibua mijadala mingine zaidi, nimeona si kosa nami leo nikaingia katika mjadala huu.
Katika maoni yake aliyoyapa anuani ya “Presidential Delivery Unit a waste of money,” aliyoyachapisha katika gazeti la The Citizen, komredi Nyange alionesha wasiwasi wake, moja kuhusu kufanikiwa kwa Kitengo kitakachoanzishwa cha Kufuatilia Utekelezaji wa Miradi Mikubwa (PDB) chini ya dhana ya BIG RESULTS NOW.
Katika andiko lake mhariri na rafiki yangu huyu wa zamani katika taaluma alionesha wasiwasi kadhaa ikiwemo kuhoji kama kuanzishwa kwa Kitengo cha Ufuatiliaji (PDB) chini ya Ofisi ya Rais si kuhamisha majukumu ambayo tayari yapo Tume ya Mipango na katika Mawizara mbalimbali?
Mahali fulani komredi Nyange alihoji kutokana na mengi ya kihistoria: “Considering the country’s failure to accomplish many development projects due to financial constraints, the establishment of the Presidential Delivery Unit does not make sense at all.”
Akichangia hoja katika makala yake aliyoipa anuani ya “Learn from history: Don’t be condemned by it,” mwanajumuiya mwenzangu na mwanamijadala katika Majadiliano Yenye Manufaa kwa Wote (Smart Partnership Movement), Balozi Sefue alieleza tofauti kubwa kati ya Tume ya Mipango na PDB.
Alieleza kuwa wakati Tume ya Mipango inapanga na kusimamia mipango na maeneo mapana ya kitaifa ya maendeleo ya nchi, PDP itakuwa ikisaidia kusimamia utekelezaji wa kasi na haraka wa maeneo machache ya mkakati na yanayohitaji matokeo ya haraka zaidi.
Balozi Sefue aliandika: “What President Jakaya Kikwete, his government and Parliament have decided is that we have to find a lasting solution to this problem of implementation.
“Putting more money through a system that falls short on delivery would be the real “waste”. Establishing the PDB will not lead to duplication of monitoring and evaluation efforts. PDB will instead fill gaps in the existing delivery system by, for the first time, bringing together essential “disciplines”.
Nimefurahi leo nami kuingia katika mjadala huu kwa sababu kama nilivyoainisha katika anuani ya makala yangu hii, mimi ni muumini wa utekelezaji si uteterekaji katika suala la maendeleo. Kama wanamjadala hao wote wanavyokubaliana, wakati fulani mahali fulani nchi yetu imekumbwa sana na changamoto ya utekelezaji.
Wakati fulani suala si fedha, suala si watu na wala suala si mipango mizuri bali kukosekana kwa mfumo makini na wa kitaalamu wa usimamizi wa utekelezaji kumekwaza sana kufikiwa kwa haraka na wakati mwingine kutofikiwa kabisa kwa baadhi ya mambo yaliyopangwa.
Dhana au falsafa ya BIG RESULTS NOW (BRN) kama ninavyoielewa imelenga kuja na tiba mujarabu ya gonjwa hili. Gonjwa la kupanga si kutekeleza. Gonjwa la kutekeleza kusikokuwa na uwiano na mipango. Na gonjwa la kutekeleza mengi yenye uwiano na mipango lakini si kwa lengo la haraka (SASA) na bila kujali aina ya matokeo: MATOKEO MAKUBWA au MAJANGA MAKUBWA!
Ukiangalia muktadha wa kuanzishwa kwa dhana hii na hicho kitengo ni dhahiri kuwa haya ni mageuzi makubwa tunayopaswa kuyapa nafasi katika nchi yetu. Nasema hivi kwa sababu binafsi nina amini kuwa walioleta dhana hii hawakutumia hisia, kujitakia bali tafiti.
                                      BRN ni utafiti si kujitakia
Napingana na wanaodhanai kuwa uamuzi wa nchi yetu kutekeleza dhana hii ya utekelezaji labda ni jambo la mtu mmoja tu kajitakia iwe hivi. Binafsi naamini kuja kwa falsafa hii ni matokeo ya uongozi uliosikiliza na kutafakati maoni na kelele nyingi za wananchi na tafiti za watafiti.
Dhana kwamba tumekuwa na tatizo katika nchi zetu zinazoendelea hasa katika eneo la kutambua vipaumbele na kutekeleza kwa makini, si suala la hisia tena. Bahati nzuri wana mjadala wenzangu niliowataja hapo juu nao wote kwa pamoja wanakubaliana na hili.
Bahati nzuri Bara la Afrika hivi sasa lina hazina ya Ripoti za utafiti zinazoainisha masuala anuai yanayokwaza Bara hili kuendelea. Katika Ripoti za Mpango wa Afrika Kujitathmini katika Utawala Bora (APRM) za nchi zaidi ya 15 sasa za Afrika zilizofikia hatua ya kutahminiwa ikiwemo Tanzania, kumesheheni matokeo haya ya kiutafiti.
Ripoti ya nchi yetu kwa mfano ya APRM ile ya awali (2009) na ya sasa iliyokamilika ya mwaka 2013 zote zinaainisha tatizo hili la falsafa yetu ya maendeleo huko nyuma kuathiriwa sana na changamoto katika utekelezaji na usimamizi wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma.
Katika andiko la kutafakari miaka 10 tangu kuanzishwa kwa APRM ambayo Tanzania pia ni moja ya nchi wanachama tena hai, wataalamu wa masuala ya utawala bora walioongozwa na mnazi mkubwa wa sera za Mwalimu Nyerere, komredi wangu Prof. Ahmed Muhiddin wa Kenya wanasema katika kijitabu chao “African Peer Review Mechanism; Best Practices and Lessons Learnt” (2013) kuwa Afrika imeponzwa sana na eneo hili la utekelezaji na ni gonjwa la kutafutiwa dawa.
Kwa hakika kwa maoni ya watafiti hawa (empirical evidence) na hata hali halisi (observed reality)  tunayoiona katika siku na zama hizi hatupaswi kubaki tukifungwa minyororo na historia. Historia inapaswa kutoonesha makosa yetu ya jana, kutusaidia tuyarekebishe leo ili tuwe na kesho bora zaidi.
Kwa kuwa watafiti wote hawa wanakubaliana kuwa kuna mahali tulikosea katika nadharia yetu ya maendeleo, si kosa kuweka mikakati ya kurekebisha hali hii. Mwalimu Nyerere alisema katika “TUJISAHIHISHE” kuwa kujikosoa ni kujisahihisha.
Hivyo basi kwa nchi yetu kuichukua falsafa hii iliyopimwa na kuthibitishwa kuwa na manufaa (tested delivery model) kutoka kwa ndugu zetu Malaysia, kuiweka katika mazingira ya Kitanzania, kwangu mimi ni HATUA KUBWA.
Nimepata kukutana na Dr. Omar Abdulrahman mmoja wa watu walioisaidia sana Malaysia tunayoisikia sasa na pia mmoja ya vichwa nyuma ya Mpango kama huu wa Big Results huko Malaysia.
Kwa wasiomfahamu, Dr. Omar ndiye aliyekuwa mshauri mkuu wa Waziri Mkuu maarufu sana wa Malaysia, Dr. Mahathir Mohammed katika eneo la teknolojia kwa maendeleo.Akitoa siri ya mafanikio ya Malaysia anasema ni kuchagua, kupanga na kutekeleza.
Ukikutana na watu walioyaona haya kivitendo kama Dr. Mahathir mwenyewe na CEO wa sasa wa Kitengo cha Kusimamia Utekelezaji (PEMANDU) kule Malaysia, Prof Idris Jalla wote watakwambua siri hiyo hiyo kwamba kama unataka maendeleo ya haraka lazima uchague maeneo mahsusi, uyawekee mkakati na kisha utekeleze ipasavyo.
Ninachokiona hapa kuhusu wasiwasi unaoanza kujitokeza ni umuhimu mkubwa wa jamii kufahamishwa muktadha, maudhui na hata hatua na mafanikio ya mabadiliko haya yote ninayoamini yana manufaa kwa jamii yote.
Nasema hivi kwa sababu naamini kuwa Serikali au taasisi inaweza kupanga na kufanya makubwa lakini si tu yasionekane bali msingi na mantiki yake ukakumbana na ushindani mkubwa kwa sababu tu watu hawana ufahamu.
Ni changamoto kwa wanamipango walioko nyuma ya BRN na hata PDB kuweka mkakati maalum wa mawasiliano kwa umma, mkakati utakaotekelezwa kwa weledi ili wananchi wafahamu tena katika kila hatua kwa nini BIG RESULT ni MATOKEO MAKUBWA na si MAJANGA MAKUBWA (kama jamaa yangu mmoja alivyokwenda mbali na kuuita hivyo).
Mkakati huo utakuwa unajibu maswali magumu ya wananchi kila siku lakini pia utakuwa ndio hasa majibu kwa wasiwasi uliowajaa watu wengi waliofungwa minyororo na mfumo wa zamani waliouona haukuwa na ufanisi sana.
Hivyo naungana na Balozi Sefue kuwa tusifungwe minyororo na historia, nisisitize pia kuwa ni vyema tukaungana kama Taifa katika kutekeleza mipango yetu kuliko kuendelea kuacha utekelezaji ukitetereka kama ilivyokuwa katika mifumo ya awali.
*Mwandishi ni mtaalamu wa masuala ya mawasiliano na sheria. Kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano katika Mpango wa Afrika Kutathmini Utawala Bora (APRM Tanzania).Maoni 0713 584467.Baruapepe: habbas@aprmtanzania.org


No comments:

Post a Comment