Monday, August 12, 2013

MWANAFUNZI ALAZIMISHWA NGONO BILA KONDOMU NA MAJANGA MENGINE WILAYANI MAKETE

Kata ya Iwawa ilipo shule hiyo.
 
Na Edwin Moshi wa Globu ya Jamii, Makete
Wafunzi wa shule ya sekondari Iwawa wilayani Makete mkoani Njombe wamekiri uwepo wa wanafunzi wenzao ambao wanajihusisha na vitendo vya ngono na wengine wanaishi na virusi vya UKIMWI, licha ya jamii kudhani kuwa wanafunzi hawawezi kuwa na virusi hivyo kwa minajili kwamba bado ni wadogo.
Hayo yamebainika baada ya mtandao huu kufanya mahojiano ya kina na baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hivi karibuni kwa ruhusa ya mkuu wa shule hiyo Bw. Christopher Haule hapo kufuatia wananchi wengi wilayani hapo kudhani kuwa wanafunzi hao hawana maambukizi ya vvu kwa kuwa ni wadogo na huwenda hawajaanza kujihusisha na vitendo vya ngono.
Mwanafunzi mmoja (jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) amesema ana marafiki zake zaidi ya watano ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI na hajui walivipataje, hivyo anaamini wapo wanafunzi wengi ambao wana maambukizi.
Amesema jamii inapaswa kuondokana na dhana potofu kuwa mabinti ama vijana wadogo hawana vvu waache mara moja kwa kuwa virusi vinampata mtu yeyote bila kujali umri.
“Mtu anayedhani kuwa wanafunzi huwa hawana vvu ni uongo, na pia waanatakiwa kuacha kujihusisha kimapenzi na wanafunzi kwa madai kuwa hawana vvu, lakini wakumbuke sheria za nchi haziruhusu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi, jamani Ukimwi upo kwa kila mtu” alisema mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi mwingine amesema yeye hafahamu kama wanafunzi hao wenye vvu wanajihusisha kimapenzi na watu kwa kuwa wapo ambao wanaishi na wazazi wao na wengine wamepanga kwenye nyumba maarufu kama mageto ambao kwa kiasi kikubwa wako huru kufanya mambo yao kwa kuwa hawana muangalizi.
“Ni kweli kabisa wapo wanafunzi wenye vvu wanaoishi wenyewe kwenye mageto, lakini mimi sijui kama wana wapenzi ama lah, maana ni ngumu kujua na mimi sipo hapa kwa ajili ya kufuatilia maisha ya mtu, na hao ninao kwambia kwa kuwa ni marafiki zangu na waliwahi kuniambia kuwa wanaishi na vvu” alisema mwanafunzi huyo(jina tunalo)

Mmoja wa mwanafunzi aliyezungumza na mtandao huu
 
Mwanafunzi upande wa kushoto wa picha hii amemweleza mwandishi wetu kuwa mpenzi wake anamlazimisha kufanya mapenzi bila kondomu
 
“Mimi kwa upande wangu Kusema kweli nina mpenzi na nilishawahi kupima vvu mwaka jana (2012) na kujikuta sina maambukizi namshukuru Mungu kwa hilo, na pia nimekuwa nikifanya mapenzi kwa kutumia kondomu lakini kuna wakati mwingine hatutumii mimi na mpenzi wangu na mara nyingi yeye ndiyo ananishawishi tusitumie, na huyo mpenzi wangu si mwanafunzi ni jamaa tu wa pale mtaani kwetu, na mimi huwa nakwenda home kwake(Nyambani kwake) na wakati mwingine anakuja geto kwangu, ili atumie kondom huwa namwambia leo ni siku zangu za hatari, hapo ndipo atavaa kondomu” alisema mwanafunzi huyo wa kike ambaye anaishi kwenye nyumba ya kupanga.
Akizungumzia suala hilo, diwani wa kata ya Iwawa Benjamin Mahenge alikiri kuwepo kwa tatizo la ukimwi kwa kila mtu, na kuongeza kuwa hata wanafunzi wapo wenye vvu ingawa ni kwa kiasi kidogo ukilinganisha na miaka iliyopita na pia wapo wanafunzi wanaojihusisha na vitendo vya ngono, na ambao wameshabainika wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria
Diwani wa kata ya Iwawa Benjamin Mahenge (kushoto) akizungumza na mwandishi wa habari hizi
"Unajua ni ngumu mwanafunzi kuniambia mimi ama kiongozi mwingine kuwa anajihusisha kimapenzi na mtu lakini kwako mwandishi kasema, mimi ninaomba wawe wawazi ili tuweze kuwasaidia hasa pale linapojitokeza tatizo hasa mimba kwa kuwa hawawataji wahusika" alisema Mahenge
Mahenge amesema huu ni muda wa jamii kubadilika na kuondokana na dhana potofu kuwa wanafunzi hawawezi kuwa na vvu, na pia wawaache wanafunzi hao wasome na si kuwarubuni na kujikuta wakifanya nao mapenzi
Pia amesema wapo wanafunzi katika kata yake ambao wamepanga na uangalizi wao si mzuri kwa kuwa wanajiamulia mambo yao wenyewe hata kama si mazuri kutokana na kukosa uangalizi wa watu wazima.
 “Unakuta mwanafunzi kajipangia kwenye chumba chake, yeye ndio kila kitu, akitaka kusoma haya, akitaka kwenda disco hakuna wa kumuuliza, hii ni hatari pia” alisema Mahenge
 
 Moja ya nyumba iliyoko Makete mjini amayo wanafunzi wamepanga
 

No comments:

Post a Comment