Thursday, December 27, 2012

Vodacom yaupa nguvu Mradi wa Mbwa Mwitu

Rais Jakaya Kikwete akionesha mbwa mwitu(hawapo pichani) wanavyorejea katika hifadhi ya Serengeti mara baada ya kuachiwa kutoka katika banda maalum walilokuwa wamehifadhiwa ikiwa ni awamu ya pili ya kundi la mbwa hao chini ya Mradi wa Uhifadhi na Ulinzi wa wanyama hao walio katika hatari ya kutoweka. Vodacom Foundation hadi sasa imeshatumia zaidi ya Sh 450 Milioni kufadhili mradi huo kama sehemu ya kuchangia maendeleo ya sekta ya Utalii nchini. Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Tifa - TANAPA Allan Kijazi, Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Vodacom Tanzania Salum Mwalim na Meneja wa Vodacom Foundation Grace Lyon. 
Rais Jakaya Kiwete Kikwete akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani)katika eneo la Nyamuma ndani ya hifadhi ya taifa ya Serengeti mara baada ya kuongoza zoezi la kuwaruhusu mbwa mwitu kumi na watano kurejea hifadhini baada ya kuwa chini ya uangalizi maalum kupitia mradi wa Uhifadhi na Ulinzi wa Wanyama hao walio katika hatari ya kutoweka. Vodacom Foundation hadi sasa imeshatumia zaidi ya Sh 450 Milioni kufadhili mradi huo kama sehemu ya kuchangia maendeleo ya sekta ya Utalii nchini.

Kampuni ya Vodacom imesema itaendelea kutoa ushirikiano katika juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika miradi inayolenga kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi na wananchi wake.

Hayo yamesemwa na Meneja Mahusiano ya Nje wa Kampuni hiyo Salum Mwalim wakati wa zoezi la kuwaachia kundi la pili la Mbwa Mwitu kumi na tano katika eneo la Nyamuma ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwishoni mwa wiki.

Mbwa hao walikuwa chini ya uangalizi maalum wa mradi wa Uhifadhi na Ulinzi wa Wanyama hao ambao wapo katika hatari ya kutoweka katika hifadhi hiyo tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini kutokana na sababu mbalimbali.

“Kampuni ya Vodacom imekuwa ikiunga mkono juhudi mbalimbali za kimaendeleo kupitia uwajibikaji kwa Jamii – CSR chini ya mfuko wake wa kusaidia Jamii - Vodacom Foundation na kwamba inaunga mkono juhudi zote zinazochukuliwa katika kuchochea maendeleo ya nchi na wananchi.”Alisema Mwalim.

Akizungumzia mradi huo wa Mbwa Mwitu Mwalim amesema Vodacom imeshatumia zaidi ya Sh. 450 Milioni kufadhili mradi huo tangu mwaka 2010 kwa kutambua umuhimu na mchango wa sekta ya Utalii hapa nchini.

“Vodacom imekuwa mfadhili mkuu wa meradi huu tangu ulipoanzishwa na inafanya hivyo kutokana na umuhimu wa Hifadhi ya Serengeti katika sekta ya Utalii na mchango wake katika maendeleo ya nchi hii.”Alisema Mwalim.

“Tunapoowaangalia wanyama hawa tunaweza tusione jambo muhimu ndani yake lakini kwa kuangalia umuhimu wa sekta ya Utalii na mchango wake katika pato la taifa kwa wakati huu ni wazi kwamba kila jambo linaloongeza thamani ya hifadhi zetu ni la msingi kwa mustakabali wa uchumi wa nchi yetu.”Aliongeza Mwalim wakati akizungumza katika hafla hiyo iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

Mbali na ufadhili wa fedha, teknolojia ya mtandao wa Vodacom ndio inayotumika kufuatilia maisha ya wanyama hao mara baada ya kuachiwa huru kupitia vifaa maalum wanavyofungwa mbwa hao kuwezesha kazi ya ufuatailiaji kwa njia ya Satelite.

“Tumewezesha teknolojia ya simu ya mtandao wa Vodacom pia kutumika kuwezesha ufuatiliaji wa maisha ya mbwa hawa mara baada ya kuachiwa huru ili kutopoteza rekodi za maedneleo yao hifadhini.”Alisema Mwalim.

Lengo la mradi wa uhifadhi Mbwa Mwitu ni kurejesha viumbe hao katika hali yake ya kawaida katika hifadhi ya Serengeti baada ya kutoweka mwanzoni mwa miaka ya tisini.

Chini ya mradi huo viumbe hao hushikwa na kutunzwa ndani ya boma maalum ili kuwawezesha kuzaliana na hatimae huachiwa huru kuendeleza maisha asilia katika hifadhi ya Serengeti. Lengo ni kufikisha idadi ya Mbwa Mwitu sitini ambao kuanzia hapo watakuwa na uwezo wa kuendeleza vizazi ndani ya hifadhi hiyo.

Kwa mujibu wa mratibu wa mradi huo Emmanuel Massenga Hifadhi ya taifa ya Serengeti inakadiriwa iliwahi kuwa na zaidi ya mbwa mwitu mia tano kabla ya kuanza kutoweka hadi kufikia hatari ya kutoweka kabisa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo magonjwa na kuuawa na wananchi.

Jumla ya Mbwa Mwitu Kumi na mmoja waliachiwa Agosti mwaka huu chini ya mradi huo na hivyo kufanya idadi ya mbwa mwitu hao ndani ya hifadhi ya Serengeti kwa sasa kufikia ishirini na sita.

Zoezi la kuachiwa huru kwa kundi la pili la mbwa mwitu hao liliongozwa na Rais Jakaya Kikiwete ambapo ametaka kujitokeza kwa wadau zaidi kusaidia mradi huo.

No comments:

Post a Comment