Friday, October 19, 2012

TANZANIA YAISHAURI ICC KUJIEPUSHA NA USHAWISHI WA KISIASA

Balozi wa Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi akizungumza wakati wa mjadala wa wazi ulioandaliwana Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na kufunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon. Mjadala huo ulihusu uhusiano kati ya Amani na Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) miongoni mwa mambo aliyosisitiza Balozi Manongi ni pamoja na kuishauri ICC kutenda haki bila kuegemea upande wowote na kwamba ijitahidi kujiepusha na ushawishi wa kisiasa kutoka nchi yoyote ile likiwamo Baraza Kuu la Usalama.
Wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mkutano wake wa wazi uliokuwa ukijadili uhusiano kati ya Amani na Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai. 
 
Na Mwandishi Maalum 

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) imeshauria kutekeleza majukumu yake bila ya kushawishi wa kisiasa kutoka nchi yoyote ile likiwamo Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ushauri huo umetolewa na Tanzania kupitia Balozi wake wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Matiafa, Tuvako Manongi, wakati wa mjadala wa wazi uliohusu uhusiano kati ya Amani na Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC). 

Mjadala huo uliandaliwa na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa. Akizunguma katika mjadala huo uliofunguliwa na katibu Mkuu wa UM, Ban Ki Moon, Balozi Manongi amesema, ili Mahakama hiyo iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo inapashwa kujiepusha na ushawishi au mashikinikizo ya kisiasa. 

Akafafanua kwamba, kwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo zimekwisha kuitambua mahakama hiyo, inategemea na inaamini kwamba itatekeleza majukumu yake bila ya upendeleo wa aina yoyote ile. 

 Akaeleza wazi kwamba nchi nyingi hasa zile za Afrika zimekuwa zikionyesha wasi wasi wao juu ya mwenendo wa Mahakama hiyo licha ya ukweli kuwa , nchini nyingi za Afrika siyo tu zimeitambua lakini masuala mengi yanayoshughulikiwa na makahama hiyo yanaihusu Afrika. “ Uhuru wa kutoadhibiwa lazima uzingatiwe wakati wowote na mahali popote”. 

Anasema Balozi na kuongeza. “ Usemi kwa kwamba haki ni lazima itendeke, lakini vile vile lazima ionekane. Na huu ni ukweli kwa chombo chochote cha kisheria kama inavyotakiwa kufanyika pia katika ICC”. 

Akasisitiza. Na kuongeza kwamba ili haki hiyo itendeke na kuonekana ni lazima basi iwe kwa wote bilaya kujali au kuzingatia ushawishi wa kisiasa. Na kufafanua zaidi kwamba mataifa mengi ya Afrika yanaona kama vile uwajibishwaji katika ICC unalenga upande mmoja. Na hili ni tatizo ambalo linapelekea ICC kutopata ushirikiano wa kutosha. 

 Akaeleza kwamba majukumu ya Baraza Kuu la Usalama la UM na yale ya ICC kwa kiasi fulani yanashabihiana kutokana na kweli kwamba asilimia kubwa ya majukumu yao yanaihusu Afrika. “ Jukumu la kutafuta amani na haki ni jukumu la msingi kwa Baraza kuu na hali kadharika kwa ICC. Na mara nyingi imeelezwa kuwa amani haiwezi kuwapo bila haki. 

Na kwa hakika amani na haki ni kama pande mbili za sarafu zinazotegemeana, kwa sababu upande mmoja hauwezi kustawi bila ya mwingine” akasisitiza Balozi Manongi Na kuongeza lakini katika mazingira Fulani Fulani, Jumuia ya Kimataifa na Baraza kuu la Usalama zimejikuta zikilazimika kujaribu kutafuta uwiano kati ya pande hizi mbili hasa pale upande mmoja unapoonekana kuuelemea upande mwingine. “ Ndio maana haishangazi kwamba kitendo cha kutafuta uwiano kati ya haki na amani kumezua hofu kubwa. 

Kutokana na kwamba ni jambo lisiloingia akilini kwa mahakama kutafuta haki kwa gharama ya mchakato wa kutafuta amani. Hata kama itamaanisha kutoa unafuu wa muda kwa watuhumiwa kutochukuliwa hatua” akasema Balozi Na kusisitiza kwamba, mchakato wa kutafuta amani kwa namna yoyote ile usilinganishwe na uhuru wa kutoadhibiwa. 

Aidha amelitaka Baraza Kuu kuwa wazi zaidi kwa kutoa maelezo kwa nchi ambazo zimeomba uahilishaji wa mashtaka na hii itasaidia kuboresha ushirikiano na kuondoa hisia potofu dhidi ya ICC. Halikadharika Mwakilishi huyo wa Tanzania katika UM, anasema ICC si chombo pekee chenye jukumu la kutafuta haki kwa waathirika wa vitendo vya jinai. 

Kwakile alichosema hata nchi moja moja zinawajibu na haki ya kutafutua haki kwa waathirika kwakutumia taasisi zake za kisheria, kinachotakiwa ni kuzijengea uwezo wa kutekeleza jukumu hilo hasa kwa nchi zile ambazo zimetoka katika vita au machafuko. 

Kwa upande mwingine, Tanzania imelitaka Baraza Kuu kuisaidia ICC kwa maana ya raslimali ili iweze kutekeleza majukumu yake ya msingi na vile vile kuzishawishi nchi kutoa ushirikiano kwa mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment