Monday, June 20, 2011

BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA

Mhe.  Waziri Mkuu Peter Mizengo Pinda,
Tunaomba kuanza  kwa kukupa pole kwa majukumu mazito uliyo nayo katika ujenzi wa taifa letu. Pia tunakupongeza kwa uimara na ushupavu wako katika kusimamia masuala mbalimbali ya kimaendeleo nchini.
Mh. Mizengo Pinda
Mhe. Waziri Mkuu,sisi wanafunzi wa kitanzania katika Chuo Kikuu Cha Urafiki – Lumumba kilichopo jijini Moscow inchini Urusi tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kuweza kutupatia udhamini wa masomo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Kwani fursa hiyo ni moja ya njia za kuelimisha taifa  na pia kuongeza idadi ya watendaji bora katika sekta mbalimbali nchini.

Mhe. Waziri Mkuu, lengo kuu la waraka huu kwako ni kukufikishia malalamiko yetu moja kwa moja  juu ya kero mbalimbali tunazozipata kuhusiana na zoezi zima la mikopo hii tunayopatiwa na serikali yetu. Tumeamua kufikisha malalamiko haya kwako kwa sababu wahusika wakuu (WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI pamoja na BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU) hawataki kusikiliza kilio chetu. Tumeawaandikia barua nyingi sana kuhusiana na malalamiko yetu pasipo kujibiwa jibu lolote, na sisi hatuwezi kuendelea kukaa kimya huku tukizidi kuumia, wakati serikali ina kila sababu ya kutusikiliza kwani hii ni haki yetu ya msingi kabisa.

Mhe. Waziri Mkuu, malalamiko yetu ni haya yafuatayo:

1:UTARATIBU MBOVU WA MALIPO YA FEDHA ZA ADA.
Kila mwaka bodi imekuwa na utaratibu wa kutokulipa ada kamili za wanafunzi kwa wakati. Baadhi ya wanafunzi hufikia hatua ya kutoa fedha zao za kijikimu ili kufidia mapungufu hayo katika malipo ya ada.
Mfano:
Mwaka 2008/2009 baadhi ya wanafunzi walilazimika kulipa sehemu ya ada toka katika fedha zao za kujikimu. Na pia mpaka leo haijulikani sehemu ile ya ada za wanafunzi hao ilikwenda wapi licha ya kuuliza mara kwa mara juu ya suala hilo Wizarani na Bodi kwenyewe.
Mwaka huu 2010/2011, bodi imechelewa kutulipia ada kwa takrirban miezi 9 (kwani ada ilitakuwa kulipwa mwezi wa 9 mwaka jana(2010) lakini imekuja kulipwa mwaka huu wa 2011 mwezi wa 5, wakati ndiyo mhula wa pili unaisha. Na cha kusikitisha zaidi wanafunzi walio wengi wamelipiwa ada pungufu kwa zaidi ya dola 1000 kwa kila mwanafunzi, na wengine hawakulipiwa kabisa.
Mhe. Waziri Mkuu, hii ni kero kubwa sana kwani mara kwa mara tumekuwa tukifukuzwa madarasani kwa sababu hatujalipa ada. Tunadharirika sana. Na hata sasa baadhi yetu wametangaziwa kutokufanya mitihani yao ya kuhitimu shahada ya kwanza(degree) na wengine mitihani yao ya kufunga mwaka. Na hali hii hutokea kila mwaka.

2:MAKATO KATIKA FEDHA ZA KUJIKIMU
Mhe. Waziri Mkuu, tunasikitika sana kusema kuwa ni jambo lililozoeleka sasa kwa Bodi kutukata fedha zetu za kujikimu kila mwaka . na kila mara tunapodai kiasi kilichokatwa, wamekuwa wakisema fedha zinapungua kwa sababu ya rate of exchange pale wanapobadili fedha za kitanzania (shilingi) kwenda dola za kimarekani (USD), lakini cha ajabu ni kwamba wakati mwingine ada inapopungua bodi huwa inafidia kiasi kilichopungua. Je, ina maana fedha zetu za kujikimu tu ndizo zinazostahili kuathiriwa na rate of exchange na kutokufidiwa kiasi kinachopelea kila mwaka?

Mfano mzuri ni mwaka huu wa 2010/2011. Bodi imetuma kwa kila mwanafunzi fedha pungufu za kujikimu kwa wastani wa dola za kimarekani 477 na bado wakatueleza eti ni kwa sababu ya rate of exchange. Tumewaomba sana watutumie fedha hizo kwani sisi tunaathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na makato hayo, lakini mpaka leo hatujapatiwa jibu lolote wala hatuoni dalili zozote za suala letu hilo kushughulikiwa na Bodi ya mikopo wala Wizara ya elimu.

3:KUTOKUTUMIWA FEDHA ZA BIMA YA AFYA .
Mhe. Waziri Mkuu, mwaka huu wa 2010/2011, serikali haikutupatia kabisa fedha za kulipia bima ya afya. Kwa masharti ya chuoni na Nchini urusi, mwanafunzi kama HUJALIPIA BIMA YA AFYA HUWEZI KUPATIWA HUDUMA YOYOTE ILE YA AFYA, HUWEZI KURUHUSIWA KUFANYA USAJILI WALA KUPATWA VIZA(kila mwaka huwa tunahitajika kuomba viza mpya  na kufanya usajili ili tuweze kuruhusiwa kuendelea na masomo kwa mwaka unaofuata). Licha ya kuikumbusha wizara na bodi juu ya kutupatia fedha hizo, lakini mpaka leo mwaka unaelekea kuisha hatujapatiwa fedha hizo wala hakuna jibu la aina yoyote ile.

4:MWAMBATA WA ELIMU.
Mhe. Waziri Mkuu, ni miaka mingi sasa imepita tangu tuanze kuiomba wizara kutuletea mwambata wa elimu nchini urusi. Matatizo yetu mengi yanachelewa sana kupatiwa ufumbuzi na wakati mwingine yanashindikana  kabisa kupatiwa ufumbuzi kwa sababu hatuna mwambata wa elimu nchini urusi. Mara kwa mara tumelazimika kupeleka matatizo yetu kwa maofisa wa ubalozi ambao nao pia wana majukumu yao mengine tofauti tofauti, tunashukuru wamekuwa wakijitahidi kutusaidia. Lakini kukosekana kwa Mwambata wa elimu bado ni tatizo kubwa sana linalotuathiri wanafunzi nchini urusi.

5: OMBI LA NYONGEZA KATIKA FEDHA ZA KUJIKIMU.
Mhe. Waziri Mkuu, mara kwa mara tumekuwa tukiilalamikia na kuiomba Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi stadi kutupatia nyongeza ya fedha za kujikimu pasipo mafanikio yoyote. Mji tunaoishi (MOSCOW) ni mojawapo ya miji ghali sana duniani, maisha yetu huku yameendelea kuwa duni sana na wakati mwingine tunashindwa hata kupata baadhi ya huduma muhimu. Mara kwa mara tumeijulisha wizara ya elimu, na hata tumeweza kuipatia michanganuo inayoonesha jinsi fedha wanazotupatia kwa sasa zinaishia katika kulipia mambo mbalimbali ya lazima na wakati mwingine tunabakiwa na kiasi kidogo sana cha pesa ambacho ndicho tunalazimika kukitumia kwaajili ya chakula(japokuwa wengi wetu tunakula aidha mlo moja au miwili tu  kwa siku). Kwa kweli tunaiomba serikali kutufikiria katika jambo hili kwani hali tuliyonayo kwa sasa ni mbaya sana, pia ikizingatiwa kuwa nchini Urusi KILA MWAKA MWEZI WA 9 BEI ZA BIDHAA NA GHARAMA ZA HUDUMA MBALIMBALI HUPANDISHWA na hivyo kuzidi kutuathiri zaidi sisi wanafunzi wa kigeni.

Mhe. Waziri Mkuu, tunatumaini kuwa malalamiko, vilio na maombi yetu, utayapokea na kuyafanyia kazi mapema. Tunakutakia afya tele na mafanikio mema katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa letu.

Asante sana.

WANAFUNZI WA KITANZANIA - CHUO KIKUU CHA URAFIKI LUMUMBA, MOSCOW-URUSI.

No comments:

Post a Comment