Friday, December 14, 2018

TANZANIA YAFUNGUA OFISI NDOGO YA UBALOZI HONGKONG CHINA

Na Grace Semfuko-MAELEZO
Tanzania imefungua ofisi ndogo ya kibalozi Hongkong nchini China ambayo itahudumia masuala ya kidiplomasia na kuongozwa na Balozi wa Heshima wa Tanzania Dkt Annie Wu alieteuliwa Septemba 2 mwaka huu na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wakati alipohudhuria mkutano wa wa mahusiano ya China na Afrika,  FOCAC huko Beijing nchini China.

Ofisi hiyo mpya  katika jiji la  Hongkong,  nchini China itasimamia masuala ya kibalozi na kuwasogezea karibu huduma hizo, tofauti na hapo awali ambapo huduma za kibalozi zilikuwa zikipatikana Beijing.

Akizungumza Jijini Hongkong nchini China jana, Balozi wa Tanzania nchini humo, Mbelwa Kairuki, alisema ni fursa kwa watanzania na wachina kutumia ofisi ya Hongkong kupata huduma mbalimbali katika ofisi hiyo kwa urahisi.

Kwa upande wake Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini China, Dkt. Annie Wu ameonyesha kufurahishwa kuaminiwa na Serikali ya Tanzania kwa majukumu hayo ya heshima aliyopewa na kuihakikishia  serikali kuwa pamoja na mambo ya kidiplomasia, ataitangaza Tanzania kwa wawekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Aidha amewakaribisha wadau wote watembelee ofisi mpya ya Tanzania ili kupata taarifa husika kuhusu utalii, biashara na uwekezaji  kwa manufaa ya  Tanzania na China.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha uwekezaji Tanzania, Bw Geoffrey Mwambe amesema kufunguliwa kwa Ubalozi huo kutasaidia kuongeza uwekezaji zaidi, Kwani wafanyabiashara wa China watatumia Ubalozi huo katika kufuatilia masuala ya uwekezaji.

Balozi Dkt. Annie Wu, ambaye ni mtu mashuhuri nchini China na Hongkong anasifika kwa kuitangaza Tanzania kwenye masuala mbalimbali yakiwepo ya kibiashara na uwekezaji, pia aliwahi kuandaa makongamano ya kibiashara, yaliyojenga mahusiano ya uwekezaji  baina ya China na Tanzania, ambapo atahudumu kwenye nafasi hiyo ya Ubalozi wa Heshima-Hongkong kwa miaka mitano.

Kwa mujibu wa kituo cha uwekezaji Tanzania, TIC-China, China inaendelea kuongoza duniani kwa kuweka mitaji mikubwa nchini Tanzania; kwa zaidi ya dola Bilioni 5.8,  kuanzia mwaka 1990 mpaka 2017, ambapo kuna jumla ya miradi 723, huku ikitoa ajira 87,126 kwa thamani ya dola Milioni 5 962.74, ikifuatiwa na Uingereza, yenye miradi 936 ya thamani ya dola Milioni 5,540.07, iliyozaa ajira 274,401, na Marekani ikiwa na miradi 244 ya thamani ya dola 4,721.15, iliyozalisha ajira 51,880.

Tawimu hizo za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zimebainisha kuwa China inaendelea kuwa nchi yenye lengo la kuwekeza zaidi katika maeneo mbalimbali hapa nchini, yakiwemo  kilimo, viwanda, utalii, Ujenzi, Teknolojia ya Mawasiliano na maeneo mengineyo .

No comments:

Post a Comment