Wednesday, December 12, 2018

RC MTAKA ATEKELEZA AGIZO LA RAIS, KUWAGAWIA VITAMBULISHO WAJASIRIAMALI WADOGO



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera boksi lenye vitambulisho vya wajasiliamali wadogo, ikiwa ni utekezelaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa kwa Wakuu wa Mikoa wote nchini, kuwapa vitambulisho hivyo wajasiliamali wadogo ambao mauzo yao ni chini ya milioni nne kwa mwaka, ili vitambulisho hivyo viweze kuwafikia wajasiriamali hao mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga boksi lenye vitambulisho vya wajasiliamali wadogo, ikiwa ni utekezelaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa kwa Wakuu wa Mikoa wote nchini, kuwapa vitambulisho hivyo wajasiliamali wadogo ambao mauzo yao ni chini ya milioni nne kwa mwaka ili vitambulisho hivyo viweze kuwafikia wajasiriamali hao mkoani Simiyu.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani boksi lenye vitambulisho vya wajasiliamali wadogo, ikiwa ni utekezelaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa kwa Wakuu wa Mikoa wote nchini, kuwapa vitambulisho hivyo wajasiliamali wadogo ambao mauzo yao ni chini ya milioni nne kwa mwaka ili vitambulisho hivyo viweze kuwafikia wajasiriamali hao mkoani Simiyu.





Na Stella Kalinga, Simiyu


Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo, ambapo amewakabidhi Wakuu wa Wilaya na Maafisa Biashara wa Halmashauri mkoani hapa jumla ya vitambulisho 25,000, vitakavyotolewa kwa wajasiriamali wadogo wenye mauzo pungufu ya milioni nne kwa mwaka.

Akikabidhi vitambulisho hivyo Mtaka amesema vitawasaidia wajasiriamali wadogo kutambuliwa,kuwajengea ujasiri na uthubutu na kuwafanya kunufaika na fursa mbalimbali huku akibainisha kuwa vitachangia pia kuwaibua wajasiriamali wapya mkoani Simiyu.

Ameongeza kuwa Simiyu imejipanga kuwafikia wajasiriamali wote wadogo kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais, huku akiwaonya na kuwatahadharisha wafanyabiashara wakubwa wanaotambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutojaribu kujipatia vitambulisho vya wajasiriamali wadogo kwa njia ya udanganyifu.

“Niwatahadharishe wafanyabiashara wasije wakatumia nafasi ya vitambulisho hivi vya wajasirimali wadogo, kufanya udanganyifu wowote wa wao kuvitumia vitambulisho hivyo kujitambulisha kama wafanyabiashara wadogo; huu udanganyifu hatutaupa nafasi na sisi kama Serikali tumejiandaa kuainisha kila mtu anachofanya, mahali anapokaa, historia yake ya biashara”

“Ofisi za Wakurugenzi zitatoa magari yatakayowawezesha maafisa Biashara kwenda vijijini kuwafikia wajasiamali wadogo,tunaamini walengwa wa vitambulisho hivi ni wale ambao nauli ya kule aliko na Makao Makuu ya Wilaya inaweza kuwa ndiyo fedha inayohitajika achangie kupata kitambulisho hicho,kwa hiyo kuna kadi zitabaki wilayani lakini nyingine zitapelekwa mahali walipo walengwa” alifafanua Mtaka.

Baadhi ya wakuu wa wilaya wakizungumza mara baada ya kupokea vitambulisho hivyo wamesema watahakikisha vinawafikia walengwa waliokusudiwa na hakutakuwepo na udanganyifu wowote katika zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo.

“Niwahakikishie wajasiriamali wadogo wote kuwa watapata vitambulisho kama Mhe Rais alivyoelekeza na nitoe wito kwao kuja kuchukua vitambulisho hivi ili asiwepo mtu yeyote wa kuwabugudhi na wafanye kazi zao kwa uhuru” Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga

“ Niwatoe hofu wajasiriamali wote wadogo kuwa kila aliye na sifa ya kupata kitambulisho hiki atapata na kwa wale wanaodhani watatumia vitambulisho hivi kukwepa kodi nichukue nafasi hii kutoa onyo kuwa hatutavumilia udanganyifu wa aina yoyote” Mkuu wa Wilaya ya Busega,Mhe. Tano Mwera.

Baadhi ya wajasiriamali Wadogo Mkoa Simiyu wameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutoa vitambulisho hivyo ambavyo vitawaondolea adha mbalimbali walizokuwa wakizipata ikiwepo ya kuogopa kufanya biashar zao kutokana na kutotambuliwa rasmi.

“ Tanamshukuru sana Rais ametupa ujasiri wa kufanya biashara zetu kwa uhuru maana kuna watu walikuwa wanaogopa kufanya biashara kwa sababu ya kuogopa kodi, kupitia vitambulisho hivi tutafanya biashara kwa uaminifu, uhuru na ujasiri na katika wilaya yetu ya Bariadi, Tanzania ya Viwanda hasa vile vidogo itawezekana” alisema Bahati Kaitila mjasiriamali mdogo kutoka Bariadi.

“ Nimelipokea vizuri suala la kupewa vitambulisho kwa sababu vitatusaidia sisi wajasiriamali wadogo kupata ujasiri zaidi wa kufanya kazi zetu, tunaweza kuanza na kitu kidogo lakini baadaye tukafanya makubwa” alisema Grace Mukali mjasiriamali mdogo kutoka wilaya ya Bariadi.

No comments:

Post a Comment