Friday, December 14, 2018

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. KANYASU AIGIZA TFS ITATUE KERO YA USAFIRISHAJI VINYAGO KWA WATALII

LUSUNGU HELELA-WMU
Baada ya  malalamiko ya  Watalii walio wengi  kulazimika kuacha  vinyago kwenye viwanja vya ndege walivyokuwa wamevinunua kwenye maduka mbalimbali nchini kutokana na kukosekana kwa vibali kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) hatimaye  Naibu Waziri na Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu ameiagiza TFS iangalie namna bora  ya kutatua tatizo hilo kwa vile limekuwa likiwaletea usumbufu watalii.

Amelibainisha hilo wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano na Watumishi wa makao makuu wa Wakala wa Huduma za Misitu  Tanzania, jijini Dar es Salaam. Amefafanu kuwa  watalii wengi  hununua vinyago hivyo kwenye maduka mbalimbali hapa nchini kama zawadi ya kupeleka nchini kwao lakini  wanapofika kwenye viwanja vya ndege kwa ajili ya kusafiri navyo hudaiwa vibali vya kusafirishia  vinyago hivyo jambo ambalo huwalazimu kuviacha kutokana na usumbufu wanaoupata.

Amesema jambo hilo limekuwa likiwafanya watalii wengi kuondoka nchini wakiwa wamekasirishwa kutokana na utaratibu huo kutokuwa wazi huku wakiamini kuwa wamedhulumiwa mali yao. Amesema malalamiko hayo  sio mazuri licha ya kuwa TFS nia yake ni njema ya kuhakikisha kuwa lazima kuwe na vibali ya kusafirishia vinyago hivyo kwa ajili kuthibiti  uharibifu wa misitu.

Amesema TFS lazima ifanye mazungumzo na taasisi nyingine  ili kuweza kutatua kero hiyo ambayo imekuwa ikileta sintofahamu kwa watalii na sekta ya utalii kwa ujumla. Amesema ni rahisi kumpoteza  mteja (Mtalii) lakini huweza kuchukua hata zaidi ya miaka kumi kuweza kumrudisha mteja ambaye ulikuwa umempoteza.

Amesema nia ya TFS ni nje katika kulinda misitu lakini tatizo linaloonekana ni kwamba hakuna mawasiliano thabiti kati ya TFS na Taasisi zingine kuhusiana  na biashara ya vinyago. Amesema TFS ni lazima ikae meza moja na wauzaji wa vinyago pamoja na Taasisi za uhifadhi ili waweze kutatua kero hiyo wanayokumbana nayo watalii.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TFS, Dos Santos Silayo ameahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi ili kuwaondolea usumbufu watalii wanaokuwa wamevinunua vinyago hivyo. Hata hivyo amesema suala la uthibiti wa usafirishaji  vivyago lipo kisheria lakini kutokana na tatizo hilo atafanya mazungumzo na taasisi nyingine ili kuona namna bora ya kutatua kero hiyo.
  Naibu Waziri na Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumza na watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) wakati aliwapotembelea kwa ajili ya kuzungumza nao  ikiwa ni mara ya kwanza  tangu alipoteuliwa kushika nyadhifa hiyo.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dos Santos Silayo akiwasilisha taarifa kabla  Naibu Waziri na Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu  kuzungumza watumishi wa makao makuu wa  TFS, jijini Dar es Salaam.    
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dos Santos Silayo akifafanua jambo kabla   Naibu Waziri na Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu kuzungumza na Menejimenti ya  TFS, jijini Dar es Salaam.
  Baadhi ya watumishi wa Wakala wa  Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) wakimsikiliza Naibu Waziri na Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati ali[pokuwa akizungumza nao makao makuu ya TFS jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA-MNRT)

No comments:

Post a Comment