Thursday, November 1, 2018

LUGOLA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA VITUO VYA POLISI TABATA,BUGURUNI NA KUTOA MAAGIZO YA DHAMANA KUTOLEWE SAA 24

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akiingia Kituo cha Polisi Tabata, jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha polisi hicho kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini. Pia Lugola alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha polisi Buguruni jijini humo leo
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akiwaita majina watuhumiwa (hawapo pichani) waliopo katika mahabusu ya Kituo cha Polisi cha Tabata, jijini Dar es Salaam, leo, ili kujua aina ya makosa waliotuhumiwa pamoja na kujua muda waliokaa katika kituo hicho endapo imefika zaidi ya saa 24 bila kupewa dhamana. Pia Lugola alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha polisi Buguruni jijini humo leo. Lengo la ziara hiyo ni kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akimuhoji Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Tabata, jijini Dar es Salaam, Bakari Gothi (watatu kushoto) kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji kazi katika kituo chake, mara baada ya Waziri huyo kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo hicho leo. Pia Lugola alifanya ziara kama hiyo katika Kituo cha Polisi Buguruni jijini humo. Lugola anafanya ziara ya kushtukiza katika vituo mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati) akionyeshwa taarifa za watuhumiwa waliopo mahabusu ya Kituo cha Polisi cha Buguruni, jijini Dar es Salaam, leo, wakati Waziri huyo alipofanya ziara ya kushtukiza katika Kituo hicho kwa lengo la kufuatilia utendaji kazi. Pia Lugola katika siku hiyo hiyo alifanya ziara ya aina hiyo katika kituo cha polisi Tabata, jijini humo. Kulia ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Buguruni, Adam Maro.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati) akimpa maelekezo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, mara baada ya Waziri huyo kumaliza ziara yake ya kushtukiza katika Kituo cha Polisi cha Tabata na Buguruni jijini Dar es Salaam, leo. Lugola alisema lengo la ziara hiyo ni kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini. Kushoto ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Buguruni, Adam Maro. 
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


Na Felix Mwagara, MOHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara ya kushtukiza kituo cha Polisi Tabata na Buguruni vya jijini Dar es Salaam ili kujua kama maagizo yake aliyoyatoa katika vituo mbalimbali kama yameanza kufanyiwa kazi.

Waziri Lugola alianza ziara yake saa 2:45 asubuhi kwa kuibukia katika kituo cha Tabata na moja kwa moja alianza kuulizia mahudhurio ya wafanyakazi wote wa kituo hicho na kujua nani yupo kazini na nani hayupo na kwanini hajafika ofisini hapo kwa muda huo wa asubuhi.

Wakati alipokua kituoni hapo, pia Lugola alikichukua kitabu cha taarifa za watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu hiyo akiwahoji watuhumiwa kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.

Lugola baada ya kumaliza katika kituo hicho, saa 5:27 alielekea kimyakimya katika kituo cha Polisi cha Buguruni, na aliwahoji watuhumiwa waliopo mahabusu katika kituo hicho na kujua makosa mbalimbali yanayowakabili huku polisi wapepelezi wa tuhuma zao wakiwepo katika tukio hilo.

Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara yake, Lugola alisema, alitoa maagizo mbalimbali katika ziara zake nchini, hivyo anafuatilia kujua maagizo yake yameanza kufanyiwa kazi au bado baadhi ya vituo kama wameyapuuza.

“Lengo la hii ziara yangu ni kuboresha utendaji kazi wa vituo vya polisi nchini, sijaja kumuadhibu mtu mimi, hivyo msiwe na wasiwasi, bali kilichonifanya hapa nije nikufuatilia maagizo mbalimbali ambayo niliyatoa kama kweli mnayafanyia kazi,” alisema Lugola.

Maagizo aliyoyatoa mwezi miwili iliyopita katika ziara zake mikoa mbalimbali nchini ni kuhakikisha pikipiki zinaondolewa katika vituo vya polisi, dhamana zitolewe saa 24 ikiwemo Jumamosi na Jumapili, pamoja na polisi kutowabambikizia kesi wananchi.

Hata hivyo, Lugola alivipongeza vituo hivyo vya polisi vilivyopo wilayani Ilala na pia Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma alichokitembelea wiki iliyopita, kwa kuanza kuyafanyia kazi maagizo yake aliyoyatoa zikiwemo baadhi ya bodaboda, zimeondolewa vituoni na zilizobaki zina kesi mahakamani.

“Nilifanya ziara ya kushtukiza pale Kituo cha Polisi cha Tabata, na pia nimekuja hapa Buguruni, kwakweli wameaanza kuyafanyia kazi maagizo yangu, pikipiki zote nilizozikuta zinasababu yakuwepo hapo, na si vinginevyo kama walivyokua wanaziweka kiholela hapo awali,” alisema Lugola.

Pia lugola aliwataka Makamanda wa polisi nchini kuwafuatilia askari wao kwa umakini ili kujua utendaji kazi wao, na pia Waziri huyo alisema atakua anafanya ziara kama hizo mara kwa mara hivyo vituo vya polisi nchini viwe sawa muda wote.

“Hamjui siku wala saa ambapo nitakuja, tufanye kazi, tuwahudumie wananchi, tusiwaonee wananchi, tujitume kufanya kazi kwa weledi, sitamvumilia mtu ambaye atavunja utaratibu,” alisema Lugola.

No comments:

Post a Comment