Thursday, October 4, 2018

TUME YA MADINI YATOA LESENI MPYA ZA MADINI 7879 KAMPUNI NYINGI ZAZIDI KUJITOKEZA KWENYE UWEKEZAJI WA MADINI



Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula (kushoto) akielezea takwimu za leseni zilizotolewa na Tume ya Madini tangu kuanzishwa kwake kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dodoma mapema tarehe 04 Oktoba, 2018. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula (katikati) akitoa ufafanuzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya na kushoto ni Mkurugenzi wa Leseni na TEHAMA wa Tume ya Madini, Torece Ngole



Na Greyson Mwase, Dodoma

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Mei hadi Septemba mwaka huu, Tume ya Madini, imetoa leseni 7879 ambazo maombi yake yaliidhinishwa kupitia kikao cha Tume kilichofanyika tarehe 25 Septemba, 2018 kilicholenga kujadili taarifa za Kamati za Tume na utendaji kazi katika kipindi cha mwezi Mei hadi Septemba, 2018.

Profesa Kikula ameyasema hayo leo tarehe 04 Oktoba, 2018 kupitia mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Tume ya Madini zilizopo jijini Dodoma.

Akielezea kuhusu maombi ya leseni za madini 7879 yaliyoidhinishwa katika kikao cha Tume, Profesa Kikula alieleza kuwa ni pamoja na Leseni za Utafutaji wa Madini (Prospecting License – (PL) 263; Leseni Kubwa (Special Mining License – (SML) 03;(ziliidhinishwa ili kupelekwa kwenye mamlaka husika ambayo ni Baraza la Mawaziri) Leseni za Uchimbaji wa Kati (Mining License – (ML) 14 pamoja na leseni 1 ya Sihia (Transfer) ya uchimbaji wa Kati.

Aliendelea kufafanua kuwa, maombi leseni za uchimbaji wa kati 14 yaliyopitishwa kuwa ni pamoja na kampuni za Dangote Industries Limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya chokaa katika eneo la Mtwara; Nazareth Mining Investment Co Limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) katika eneo la Ruangwa mkoani Lindi na kampuni ya Sunshine Mining (T) Limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini dhahabu katika eneo la Chunya mkoani Mbeya.

Aliendelea kutaja kampuni nyingine kuwa ni pamoja na Said Seif Abdallah kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya ujenzi katika eneo la Masasi mkoani Mtwara; Off Route Technologies (T) Limited kwa ajili ya uchimbaji wa makaa ya mawe katika eneo la Ileje mkoani Mbeya; leseni yenye ubia kati ya Shabani Daud Ibrahim, Andrew Bollen, Dunstan M. Mongi na Vedastus Mtesigwa kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu katika mkoa wa Geita.

Maombi mengine yaliyopitishwa ni pamoja na leseni yenye ubia kati ya Jumbo Limited, na Ally Mbarak Mohamed kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) katika eneo la Ruangwa mkoani Lindi, Jacana Resources (Tanzania) Limited kwa ajili ya uchimbaji wa mchanga bahari (mineral sand) katika eneo la Temeke lililopo jijini Dar es Salaam na P. B. Mining Company kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya fedha, dhahabu, shaba, zinki na galena katika eneo la Chunya lililopo mkoani Mbeya.

Profesa Kikula alisisitiza kuwa, kikao hicho pia kilipitisha ombi la kubadili umiliki kutoka kwa Mbarouk Saleh Mbarouk kwenda katika kampuni ya M. B. Mining (T) Limited kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya ujenzi katika eneo la Morogoro.

Profesa Kikula aliendelea kutaja maombi ya leseni nyingine zilizopitishwa katika kikao hicho kuwa ni pamoja na Leseni za Uchimbaji Mdogo (Primary Mining License – (PML) 6313; Leseni za Uchenjuaji wa Madini (Processing License) 08 na leseni za Biashara ya Madini ambapo leseni kubwa (Dealers License) ni 557; na leseni Ndogo (Broker’s License) 720

Katika hatua nyingine Profesa Kikula alisema kuwa, Mipango ya Ushirikishwaji wa Utoaji wa Huduma na Bidhaa kwa Wazawa katika Miradi ya Madini (local content plan) 19 ilipitishwa kati ya mipango 26 iliyowasilishwa kutoka katika kampuni mbalimbali za utafutaji na uchimbaji wa kati na mkubwa wa madini.

Alielekeza waombaji leseni za madini kuwasilisha mipango yao kwa wakati ili iweze kupitiwa na kamati husika na kuwezesha leseni kutolewa mapema. Pia aliwataka waombaji wote wa leseni za madini kufuatilia leseni zao kwenye Ofisi za Madini zilizopo mikoani walikoombea leseni zao na kusisitiza kuwa orodha ya leseni zilizoidhinishwa inapatikana katika tovuti ya Tume.

Wakati huohuo Profesa Kikula alisema kuwa Tume ya Madini imejipanga katika kuhakikisha kila mtanzania ananufaika ipasavyo na rasilimali za madini nchini
Aliongeza kuwa, Tume imeweka mikakati ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwatengea maeneo kwa ajili ya uchimbaji madini na kuwataka kuunda vikundi na kusajiliwa kupitia viongozi wao hivyo kuwezesha upatikanaji wa leseni za madini na kufanya shughuli zao pasipo kikwazo chochote.

“Sisi kama Tume ya Madini tunatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo wa madini na ndio maana tumekuwa tukifanya ziara katika maeneo ya wachimbaji wadogo na kutatua changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na migogoro; tunataka wafanye kazi katika mazingira salama kabisa,” alisema Profesa Kikula.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akielezea mchango wa Sheria Mpya ya Madini alisema kuwa tangu kuanza kwa utekelezaji wa sheria mpya iliyoweka ongezeko la kutoka asilimia nne hadi sita za mrabaha na tozo la asilimia moja la kodi ya ukaguzi wa madini, makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 194 hadi shilingi bilioni 301 kwa mwaka likiwa ni ongezeko la asilimia 55.

Pia, Mkurugenzi wa Leseni na TEHAMA kutoka Tume ya Madini, Torece Ngole akielezea mikakati ya Tume katika kukabiliana na changamoto ya migogoro kwenye uchimbaji wa madini inayosababishwa na wachimbaji wadogo kwa kuvamia maeneo yenye leseni kubwa, alisema kuwa Tume imeshaanza kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mpaka sasa imeshatenga maeneo 74

Alisisitiza kuwa Tume imekuwa ikiwaelimisha wachimbaji wadogo kuhusu sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuunda vikundi ili waweze kupatiwa maeneo na leseni za uchimbaji madini.

No comments:

Post a Comment