Sunday, October 28, 2018

SHERIA MPYA YA PSSSF NA SULUHISHO LA “FAO LA KUJITOA

Kwa kipindi kirefu kumekuwepo na changamoto ya kimtazamo kati ya dhana ya Hifadhi ya Jamii na Fao la kujitoa, Changamoto hii kwa kiasi kikubwa inasababishwa na uelewa mdogo miongoni mwa wanachama na wadau wa sekta ya Hifadhi ya Jamii. Suala hili limepelekea malalamiko mengi huku wengine wakijutia kuchangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Ili kulielewa jambo hili kwa mapana yake nianze kwa kuelezea dhana ya Hifadhi ya Jamii kama utaratibu unaowekwa na Jamii kwa lengo la kuwapatia wanajamii kinga dhidi ya majanga ya kiuchumi na kijamii yanayosababisha upungufu au upotevu wa kipato kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ugonjwa, ukosefu wa ajira, ulemavu na uzee. Kuna aina mbili za mifumo ya hifadhi ya jamii ambayo ni mifumo rasmi na mifumo isiyo rasmi. Mifumo rasmi ni ile ambayo inawekwa kwa mujibu utaratibu, kanuni na Sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mifumo isiyo rasmi ni ile ambayo jamii inajiwekea kupitia mila na desturi zake. 

Katika Mfumo rasmi wa Hifadhi ya Jamii umegawanyika katika makundi makubwa mawili ambayo ni Hifadhi ya Jamii kwa utaratibu misaada kwa jamii “Social Assistance Schemes” ambapo misaada na ruzuku hutolewa kwa jamii kuwapatia wananchi huduma za misingi za Hifadhi ya Jamii. Huduma hizo hutolewa kwa malengo mbalimbali kama vile; kugharamia elimu ya msingi, afya, maji, ruzuku, uzee, ulemavu na kukabiliana na majanga yanayotokea kwenye jamii. 

Pili ni Hifadhi ya Jamii katika utaratibu wa bima kwa jamii “social insurance”.  Aina hii ya hifadhi ya jamii ipo katika sehemu mbili ambazo ni sehemu ya kwanza ni Fao la jamii kwa mujibu wa Sheria; Wafanyakazi hupaswa kuchanga na kupata mafao kwa mujibu wa Sheria kama vile Mifuko ya pensheni na Fao la Afya. Sehemu ya pili ni Mfuko wa hiari “Supplementary Schemes”, ambapo Wanachama huchangia kwa hiari.

Hapa nchini Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kutekeleza dhana ya hifadhi ya jamii. Hatua hizo ni pamoja na kutoa huduma za msingi kama elimu, afya, maji, pembejeo za kilimo na ruzuku kwa wananchi;  kwa lengo la kutoa kinga kwa wananchi  ili  kuwawezesha kuishi maisha yenye staha.

Kwa upande wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini ilianza kama Mifuko ya akiba “Provident Fund” na baadaye Serikali iliibadilisha kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii “social security” ili kukidhi matakwa ya dhana ya Hifadhi ya Jamii.  Kabla ya kuunganishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii tulikuwa na mifuko saba ambayo ni PSPF, NSSF, PPF, LAPF, GEPF, NHIF na WCF. Mifuko hii inaendeshwa kwa utaratibu wa Bima ya Jamii “Social Insurance”. 

Aidha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha Huduma zinazotolewa na Mifuko hiyo, shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA) kwa nyakati tofauti imewasilisha kilio cha kuunganisha mifuko. Kufuatia maombi hayo, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii –SSRA ilifanya tathimini ya kitaalamu ili kupata namna bora ya kuunganisha mifuko hiyo. 

Matokeo ya tathimini hiyo iliunga mkono hoja ya kuwa na mifuko miwili yaani Mfuko utakaohudumia sekta ya umma na mwingine kwa ajili ya sekta binafsi, suala lililopelekea kutungwa kwa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (The Public Service Social Security Fund Act No. 2 of 2018). Sheria hiyo, pamoja na mambo mengine, inaunganisha Mifuko ya Pensheni minne (4) ambayo ni Mifuko ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda Mfuko mmoja kwa ajili ya Watumishi wa Umma yaani PSSSF. 

Sambamba na kuanzishwa kwa Mfuko wa PSSSF, Sheria hii imefanya marekebisho kwenye Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, (The National Social Security Fund) Sura ya 50 ili kuufanya Mfuko wa NSSF kuwa Mfuko utakaohudumia wafanyakazi wa Sekta Binafsi na Sekta isiyo rasmi. 

Kukosekana kwa utaratibu wa kinga ya kipato kwa wafanyakazi wanaopoteza ajira kumesababisha wafanyakazi hawa kujitoa uanachama kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuchukua michango yao ili kujikimu baada ya kupoteza ajira. Utaratibu huo wa kujitoa uanachama na kuchukua mafao yao umezoeleka miongoni mwa wanachama wa Mifuko ya Pensheni na hata kuoonekana kama ni mojawapo ya mafao ya Hifadhi ya Jamii maarufu kama “Fao la Kujitoa”. Hivyo, kutokuwepo kwa utaratibu mbadala wa kujipatia kipato mara baada ya kupoteza ajira kumesababisha baadhi ya wafanyakazi kudai kulipwa michango yao ya pensheni.

Aidha, kutokana na ukuwaji wa sekta binafsi kumekuwepo na mabadiliko katika soko la ajira ambapo yamechangia ongezeko la fursa za ajira zenye masharti ya muda mfupi ya ajira hivyo kusababisha wafanyakazi hao kuomba kujitoa uanachama mara mikataba yao ya ajira inapokwisha. 

Takwimu zinaonyesha kwamba wafanyakazi walio kwenye kundi la masharti ya ajira za kudumu ndio lina matukio mengi ya wanachama kujitoa. Kwa mfano katika kipindi cha Julai 2016 hadi Disemba 2017, kati ya wanachama 23,000 waliojitoa kwenye Mfuko wa PPF asilimia 78.3 sawa na wanachama 18,000 walikuwa wafanyakazi walio kwenye masharti ya kudumu. 

Wafanyakazi 5,000 sawa na asilimia 21.7 walitokana na kundi la Wafanyakazi walioajiriwa kwa Mikataba ya muda mfupi na ambao hawana ujuzi mkubwa walioajiriwa kwenye mashamba, migodi na miradi mbalimbali ya muda mfupi. Kuwepo kwa idadi kubwa ya wafanyakazi wanaojitoa kutoka kwenye kundi la wafanyakazi wenye mikataba ya ajira ya muda mrefu kunaashiria kwamba baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakijitoa bila sababu za msingi. 

Utaratibu wa wanachama kujitoa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii una athari nyingi, miongoni mwa athari hizo ni pamoja na Wanachama kupoteza sifa za kupata mafao mbalimbali ambayo wangepata hata kabla ya kustaafu kama mafao ya matibabu, elimu, nyumba, kuumia kazini, uzazi, ulemavu na mikopo mbali mbali. 

Aidha, Mwanachama anaejitoa hupoteza sifa ya kulipwa mafao ya pensheni mara atakapotimiza umri wa kustaafu na hivyo hatakuwa na kipato chochote cha uhakika kuweza kujikimu. Hali hii itamfanya kuwa tegemezi kwa familia, jamii au serikali. 

Ili kukabiliana na tatizo hili la wanachama kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na kukidhi mahitaji ya mfumo wa hifadhi ya jamii wa kuwa na utaratibu wa kinga ya kipato kutokana na upotevu wa ajira, Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii ilikuja na mapendekezo ya kuanzishwa kwa Fao la Upotevu wa Ajira. Mapendekezo ambayo tayari yamekwisha kuingizwa kwenye sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ya mwaka 2018.

 Fao hili la upotevu wa ajira itakalotolewa kwa wafanyakazi ambao ni wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pale wanapopoteza ajira zao.  Fao hili litatokana na mchango wa Pensheni wa Mwanachama kumuwezesha kujikimu katka kipindi anachotafuta ajira nyingine.

Uanzishwaji wa fao hili litawezesha kutekelezwa na kuimarishwa kwa dhana ya hifadhi ya jamii kwa kuwajali wafanyakazi watakaopoteza ajira kwa kuwawekea kinga ya kipato itakayo wawezesha kupata fedha za kujikimu katika kipindi wanachotafuta kazi.

Lakini pia uwepo wa fao la upotevu wa ajira kutaondoa migogoro ya kikazi na malalamiko ya wafanyakazi yaliyopo kutokana na kuwepo utaratibu unaokubalika na hivyo kuongeza ari na tija sehemu za kazi.
Fao la upotevu wa ajira kutaimarisha mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kupunguza matumizi ya fedha ya kuwalipa wanachama wanaoamua kujitoa kwenye mifuko bila sababu za msingi na kisha kuwa mzigo kwa jamii na serikali hapo baadaye. Wakati huo huo utaratibu huu hautakuwa na gharama kwa serikali kwa sababu fedha za malipo ya Fao la Upotevu wa ajira zitatokana na michango ya pensheni ya mwanachama mwenyewe.

Utaratibu wa utoaji wa hili fao la upotevu wa ajira
1. Kanuni ya mpya Mafao ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018, Kanuni ya 20 imebainisha kuwa mafao ya upotevu wa ajira yatakuwa sawa na asilimia 33.3 ya mshahara wa mwezi wa mwanachama aliyepoteza ajira.

2. Kanuni 21; Muda wa ulipaji wa mafao ya upotevu wa ajira; 
Mafao haya yatalipwa kwa kipindi kisichozidi miezi 6 kwa mwaka na mwanachama atalipwa kwa kipindi kisichozidi miezi 18 katika kipindi chote cha ajira;

3. Kama mwanachama atakua hajapata ajira baada ya miezi 18 anaweza kumuandikia Mkurungenzi Mkuu kuomba kuhamisha michango yake kwenda kwenye Mfuko wa hiara wa chaguo lake na anaweza kuendelea kuchangia katika mfuko huo

4. Michango hiyo ya mwanachama itakua ni sawa na malipo ya mkupuo maalum ukitoa mafao ya upotevu wa ajira aliyokwisha kulipwa

5. Kwa mwanachama aliyechangia chini ya miezi 18 atalipwa asilimia 50 ya michango yake 

6. Kama mwanachama atakosa ajira baada ya miezi 18 baada ya malipo haya kukoma, ataweza kubadilisha michango yake kwenda kwenye Mfuko wa hiari wa chaguo lake kwa kumuandikia Mkurungenzi Mkuu kuomba kuhamisha michango hiyo na anaweza kuendelea kuchangia katika mfuko  huo.

7. Michango hiyo ya mwanachama itakua ni sawa na malipo ya mkupuo maalum ukitoa mafao ya upotevu wa ajira aliyokwisha kulipwa

Ni wito kwa kila Mtanzania ambaye bado hajajiunga na mfuko wowote wa hifadhi ya jamii anaweza kuamua kujiunga na kuchangia mfuko wa Hifadhi ya Jamii huku Mamlaka ikiwahakikishia kuendelea kulinda na kutetea maslahi ya wanachama. Ni juhudi za SSRA kuhakikisha Mifuko inaendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kujenga sekta imara na endelevu yenye Mafao bora kwa wanachama wake.

Uwekezaji wenye tija na manufaa kwa wanachama hata kabla ya kustaafu ukiwa ndio matamanio.

No comments:

Post a Comment