Wednesday, October 24, 2018

RAIS WA ZANZIBAR AHAKIKISHIWAUSHIRIKIANO NA MTAWALA WA RAS AL KHAIMAN


MTAWALA wa Ras al Khaimah Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi amemuhakikishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kuwa serikali yake itatoa ushirikiano katika kufanikisha shughuli ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kupitia Mkataba uliosainiwa hapo jana.

Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na mwenyeji wake Rais Dk. Shein katika ukumbi wa Ikulu mjini Zanzibar, ambapo katika mazungumzo hayo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alihudhuria pamoja na viongozi wa Ras al Khaimah na wa Zanzibar.

Katika maelezo yake, Shaikh Al Qasimi alisifu juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Kampuni ya RAK GAS ya Ras al Khaimah katika kutekeleza mipango iliyopo ya utafutaji wa nishati hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Mtawala huyo alieleza kuvutiwa kwake na mipango inayoendelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya mafuta na gesi hasa kwa maamuzi yaliyofikiwa ya kutaka kujenga bandari maalum ya mafuta na gesi katika eneo la Mangapwani.

Aidha, Mtawala huyo alisema kwamba Serikali ya Ras al Khaimah itatekeleza ahadi iliyoitoa mwezi Januari mwaka huu wakati Rais Dk. Shein alipotembelea nchi hiyo ya kushirikiana na Zanzibar kinyenzo na kitaalamu katika kujitayarisha kuingia katika uchumi wa mafuta na gesi asilia.

Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi ambaye hapo jana aliungana na Rais Dk. Shein katika viwanja vya Ikulu mjni Zanzibar kushuhudia utiaji saini Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia, alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kwamba nchi kadhaa duniani zinapata changamoto kwa kushindwa kujitayarisha vizuri katika kuipokea sekta hiyo.

Kadhalika kiongozi huyo alisifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza sekta ya utalii na kuahidi kwamba Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili Zanzibar iweze kufikia malengo yake iliyojiwekea katika kuendeleza sekta hiyo.

Kiongozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kwamba Ras al Khaimah inatumia uzoefu wake ulionao kwa kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Kuhusu sekta ya elimu, Kiongozi huyo aliipongeza Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar chini yauongozi wa Rais Dk. Shein kwa juhudi inazoendelea kuzichukua katika kuendeleza sekta ya elimu ili kuweza kukidhi mahitaji ya wataalamu wanaohitajika nchini katika sekta mbali mbali pamoja na kuweza kwenda sambamba na mahitaji ya karne ya 21.

Kiongozi huyo alieleza kuwa ili kuhakikisha Zanzibar inafikia azma ya kuwa na wataalamu wa kutosha aliahidi kwamba pande zote mbili zitashirikiana kuimarisha sekta ya elimu kwa nchi hiyo kutoa nafasi za masomo kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na kubadilishana wanafunzi baina ya pande mbili hizo.  
Alieleza kwamba wananachi wan chi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wanahistoria kubwa inayoonesha kuwa wamekuwa na ushirikiano wa kidugu na ndugu zao wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba ziara hiyo itazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo.

Alisema kwamba ziara yake hiyo inatoa fursa nzuri ya kuharakisha utekelezaji wa mambo mbali mbali yaliyokubaliwa katika ziara aliyoifanya Rais Dk. Shein mwezi Januari mwaka huu katika nchi za Falme za Kiarabu.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alitumia fursa hiyo kwa kueleza juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ili kuimarisha ustawi wa wananchi.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya utalii ambayo ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar hivi sasa na kueleza azma na mikakati iliyowekwa ili kuongeza idadi ya watalii ifikapo mwaka 2020.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza mipango ya Zanzibar ya kujenga bandari maalum ya kusafirisha mafuta na gesi asilia kwa azma ya kurahisisha usafiri wa nishati hiyo ili kuondoa changamoto zilizopo hivi sasa za usafirishaji wa bidhaa pamoja na kujitayarisha na mipango ya hapo baadae.

Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa Mtawala huyo kwa kukubali kushirikiana na Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha sekta ya elimu, kwa kukubali kutoa nafasi maalum za masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar katika nyanja mbali mbali zinazofundishwa katika vyuo vya Ras al Khaimah.

Alitoa shukurani maalum kwa Serikali ya nchi hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kukuza uchumi na kuimarisha utoaji huduma mbali mbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kusaidia kuimarisha sekta ya maji safi na salama hapa Zanzibar.

Alieleza haja kwa Ras al Khaimah kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo tayari imeshapata mafanikio makubwa katika sekta hiyo huku akieleza umhimu wa pande mbili hizo kushirikiana katika sekta ya usafri wa anga hatua ambayo itasaidia shughuli za utalii, biashara na shughuli nyenginezo za kijamii.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein amemueleza kiongozi huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kuyatekeleza makubaliano yote yaliyokubaliwa katika ziara zote zilizofanyika nchini humo pamoja na yale yote yaliyokuwemo katika Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia.

Shaikh Saud Bin Saqr Al Qasimi ameondoka nchini leo kurejea Ras al Khaimah ambapo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume aliagwa kwa heshima zote za Kitaifa pamoja na kuagwa na viongozi mbali mbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa  Haji Ussi Gavu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822  



E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment