Wednesday, October 10, 2018

Raia wa Syria, Sudan Kusini wakamatwa JNIA wakisafirisha mamilioni

 Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi  Barnabas Mwakalukwa akimuonesha mtuhumiwa raia wa Sudan Kusini Bi. Nada Zaelnoon Ahamed
  Fedha taslim dola 70,000 za Kimarekani sawa na shilingi milioni 156 za Kitanzania na paundi 3410 za Sudan zilizotaka kusafirishwa bila kufuata taratibu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi  Barnabas Mwakalukwa akimuonesha mtuhumiwa rais wa Syria Bw. Mohamed Belal 

ABIRIA wawili Raia wa Sudan Kusini na Syria leo wamekamatwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wakisafirisha fedha taslim dola 70,000 za Kimarekani sawa na shilingi milioni 156 za Kitanzania na paundi 3410 za Sudan bila kufuata taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la JNIA, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi, Barnabas Mwakalukwa alimtaja Raia wa Sudan Kusini Bi. Nada Zaelnoon Ahamed (38) mwenye hati ya kusafiria namba P01563534 amekamatwa saa 10:00 jioni akiwa eneo la ukaguzi wakati akiingia ndani tayari kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ 485) akielekea Nairobi.

Hatahivyo, Afande Mwakalukwa amesema abiria huyo am3kamatwa na dola 60,000 za Kimarekani na paundi za Sudan 3410, ambazo zote kwa pamoja alishindwa kutoa taarifa ya fedha alizokutwa nazo kwa mujibu wa sheria ya utakatishaji fedha ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Pia alimtaja Bw. Mohamed Belal (31), Raia wa Syria mwenye hati ya kusafiria namba 003-16L096876 aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia (ET 864) kuelekea Syria kupitia Addis Ababa amekamatwa na dola za kimarekani 10,000 sawa na Tsh. milioni 20 za Kitanzania, ambazo naye alishindwa kuzitolea taarifa.

“Watuhumiwa wote wawili wamezuiwa na hawawezi kuendelea na safari zao kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria zilizopo,” amesema Afande Mwakalukwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewapongeza maafisa usalama wa JNIA kwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha wasafiri, wadau na maeneo yote ya viwanja vya ndege yanabaki salama na vitendo vya kiuhalifu havina nafasi katika viwanja hivyo.

Bw. Mayongela amesema pamoja na watumishi hao kufanya kazi katika wakati mgumu kutokana na baadhi ya abiria kuwa watata kila wanapotaka kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Ametoa wito kwa wadau, wasafiri na wafanyakazi wote kushirikiana na maafisa usalama, vyombo vya ulinzi na usalama katika kutoa taarifa stahiki ili vitendo vya kiuhalifu kama hivi visipate nafasi kwenye viwanja vya ndege kwani ndio vinatoa taswira ya nchi.

“Viwanja vya ndege visitumike kama uchochoro wa kupitisha nyara za serikali, dawa za kulevyia, fedha haramu au matukio yeyote yanayoashiria uvunjifu wa Amani au uvunjaji wa sheria za nchi,”

Pia aliongeza “Niombe wananchi na vyombo vya usalama kufanya kazi kwa weledi kwa sababu wasipofanyakazi kwa weledi matukio kama haya yangeweza kupata nafasi na kuharibu taswira ya nchi, kwa ujumla mwisho wa siku inaharibika, kwani nia yetu na lengo letu ni zuri ni kuhakikisha hatutumiki kwa namna moja au nyingine kufadhili au kuwezesha shughuli za kiuhalifu zifanyike katika maeneo yetu”.

Amesema na hii ni moja ya ushahidi maafisa usalama wanapata mafunzo na kujengewa uwezo wa kuwa na vifaa vya kisasa kwani vitu mbalimbali vimekuwa vikigundulika kupitia mashine za ukaguzi, na pia kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, hivyo ametoa wito watu wasidhubutu tena kujaribu kwa namna yeyote ile akidhani viwanja vya ndege wamelala, kwani ulinzi na usalama unaendelea kuimarika.

Kwa upande wake Meneja wa Forodha wa Kituo cha JNIA, Bw. Njaule Mdendu amesema abiria wote wanaosafiri au kuwasili endapo wanakiasi kikubwa cha fedha za kigeni kuanzia dola 10,000 za Kimarekani sawa na Milioni 10 za Kitanzania anapaswa kutoa taarifa Idara ya Forodha kwa kuwa ni matakwa ya sheria ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012 na kanuni za mwaka 2016, na asipofanya hivyo ni kosa la jinai.

Bw. Mdendu amesema abiria wanapaswa kuchukua fomu maalum akieleza utambulisho wake na kiasi cha fedha anachoingia nacho au kutoka nacho, na fomu atazipata kwenye ofisi zote za forodha za mipakani kwenye viwanja vya ndege, mipaka ya ardhi na majini endapo atakuwa akitumia usafiri wa barabara au majini.

“Hizi fomu pia zipo kwenye tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na akishajaza anawasilisha ofisi za Forodha na kiasi cha fedha anachosafiri au kuwasili nacho na afisa atazihakiki na akiridhika ataruhusu aendelee na safari yake, na napenda kuwatoa hofu watu kuwa fedha zao hawanyang’anyi baada ya kutoa taarifa na ataondoka nayo, lakini endapo usipotoa taarifa ni kosa na inaadhabu yake kulingana na kiasi cha fedha ulichokutwa nacho, hivyo tuwaombe abiria kutimiza matakwa ya kisheria, kwani watu wamekuwa wakifanya makosa bila kujua sheria,” amesema.

No comments:

Post a Comment