Monday, October 1, 2018

NCHI ZA SADC ZATAKIWA KUKUZA UELEWA WA SHUGHULI ZA JUMUIYA HIYO KWA WANANCHI WAKE

Zamaradi Kawawa, MAELEZO, Windhoek, Namibia 

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC zinatakiwa kukuza uelewa wa shughuli za SADC kwa wananchi wake kwa kufundisha mashuleni historia ya ukombozi wa nchi hizo pamoja na kutumia wimbo wa SADC na bendera yake kwenye shughuli za kitaifa na kimataifa.

Baraza la SADC la Mawaziri wa nchi wanachama wanaoshughulikia sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na Uchukuzi walikubaliana hayo katika kikao kilichofanyika Septemba 27,2018 Windhoek, Namibia baada ya kufunguliwa na Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia Mheshimiwa Tom Alweendo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo.

Kikao cha Baraza la Mawaziri wa SADC kilisema wananchi wa SADC wanatakiwa kuelimishwa kuhusu SADC kwa kufahamu historia yake na ukombozi wa nchi wanachama, alama za SADC zikiwemo bendera, nembo, wimbo na itifaki yake kwa kuhusisha elimu hiyo kwenye mtaala wa elimu kwa nchi wanachama.

Akifungua kikao hicho, Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia Mheshimiwa Alweendo alisema kuna taarifa nyingi nzuri za kuwaeleza wananchi wa nchi wanachama kuhusu SADC hivyo ni jukumu la Serikali za nchi za SADC kuelimisha na kuwaeleza wananchi wake wakati chombo hicho kkiendelea kujiimarisha.

Kikao hicho cha siku moja kilichokutana kwa lengo la kupitia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi wanachama kwenye maeneo ya sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na uchukuzi kilisimama kwa dakika moja kabla ya kuanza ili kuonyesha masikitiko yao kwa vifo vya watanzania zaidi ya 200 vilivyotokana na ajali ya MV Nyerere Ziwa Victoria, Mwanza.

Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo bi. Susan Mlawi kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ambaye kwa niaba ya Serikali alipokea salamu za pole kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo kufuatia vifo vya watanzania zaidi ya 200 vilivyotokana na ajali ya MV Nyerere kwenye Ziwa Victoria mkoani Mwanza hivi karibuni.

Aidha, Kikao hicho kiliipongeza Tanzania kwa kupata tuzo ya dunia ya usalama wa anga baada ya kufaulu kwa kukidhi vigezo vilivyowekwa na Baraza la usafiri wa anga duniani vinavyohusu uhakika wa usalama wa anga.Wakati wa kikao hicho cha baraza la SADC la Mawaziri wa sekta za Mawasiliano, Habari, Ujenzi na Uchukuzi, Bi Mlawi alieleza nia ya Tanzania ya kupeleka mgombea kwenye nafasi ya Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kuomba ushirikiano wa nchi wanachama wa SADC wakati wa uchaguzi ukifika.

Alimtaja mgombea huyo kuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dr Agnes Kijazi, mwanamke msomi wa ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD) mwenye uzoefu wa miaka 30 kwenye masuala ya hali ya hewa kutoka nchi za SADC.Mheshimiwa Alweendo kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho alisema nchi wanachama wa SADC zimepiga hatua kubwa kwenye masuala ya hali ya hewa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya satellite iliyoimarisha kwa kiasi kikubwa matokeo ya utabiri wa hali ya hewa hivyo kuwezesha nchi kukabiliana na majanga ya ukame, mafuriko na moto yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dr. Agnes Kijazi ambaye pia alitambulishwa katika kiako hicho aliiambia Idara ya Habari-MAELEZO kuwa Tanzania inajipanga kutekeleza miradi miwili mikubwa ya SADC ikiwemo uboreshaji wa chuo cha yaifa cha hali ya hewa kilichopo Kigoma pamoja na uwekaji wa miundo mbinu ya kisasa ya utabiri wa hali ya hewa itakayoimarisha huduma za utabiri wa hali ya hewa kwa nchi ili kupunguza umaskini. 

Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC ina nchi wanachama 16 zikiwemo Namibia ambaye ni mwenyekiti na Tanzania ni Makamu mwenyekiti wa Jumuiya hiyo. Nchi nyingine ni Zimbabwe, Zambia, Malawi, Afrika Kusini, Botswana, Angola, Msumbiji, Eswati, Lesotho, DRC, Mauritius, Comoro, Seychelles na Moroco. 

No comments:

Post a Comment