Mawaziri
wa Mambo ya Nje wa Italia na Afrika wameazimia kukuza na kuimarisha
Ushirikiano katika nyanja mbalimbali, hususan biashara na uwekezaji kwa
ajili ya maendeleo ya kweli barani Afrika.
Mawaziri
hao walifikia azimio hilo wakati wa mkutano wa pili wa Mawaziri wa
Mambo ya Nje wa Italia na Afrika uliofanyika Farnesina, Italia tarehe 25
Oktoba 2018 na kuhudhuriwa na Mawaziri wa zaidi ya nchi 40 akiwemo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb).
Mawaziri
hao walikutana kwa madhumuni ya kujadili kwa pamoja changamoto
zinazohusu usalama, uhuru, amani, demokrasia na namna wadau wa Italia
(wenye viwanda, Wafanyabiashara, wanazuoni na taasisi zisizo za
kiserikali) watakavyoweza kushiriki katika kukuza uchumi barani Afrika
hasa katika sekta ya uwekezaji na biashara.
Katika
hotuba yake kwenye mkutano huo ambao ulifunguliwa na Rais wa Italia,
Mhe. Sergio Mattarella, Mhe Waziri Mahiga alisisitiza suala la amani
kuwa ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi barani Afrika. Aidha,
alieleza umuhimu wa Jumuiya za Kikanda katika kusuluhisha migogoro
mbalimbali inayotokea kwenye Bara la Afrika. Katika hilo, alijulisha
jitihada zinazofanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kusuluhisha mgogoro nchini
Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Sanjari
na mkutano huo, Waziri Mahiga alipata fursa ya kufanya mazungumzo kwa
nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe Enzo Moavero na
Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD),
Bw. Gilbert F. Houngbo.
Kwenye
mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Viongozi hao
walikubaliana kuwa, kuandaliwe Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya
Tanzania na Italia ya kufanya majadiliano ya mara kwa mara yenye lengo
ya kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara,
uwekezaji, utalii, elimu na utamaduni.
Kuhusu
mazungumzo na Rais wa IFAD, wawili hao walikubaliana kuimarisha
ushirikiano wa Tanzania na Mfuko huo kwenye maeneo makuu mannne ambayo
ni Huduma za kifedha kwa wakulima wadogo, kuwajengea uwezeo vijana ili
waweze kufanya kilimo kama sehemu ya ajira, kuboresha sekta ya mifugo
pamoja na masuala ya lishe bora.
Aidha,
Rais wa IFAD alimuahidi Mhe Waziri kuwa mfuko huo utaendelea
kushirikiana vizuri na serikali ya Tanzania hata kwenye miradi
inayoendelea ikiwemo Programu ya Miundombinu ya masoko, uongezaji wa
thamani na kuwawezesha wakulima wadogo wa vijijini kifedha (Marketing
Infrastructure, Value Addition and Rural Finance-MIVRAF). Madhumuni ya
programu hiyo ni kupunguza umasikini na kuharakisha ukuaji wa uchumi
vijijini ili kuboresha kipato na usalama wa chakula kwa jamii ya watu wa
vijijini.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, Tanzania
29 Oktoba 2018
No comments:
Post a Comment