Thursday, October 4, 2018

DK.MWAKYEMBE AWATEMBELEA NAFASI ART SPACE,AWAPONGEZA KWA KUTIMIZA MIAKA 10

 Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

WAZIRI wa Habari,Sanaa,Utamaduni na Michezo Dk.Harrson Mwakyembe amewapongeza Nafasi Art Space kwa kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake huku akielezea namna ambavyo wamekuwa wadau muhimu katika kukuza na kuendeleza sanaa za aina mbalimbali nchini.

Dk.Mwakyembe amewatembelea Nafasi Art Space katika ofisi zao zilizopo Mikochen B jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na Katibu Mtendaji ww Baraza la Sanaa Tanzania(BASATA) Godfrey Mngereza pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali wakiwamo pia wa TAFCA.

Akiwa hapo Dk.Mwakyembe alipata nafasi ya kuelezwa historia ya Nafasi Art Space, mipango na mikakati ndani miaka 10 ya mwanzo.Mchoraji mahiri ambaye pia ni Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mmoja ya wajumbe wa bodi na mwalinzi wa Nafasi Art Space Profesa Elias Jengo, alitumia nafasi hiyo kueleza mafanikio ya uwepo wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nafasi, Rebecca amemueleza Waziri Mwakyembe kuwa Nafasi Art Space imefanikiwa kuipeleka mbele sanaa ya Tanzania na mkakati wao ni kuendelea zaidi ya hapo."Mkakati na malengo yetu ni kuipeleka sanaa mbele zaidi na kuongeza fursa na vipato vya wasanii kupitia sanaa," amesema.

Pia amezungumzia namna ambavyo wasanii wananufaika kwa studio za kufanyia kazi, mafunzo mbalimbali, nafasi ya kukutana na wasanii wenzao kupitia Nafasi Art Space.Pia fursa ya kukutana na wapenzi wa sanaa wanaoweza kuthamini kazi zao.Kuhusu mambo ambayo yamefanyika katika kuadhimisha miaka 10 ,Rebecca amesema Septemba mwaka huu wameshiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

"Nafasi kwa mwezi wote wa Septemba tumeshiriki mambo mbalimbali ikiwemo kwenda mashuleni,hospitalini na maeneo ya soko." Tumeshiriki shughuli za kufanya usafi na mwisho kabisa tukawa na tamashaa kubwa na la aina yake ambalo lilifanyika hapa kwetu ambapo hakukuwa na kiingilio,"amesema.

Hata hivyo baada ya kupata maelezo mbalimbali Dk.Mwakyembe ameshuhudia maonesho ya kazi za wasanii.Ameshuhudia michoro mbalimbali ya wasanii mahiri ambao wamebobea katika sanaa ya uchoraji wakiwamo Paul Ndunguru, Masoud Kibwana, Mwandale “Big Mama” Mwanyekwa, Cloud Chatanda, Amani Abeid, Safina Kimbokota, Fred Halla, Nathan Mpangala, and others.

Pamoja na yote hayo Dk.Mwakyembe amefanya mazungumzo na Ofisa wa Sanaa ya michezo wa Nafasi Kwame Mchauru.Akizungumza na wajumbe wa bodi, wasimamizi, wafanyakazi na Nafasi Art Space Dk.Mwakyembe amewahakikishia kuwasaidia katika kuendeleza sanaa nchini.Pia amewapongeza Nafasi kwa mchango ambao wanautoa katika kuendeleza sanaa na kwamba ushirikiano na uhusiano kati ya Wizara na Nafasi utaendelea kukua na kuimarika siku hadi siku.

Pia Dk.Mwakyembe amesema amefurahishwa na Nafasi katika kukuza utamaduni na utambulisho wa taifa wa Tanzania, kusaidia wasanii vijana katika elimu zao na maendeleo, na kufanya kazi pamoja kutumia sanaa kama chombo cha kuboresha jamii.




Waziri wa Habari,Sanaa,Utamaduni na Michezo Dk.Harson Mwakyembe akiangalia moja ya kazi ya uchongaji vinyago iliyofanywa na wasanii waliopo Nafaso Art Space baada ya kuwatembelea kwa lengo la kuwapongeza kwa kutimiza miaka 10

No comments:

Post a Comment