Sunday, September 30, 2018

SIKU YA MOYO DUNIANI YAADHIMISHWA KWA KUTOA ELIMU NA UPIMAJI WA AFYA

SIKU ya moyo duniani imeadhimishwa leo Septemba 29 ikiwa lengo mahususi kwa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujua na kupima magonjwa mbalimbali ya moyo, pamoja na kuelimisha jamii juu ya athari mbalimbali zinazotokana na magonjwa ya moyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa afya, wazee, jinsia na watoto Faustine Ndugulile amesema kuwa  maadhimisho ya Siku ya Magonjwa ya Moyo Duniani mwaka yamekuja na kauli mbiu ya ‘MOYO WANGU, MOYO WAKO’ kwa lugha ya kiingereza  My heart, Your heart, ikiwa na lengo la kusisitiza juu ya kila mmoja wetu kufanya uchunguzi wa moyo ili kujua hali yake.

Aidha amesema; "Magonjwa ya moyo yanaongoza kwa kusababisha vifo duniani. Inakadiriwa kuwa watu 17,500,000 hufa kila mwaka duniani kote kutokana na magonjwa ya moyo na kiharusi. Ugonjwa wa moyo ni ugonjwa ambao unaathiri watu wa rika na jinsia zote; watoto, watu wazima, wake kwa waume. Aidha, Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kwamba asilimia 40% ya vifo vyote vinavyotokea duniani vinasababishwa na magonjwa ya moyo. Pia nusu ya vifo ambavyo vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza vinatokana na magonjwa ya moyo na vilevile asilimia 80% ya vifo hivi hutokea kwenye nchi zenye uchumi wa kati na wa kiwango cha chini" amesema Ndugulile.

Aidha imeelezwa kuwa matumizi ya tumbaku na bidhaa zake yanakadiriwa kusababisha vifo vya watu 6,000,000 duniani kila mwaka na pia huchangia kusababisha asilimia 10% ya wagonjwa wenye magonjwa ya moyo. Vilevile moshi wa sigara kwa watu wasiovuta sigara (second hand smoking) husababisha vifo vya watu laki sita (600,000) na kati ya hao 28% ni watoto. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani (WHO).

Pia amesema kuwa kama hatua madhubuti za kinga, uchunguzi wa mapema na tiba stahiki hazitachukuliwa haraka, tatizo la Moyo ifikapo mwaka 2035 litaongezeka na kufikia makadirio ya wagonjwa wapya milioni 131,978,870 (sawa na ongezeko la 45% kutoka hali ilivyo kwa sasa), huku ongezeko kubwa likiwa katika ukanda wa nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa moja wapo.

Pia ameeleza kuhusu tafiti wa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza uliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) mwaka 2012, ulionyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la viashiria vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 15.9% ya wananchi wanavuta sigara, asilimia 29.3% wanakunywa pombe, asilimia 97.2% wanakula mboga mboga na matunda chini ya mara tano kwa wiki.

 Aidha utafiti ulionyesha asilimia 26% ya wananchi ni wanene kupita kiasi, asilimia 26% wana lehemu nyingi mwilini, asilimia 33.8% wana mafuta mengi mwilini, asilimia 9.1% wana kisukari na asilimia 25.9% wana shinikizo kubwa la damu. Utafiti pia ulionyesha 25% ya wananchi waliohojiwa hawajishughulishi na kazi zinazotumia nguvu na hawafanyi mazoezi yeyote. Viashiria hivi ndivyo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Moja wapo ya sababu kubwa za magonjwa ya shinikizo la damu ni kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye misuli ya moyo. Kuziba kunaweza kusababishwa na mafuta yaliyomo kwenye chakula ambayo huenda huganda katika kuta za mishipa hiyo, hali ambayo hutokea pole pole na huchukua muda mrefu hadi mishipa kuziba kabisa. Matumizi ya tumbaku, uzito uliozidi na kutofanya mazoezi huchangia sana uwezekano wa kupata ugonjwa wa shinikizo la damu na  hii hupelekea mtu kupata matatizo hayo. 

Imeelezwa kuwa ugonjwa wa Moyo umekuwa na vyanzo mbalimbali vinavyosababisha tatizo hili kukua kwa kasi hapa nchini na Duniani kote. vyanzo hivyo vikubwa ni pamoja na: Mtindo wa kimaisha (Life Style), Ulaji usiofaa, Kutofanya Mazoezi, Matumizi ya pombe, Uvutaji wa Sigara na matumizi ya bidhaa zitokanazo na Tumbaku  

Ili kuzuia ugonjwa wa Moyo na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata maradhi ya Moyo . 

Na ametoa rai kwa wananchi wote nchini watoe ahadi kwa ajili ya moyo wangu, moyo wako na mioyo ya watu wengine, na tuchukue hatua madhubuti za kujikinga dhidi ya magonjwa ya moyo na kuweka ahadi ya mtu binafsi ya kupika na kula chakula kinachokidhi viwango vya afya,

Ahadi ya kujitahidi kufanya mazoezi na kuwafundisha na kuwahimiza watoto wetu kufanya mazoezi,ahadi ya kutovuta sigara na kutumia bidhaa za tumbaku, na kuwahimiza wapendwa wetu ambao wanavuta sigara na kutumia bidhaa za tumbaku kuacha kabisa, ahadi kwa watoa huduma za afya, kujitahidi kutoa huduma bora ya kuelimisha, kukinga na kuokoa maisha, 

ahadi ya viongozi wa kitaifa kufanikisha mpango mkakati wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na amewakaribisha wananchi wote kwenye zoezi la uchunguzi linaloendelea katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.Kwa upande wake Rais wa Chama cha madaktari wa moyo nchini Dkt. Robert Mvungi amesema kuwa tatizo la moyo ni kubwa na gharama ni kubwa na kinga ni sisi wenyewe kubadili mifumo ya maisha. 

Na amesema kuwa kuna tishio kwa ugonjwa wa moyo kwani watu wenye umri mdogo hupata ugonjwa wa moyo na amesema baadhi ya visababishi ni pamoja na presha ambapo zaidi ya asilimia 20 ya watu wa chini ya miaka 25 wana presha.Sigara, mfumo wa maisha na matumizi ya pombe.

Amewaasa wananchi kubadili mifumo ya maisha,kufanya mazoezi  na kuepuka matumizi ya sigara na pombe.
 Matembezi ya Siku ya Moyo Duniani yakiendelea, ambayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya 'Moyo wangu, Moyo wako"
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile  akiongoza mazowezi siku ya Moyo Duniani yaliyoanzia viwanja vya Leaders Club na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es sala, matembezi hayo yamebeba kauli mbiu ya "Moyo wangu Moyo Wako". Wakwanza Julia ni Mkurugenzi wa kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akikagua moja kati ya mabanda yaliyokuwepo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani. Kushoto kwake ni Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Robert Mvungi, kulia kwake ni Mkurugenzi wa kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma Wizara ya Afya Dkt. Amalberga Kasangala



Madakitari wakitoa elimu na kipima afaya za wananchi walijitokeza katika maadhimisho ya siku ya Moyo Duniani.(picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii)

No comments:

Post a Comment