Thursday, September 27, 2018

RAIS MAGUFULI AZINDUA FLYOVER YA MFUGALE ENEO LA TAZARA JIJINI DAR ES SALAAM LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Septemba, 2018 amefungua barabara za juu katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara Jijini Dar es Salaam (Mfugale Flyover) ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa magari katika barabara hizo, ikiwemo kwenda na kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Mfugale Flyover imejengwa na kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui Construction Co. Ltd ya Japan kwa gharama ya shilingi Bilioni 106.7.

Ujenzi wa Mfugale Flyover umehusisha njia 4 za barabara zenye urefu wa kilometa 1, ina uwezo wa kubeba uzito wa tani 180 kwa wakati mmoja, imesanifiwa kuishi kwa miaka 100, ina barabara za pembeni (access roads), njia za waenda kwa miguu, mfumo wa mifereji ya maji ya mvua, taa za kuongozea magari na umezingatia mradi wa mabasi yaendayo haraka kwa kuacha eneo la meta 12 katikati ya barabara hizo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa Mfugale Flyover ulioanza tarehe 01 Desemba, 2015 umekamilika mapema kabla ya tarehe iliyopangwa ambayo ni 31 Oktoba, 2018 na kwamba katika juhudi za kukabiliana na msongamano wa magari Serikali itajenga Flyover nyingine eneo la Chang’ombe katika makutano ya barabara ya Nyerere na Kawawa.

Kufuatia uamuzi wa Mhe. Rais Magufuli kuwa Flyover ya makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela iitwe Mfugale Flyover, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Prof. Ninatubu Lema amesoma wasifu wa Mhandisi Patrick Aron Lipilima Mfugale na kueleza kuwa ameitumikia nchi akiwa Mhandisi kwa miaka 41 ambapo katika kipindi hicho ameongoza katika kubuni na kusimamia ujenzi wa barabara kilometa 36,258 zikiwemo kilometa 9,951 za lami na amebuni na kusimamia ujenzi wa madaraja makubwa na madogo 1,400 yakiwemo madaraja makubwa ya Mkapa (Rufiji), Umoja (Ruvuma), Rusumo (Mara), Kikwete (Malagarasi), Nyerere (Kigamboni, Dar es Salaam), Magufuli (Kilombero) na Sibiti (Simiyu/Singida).

Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Japan kwa kutoa mkopo nafuu wa ujenzi wa Mfugale Flyover, amewapongeza wakandarasi kwa kumaliza kazi mapema, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa usimamizi wake wa karibu na kwa namna ya kipekee amempongeza Mhandisi Patrick Mfugale kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Flyover hiyo, madaraja na barabara mbalimbali hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Wahandisi wengine na wataalamu mbalimbali hapa nchini kuiga mfano wa Mhandisi Mfugale wa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa, badala ya kuwa kikwazo kwa kukosa uaminifu na uadilifu ama kutoa ushauri usio na manufaa kwa Taifa.

Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kuboresha miundombinu ya Dar es Salaam kama ilivyoahidi, na kubainisha kuwa pamoja na kujenga Flyover nyingine katika eneo la Chang’ombe pia inajenga barabara za juu katika eneo la Ubungo (Ubungo Interchange), inajenga barabara ya njia 8 ya Kimara – Kibaha (Kilometa 19.2) na ameagiza mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara uitwao DMDP na ambao umetengewa Shilingi Bilioni 660 uhamishiwe Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA).

Ametoa wito kwa watumiaji wa Mfugale Flyover kuwa makini ili kuepuka ajali zisizo za lazima na ameagiza zifungwe kamera za kurekodi magari katika Flyover hiyo na nyingine zitakazojengwa Jijini Dar es Salaam.

Sherehe ya Ufunguzi wa Mfugale Flyover imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wizara, Balozi wa Japan hapa nchini anayemaliza muda wake Mhe. Masaharu Yoshida, Wabunge wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Seleman Kakoso, viongozi wa dini, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Bw. Paul Makonda.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameagana na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Masaharu Yoshida ambaye amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mzuri alioupata kwa kipindi cha miaka 3 na nusu aliyokuwepo hapa nchini.

Mhe. Masaharu Yoshida amepongeza uongozi mzuri wa Mhe. Rais Magufuli na juhudi kubwa anazozifanya katika kujenga uchumi wa Tanzania na ameahidi kuwa balozi mzuri wa Tanzania.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
27 Septemba, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia  wakati akizindua rasmi wa Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida akipena mikono na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa  baada ya kuzindua rasmi  Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa akimpongeza   Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale  baada ya kuzindua rasmi  Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018. 
Mke wa Rais Dkt. Magufuli, Mama Janeth Magufuli, akiongozana na Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na mwakilishi wa BAKWATA Sheikh Alhad Mussa Salum wakielekea kushuhudia uzinduzi rasmi wa Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida wakisalimia mamia ya wananchi waliofurika kushuhudia uzinduzi rasmi wa Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam leo Septemba 27, 2018.   
 Msafara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  ukipita katika Daraja la Juu la Mfugale (Mfugale Flyover) katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela maeneo ya TAZARA jijini Dar es salaam baada ya uzinduzi rasmi leo Septemba 27, 2018.   

No comments:

Post a Comment