Thursday, September 27, 2018

NAIBU WAZIRI WA ARDHI ABAINI UJANJA UNAOFANYWA NA WAMILIKI WA MASHAMBA KILOSA MOROGORO


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akiangalia uwekezaji uliopo katika shamba la Farm Africa Agro Focus (T) Ltd kwa kutumia ndege ya anga (Drones) wakati akikagua mashamba yaliyopo katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro. Anayechukua picha ni Afisa Habari wa Wizara ya Ardhi Hassan Mabuye.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akikagua eneo la shamba la Magore wakati akikagua mashamba yaliyopo katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akioneshwa eneo la shamba la Farm Africa Agro Focus (T) Ltd na Meneja wa Shamba hilo Venkat Chelikani wakati akikagua uwekezaji wa mashamba katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akisalimiana na Ofisa Uhamiaji mara baada ya kuwasili katika wilaya ya Kilosa kukagua uwekezaji wa mashamba katika wilaya hiyo jana.
 
 
Na Munir Shemweta, Morogoro


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amebaini ujanja wa baadhi wa wawekezaji katika mashamba makubwa wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro kumilikishwa mashamba huku wengi wao wakiwa hawajaendeleza jambo alilolieleza kuwa ni kinyume na taratibu za uwekezaji.

Aidha, Mabula alijionea jinsi baadhi ya mashamba yakionekana kwa nje kama yameendelezwa lakini kwa ndani hakuna kitu kilichofanyika na badala yake umiliki unaendeshwa kinyume kabisa na taratibu za umiliki mashamba hayo.

Akiwa katika ziara yake ya siku moja katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro jana, Mabula alisema lengo la kutembelea mashamba ya uwekezaji katika wilaya hiyo ni kubaini wawekezaji wasiofuata taratibu za uwekezaji mashamba na kutoa rai kuwa wale wote wasiozingatia sheria za uwekezaji basi mashamba yao yatafutwa.

Alisema yeye na timu yake wamebaini ujanja unaofanywa na baadhi ya wawekezaji wa mashamba kwa kuhodhi maeneo makubwa huku wakiwa hawayaendelezi na kubainisha kuwa kazi ya kutoa mapendekezo ya kunyang’anywa mashamba kwa wale wasiyoyaendeleza ishaanza kufanywa na halmashauri husika huku baadhi ya mashamba yakiwa tayari yamefutwa na kusisistiza kinachoangaliwa ni kama wamiliki wamefuata sheria.

Hata hivyo, alizitaka halmashauri wakati wa kupendekeza kufuta baadhi ya mashamba ni lazima zihakikishe zinatoa wito wa kushindwa kuendeleza shamba kwa muwekezaji ndipo taratibu za kufuta umiliki zifanyike hasa baada ya kujiridhisha kuwa mmiliki ameshindwa kabisa kufuata taratbu za uwekezaji ndipo anyang’anywe.

Alisema, lengo la kuyachukua mashamba kwa walioshindwa siyo kwa ajili ya kuyagawa tu kwa wananchi bali ni kuyagawa kwa wawekezaji wengine wenye nia njema ya uwekezaji katika sekta husika, kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, kuwapatia ardhi wale wananchi wasiokuwa na ardhi kabisa pamoja na kuwa na ardhi ya akiba itakayosaidia katika shughuli za uchumi.

Huku akitumia ndege ya anga (Drones) kuangalia uwekezaji wa mashamba Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alikagua mashamba ya wawekezaji ya Farm Africa Agro Focus (T) Ltd, Sadrudin Rajabah Meghs la Chanzuru, MS Sino Dev Co lililopo Kimamba, Sumagro Limited Co la Madoto, Noble Agricultural Enter lililopo eneo la Mvuni, New Msowelo Farm pamoja na mashamba ya Magore.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi alisema wilaya hiyo ina mashamba mengi na yenye rutuba lakini tatizo ni kuwa asilimia tisini ya mashamba katika wilaya yake ni mapori na mpango wa serikali ya kuchukua mashamba yasiyoendelezwa na kupatiwa watu wengine wenye nia ya kuwekeza.

No comments:

Post a Comment