Sunday, September 30, 2018

MKUU WA WILAYA ARUMERU AWAHIMIZA WAFANYABIASHARA KULIPA KODI KWA WAKATI


Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wafanyabiashara iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi. Semina hiyo imefanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu, Diana Masalla akiwaelimisha wafanyabiashara kuhusu mabadiliko ya Sheria za Kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Afisa Kodi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Shaban Makumlo akitoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kodi wakati wa semina ya wafanyabiashara iliyofanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu, Adelaida Rweikiza akiwaelimisha wafanyabiashara kuhusu Mfumo wa Maadili kwa Watumishi wa TRA wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wakifurahia hotuba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Jerry Muro wakati wa ufunguzi wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya Mabadiliko ya Sheria za Kodi, Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya Kodi na Mfumo wa Maadili kwa watumishi wa TRA. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO)


……………………….


Na Veronica Kazimoto,Arumeru

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amewahimiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati ili kufikia azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza wakati akifungua semina ya wafanyabiashara hao iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkuu wa Wilaya huyo amesema kuwa, maendeleo yanayopatikana kutokana na kodi, hayawanufaishi walipakodi pekee bali taifa zima kwa ujumla.

“Ndugu zangu wafanyabiashara kodi mnazolipa ndio zinaiwezesha serikali kujenga nchi na kutoa huduma mbalimbali za jamii kama vile elimu, afya, miundombinu ya usafirishaji, maji, umeme na mengine mengi,” alisema Muro.

Aliongeza kuwa, nchi nyingi zilizoendelea duniani, wananchi wake hulipa kodi kwa wakati na hiari, hivyo ili Tanzania ifikie uchumi wa kati na wa viwanda ni lazima wananchi wajenge tabia ya kulipa kodi kwa wakati.Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo, amewasisitiza wafanyabiashara hao kutumia Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFD) na kuhakikisha wanatoa risiti kila wanapouza bidhaa au huduma mbalimbali kwani mashine hizo huwasaidia kutunza kumbukumbu na kujua mwenendo wa biashara zao.

Kwa upande wake Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Diana Masalla alisema kuwa, lengo la semina hiyo ni kuongeza uelewa juu ya Mabadiliko ya Sheria za Kodi, Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya Kodi na Mfumo wa Maadili kwa watumishi wa TRA.

Semina za wafanyabiashara na watumishi wa TRA katika Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimemalizika ambapo watumishi wamesisitizwa kuzingatia maadili wakati wafanyabiashara wametakiwa kuchangamkia msamaha wa riba na adhabu na kutoa taarifa pale ambapo mtumishi yeyote wa TRA atajiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwa ni pamoja na kuomba au kupokea rushwa.

No comments:

Post a Comment