Wednesday, August 1, 2018

WATANZANIA UGHAIBUNI WARUDI KUWAKOMBOA WANANCHI WENZAO KWA MISAADA YA JAMII

Na Ahmed Ally Abdallah, Swahilivilla Tanzania
Tanzania ni moja kati ya nchi yenye watu wengi waliyopo ughaibuni hasa Amerika, na mara nyingi wajapo katika nchi yao jamii zao huwapokea kwa shangwe na nderemo kwani huamini kua, baraka zimewajia katika makaazi yao, baraka ambazo kwa kiasi kikubwa husaidia kupunguza matatizo yao hasa kwa kundi la wanawake na watoto waliyowengi kwa idadi na wanaokabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha zinazowasumbua kila kunapo kucha.
Hata hivyo, ugeni wa leo si wajana, maana si wote wanaopenda kuwa wageni wa nyumbani kwao wanapotoka, na mbaya zaidi, mara tu wanapoondoka na kuelekea huko ughaibuni, husahau kuwa huko walipotoka wamewaacha kina mama na watoto wenye changamoto nyingi zinazowakwamisha kujiletea maendeleo, hasahasa kwa wale wanaoishi vijijini au sehemu za mashamba. Ni watu wachache tu katika wale waliotoka Tanzania kuelekea Amerika ambao hukumbuka nyumbani kwao, asili yao, shida zao na shida za ndugu zao, kiasi cha kuunda vikundi vinavyo waunganisha wao wa ughaibuni na waliyopo nyimbani Tanzania ili kuzikwamua jamii zilizonasa kwenye mtego wa umasikini, njaa, shida za kijamii na changamoto nyingine nyngi za kimaisha hususani katika kundi la wanawake na watoto.
Bi Jessica Kamala Mshala ni miongoni mwa watu mashuhuri kutokea Tanzania huko Bukoba na anaeishi Maryland nchini Marekani, ambaye ameweza kuwakomboa wanawake wengi wa Tanzania katika kujikwamua na wimbi la umasikini, hasahasa kwa kuanzisha shirika la Shina. Inc huko nchini Marekani na kufungua matawi yake katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzani, Kenya, Cameroon na Nigeria, likiwa na dhumuni ya kumhamasisha mwanamke katika Nyanja mbali mbali za kimaendeleo hasahasa uchumi pamoja na kutetea haki za wanawake na watoto.
Shirika hili la Shina Inc ni shirika ambalo halifungamani na upande wowote wa siasa, dini, jinsia na itikadi yeyote, likimaanisha kuwa ni shirika lenye lengo kuu la kumsaidia mwanaadamu na sivinginevyo. Wana diaspora wengi hushirikishwa katika kuhamasishana juu ya suala la kuwasaidia watu wanyumbani huko Afrika kwani ndio asili yao, na hivyo kuzifanya nchi zenye tawi la Shina Inc kupokea misaada mbalimbali pasi ya kukopeshwa au kudaiwa. Kwa sasa ni miaka 16 tangu kuanzishwa kwa shirika hili la Shina Inc, na limeshafanya semina nyingi na miradi kemukemu katika nchi wanachama washirika hili, miradi ambayo imezaa tija tele kwa wanajamii husika. Lakini suali la kujiuliza, je, ilikuwaje mpaka Mama huyu akaweza kuanzisha shirika hili la Shina Inc na kwanini?
Anasimulia bi Jessica “mama yangu aliniusia kua, haki ya mtoto wa kike lazima ipiganiwe, haya yamekua maneno niliyoyazingatia na kunipa uzingatifu mkubwa na ujasiri wa kutekeleza busara hii pevu aliyonitunukia mama yangu, kiasi cha mimi na mume wangu bwana Amos Mushala, ambae ni Patron wa SHINA, Inc kuungana ili kutekeleza azma hii ya ukombozi wa mwanamke kifikra, kielemu na kwa kumuwezesha kujitegemea”.
Si kila mtu huipata bahati ya kwenda nje hasahasa katika nchi za kimagharibi kwa kusoma au kutafuta maisha, na miongoni mwa hao waliobahatika asilimia kubwa husahau shida na matatizo yanayowafika ndugu zao Waafrika, kiasi cha kusema kua, msemo huu wa Mcheza kwao hutunzwa husahaulika na mioyo yao ikiamini kua, kila mmoja huchuma kwa nguvu yake na hula kwa jasho lake dhana ambayo si sahihi, lakini si bi Jesica na wafuasi wake wa shina Inc, wao wazo hili potofu wameliweka pembeni na kuendelea kuutendea kazi msemo huu wa “Mcheza kwao hutunzwa” ipasavyo.
Mwaka 2018, jogoo likawika nchini Tanzania bara na visiwani, ziara ya bi Jessica na rafiki zake wa Marekani walionekana kuja kutembelea jamii za wa Tanzania, na hivyo ziara ya kwanza ilianza huko Ilemela sehemu ambayo waliweza kufanya semina iliyotunukiwa jina la Jitambue kama kikundi kwa watu 700 pamoja na vikundi 30 kwa idadi kutoka katika sehemu mbalimbali, lengo kuu ya semina hii ilikua ni kuwahamasisha kina mama kujikwamua kiuchumi, kijamii na nyanja nyengine za kimaendeleo, hata hivyo safari hii iliambatana na ufunguzi wa jengo la kuhamasishana na kusaidiana wanawake kiuchumi lililosaidiwa ujenzi wake kupitia shirika hili la Shina Inc, jengo ambalo lilipewa jina la TAG Itika Women Centre, nao wanawake wa kijiji hicho cha Ilemela wakaitika wito waliyoitwa na Bi Jessica.
Jua lilipochomoza na kutoa nuru iliyong’ara kila pembe, ndipo bi Jessica na marafiki zake walipoongoza njia kuelekea huko Bugorora, kijiji kinachopatikana wilaya ya Misenye mkoa wa Kagera, ndipo hapo hodi iliyohodishwa na Shina Inc ikaitikiwa na watu wa vikundi tofauti ikiwemo kikundi cha kina mama kinachoitwa Bugorora Kata Groups, kwa kua shina Inc husaidia jamii zilizowagusa kwa kushuhudia wenyewe tatizo hilo uso kwa macho, ndipo hapo walipoanza kushuhudia shida za jamii hiyo ikiwemo uhaba wa vitabu kwa wanafunzi wa shule zilizopo katika eneo hilo la Bugorora, kuwepo na makundi ya kujikwamua kimaendeleo ambayo yamekosa msaada wa kifedha, vifaa na hata elimu ya kujiongoza wenyewe, mbaya zaidi wanafunzi kukosa majengo ya kujisomea na badala yake kusoma chini ya mti. Ndipo hapo Shina Inc lilipojikagua mifuko yake na kutoa kile ambacho wamekikusanya kutoka kwa rafiki zao ili kuikwamua jamii ya watu hao, na uzuri zaidi, bila ya kuangalia dini, kabila, jinsia, umri, itikadi wala asili, shina Inc ikapiga la mgambo lililoitikiwa na vikundi zaidi ya 12 vyenye jumla ya watu 700 ili kuja kujifunza namna ya kujikwamua kiuchumi.
Miongoni mwao ni Roman Catholic Supportive, Answarin kutoka Muslim Mureba, Ruzinga Dance Troops, Spirituality and Health Programs ambavyo ni vikundi vya dini kutokana na makanisa mbali mbali na uzuri zaidi, shekhe mkuu wa wilaya ya Misenyi ambaye ni Shekhe Abdul alikua ni mmoja kati ya watu waliyohudhuria katika semina hiyo, hii ni kuashiria kua, licha bi Jessica na mumewe kua watu wanaofuta imani ya dini ya kikiristo, lakini hufanya kazi zao na watu wa itikadi mbaimbali, yote haya ni kutokana na kuguswa na matatizo ya jamii na wala sio dini fulani.
Safari yao iliendelea katika kijiji cha Bugandika, sehemu ambayo bi Jessica alifutwa tongo na mama yake bi Kokwitika ambaye alikua ni mkuu wa wanawake hapo Bugandika, na mwaka 1988 akauacha ujumbe mzito kwa bi Jessica wa kuwakomboa na kutetea wanawake wenzake, kiasi cha kumfanya bi Jessica kuchukua bidhaa za kina mama wa Bugandika ambazo ni mikeka, majamvi na bidhaa nyengine za asili ambazo alizisafirisha kwa shida mno kuelekea huko Marekani ili kuwatafutia soko madhubuti la kuuzia bidhaa zao, na kile kilichopatikana kikarudi mikononi mwao, hapo ndipo wanawake wa jamii hii ya Bugandika wakapa pumzi za kuvuta kiasi cha kuwaongezea kipato chao na siku za kuendelea kuishi. 

No comments:

Post a Comment