Na Dixon Busagaga wa
Globu ya Jamii kanda ya Kaskazini.
JESHI la Polisi mkoa wa Kilimanjaro limefanikiwa kukamata viroba saba vya Dawa za kulevya aina ya Mirungi sawa na kilogramu 520 zikiwa zimebebwa na watembea kwa miguu ambao walikuwa wakivusha kutoka nchi jirani ya Kenya kuingia Tanzania.
Mbali na viroba hivyo Polisi pia inamshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Samwel Muro(21) raia wa Kenya mkazi wa Kitobo baada ya kukutwa akiwa amebeba kichwani moja ya Viroba hivyo huku wengine kadhaa wakifanikiwa kuwakimbia askari baada ya kutupa mizigo ya dawa hizo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa KilimanjaroKamishna Msaidizi wa Polisi Hamis Issah alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo jana majira ya 8:30 mchana pamoja na pikipiki moja iana ya Haojue yenye namaba za usajili MC 909 BUZ ambayo inatajwa kuhusika katika usafirishaji wa mizigo hiyo.
“Hii mirungi ilikamatwa katika kijiji kinachoitwa Mnoa, kata ya Kileo wilayani Mwanga. Askari Polisi wakiwa doria walikamata viroba saba vya mirungi na walienda kwenye bonde moja na kukuta watu wametoka Kenya wamejaza hii mirungi kwenye magunia wakiwa wameificha kwenye hilo bonde.
"Kumbe wana utaratibu wao bonde likijaa wanachukua pikipiki zaidi ya 30 kwa ajili ya kusafirisha mirungi na wanasafiri kwa makundi makubwa ya pikipiki”, alisema Kamanda Issah.
Kamanda Issah alisema baadhi ya vifurushi hivyo vya Mirungi vimekutwa vikiwa vimeandikwa majina ya vijiji kuanzia njia Panda ya Himo kuelekea Dar es Salama yakiwemo maeneo ya Segera, Chalinze hadi Kibaha.
Mtuhumiwa wa usafirishaji wa Dawa za kulevya aina ya Mirungi akiwa kwenye gari la polisi na viroba vilivyojaa dawa hizo za kulevya zilizokamatwa katika moja ya bonde mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Askari polisi wakishusha viroba vyenye dawa za kulevya aina ya mirungi kituo kikuu cha polisi Kilimanjaro.
Mtuhumiwa wa usafirishaji wa Mirungi Samwel Muro mkazi wa Kitobo nchini Kenya akiwa chini ya ulinzi na pemebeni yake ni vifurushi vyenye mirungu alivyokutwa navyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Hamis Issah akitoa maelekezo kwa askari wake mara baada ya kukamatwa kwa mirungi hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Hamis Issah akiumuuliza jambo raia wa Kenya Samwel Muro aliyekutwa akiwa amebeba moja ya vifurushi kwa ajili ya kusafirishwa kutoka mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ACP Hamis Issah akionesha moja ya kifurushi cha mirungi kilichoandikwa jina la mji wa Kibaha.
No comments:
Post a Comment