Monday, August 6, 2018

NEWS ALERT: MWANAHABARI MKONGWE ERNEST SUNGURA ATEULIWA KUWA KIONGOZI MKUU VYOMBO VYA HABARI VYA CCM


*Kuongoza mageuzi makubwa ya vyombo hivyo
*Ni baada ya kufanya maboresho makubwa katika tasnia ya habari nchini


Na Derek Murusuri, Dar Es Salaam



USEMI maarufu katika vitabu vifakatifu kuhusu jiwe lililokataliwa na waashi kuwa jiwe kuu la pembeni, unasadifu uteuzi wa gwiji la habari nchini, Ernest Samson Sungura, kuongoza mageuzi makubwa ya vyombo vya habari vya CCM.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya vyombo vya habari vya CCM zinasema kuwa uteuzi wa Comrade Sungura umetangazwa leo jijini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali, ambaye alisema uteuzi huo umeidhinishwa na Kamati Kuu ya CCM.



Comrade Sungura sasa anakuwa Kiongozi Mkuu wa vyombo vya habari vya CCM, aliyepewa jukumu kubwa la kufanya mageuzi ya kimuundo na kimfumo (restructuring) ya vyombo hivyo na kuvifanya vitoe ushindani madhubuti (competitive) katika tasnia ya habari ndani na nje ya nchi.

Kabla ya uteuzi huo, Sungura alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa vyombo vya habari Tanzania (TMF) lakini aliondolewa katika taasisi hiyo na Bodi yake (TMF) muda mfupi baada ya kutangazwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC). 


Sungura ndiye mwasisi wa Tanzania Media Foundation (TMF), taasisi iliyoleta mageuzi makubwa katika tasnia ya habari nchini na kuifanya nchi jirani ya Kenya kuja kujifunza nchini kabla ya kuanzisha taasisi kama hiyo nchini mwao.
Comrade Sungura ndiye anatarajiwa kuviongoza vyombo vya habari vya CCM katika mageuzi haya makubwa. Vyombo hivyo ni pamoja na televisheni, redio, magazeti na vile vya mtandaoni ambavyo katika siku za karibuni vimetokea kuwa na wafuasi wengi duniani.

Pamoja na mafanikio mengine, Sungura amekuwa na rekodi nzuri na ya kipekee katika kuleta mageuzi ya kimkakati kwa taasisi za habari nchini.

Baadhi ya mafanikio makubwa yameonekana katika kuzipatia taasisi hizo uongozi na menejimenti madhubuti, hivyo kuleta maboresho katika maudhui, miundo na mifumo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha vyanzo vya mapato na kusaidia vyombo vya habari kujiendesha kama taasisi kamili zinazopata faida.  

Sungura ana uzoefu wa zaidi ya miaka 24 (1994-2018) katika tasnia ya habari nchini, hasa katika kuwajengea uwezo wanahabari vijana huku akibuni program mbalimbali za kuijenga na kuiimarisha tasnia ya habari.


Amekuwa anajulikana kwa wengi kama kiongozi mahiri mwenye kujali matokeo, kocha, menta (mentor), mshauri wa kitaalam na mwalimu.  


Disemba 2017, Comrade Sungura alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mwezi Mei mwaka huu, alikuwa miongoni mwa wajumbe tisa (9) waliopendekezwa na Mwenyekiti wa CCM Dk John Pombe Magufuli kugombea nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu ya CCM.  

Wakati akichukua uongozi wa Chama, Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli, aliahidi kuleta mageuzi katika vyombo vya habari vya chama hicho ili kuvifanya kuwa mshindani mzuri katika sekta ya habari ikiwa ni pamoja na kuwa mhimili katika kusaidia mabadiliko ya kiuchumi nchini.

Sekta ya habari na mawasiliano ni muhimu sana katika siasa za dunia, ikiwemo Tanzania, hasa katika kutoa ushawishi na uungwaji mkono wa mikakati na sera za Chama cha kisiasa kwa umma. 


Mafanikio makubwa ya tasnia ya habari katika muongo mmoja uliopita, kwa kiasi kikubwa umetokana na juhudi kubwa alizozifanya Sungura kupitia taasisi aliyoiongoza ya TMF.

Bodi ya TMF ilimshinikiza Sungura aondoke katika wadhifa wake kama Mkurugenzi Mtendaji wa TMF baada ya kushinda katika uchaguzi uliomwingiza katika chombo kikubwa cha maamuzi cha CCM, NEC.

Sungura ni miongoni mwa wanahabari makini na wenye rekodi ya ufuatiliaji ambao wamepitia mafunzi katika fani zaidi ya uandishi wa habari.


Sungura ana uwezo mkubwa, amebobea katika fani ya habari, usimamizi wa biashara, mafunzo ya wanahabari, ikiwa ni pamoja na uandaaji wa mikakati na pia ni mtu asiyeshindwa jambo analokabidhiwa, hakika CCM imefanya uchaguzi sahihi, alisema Flora Magabe.


Sungura ndiye mwasisi wa mabadiliko ya maboresho yaliyosaidia kuongeza uwezo na weledi katika sekta ya habari nchini ndani ya  muongo mmoja uliopita (transformation of the media sector in Tanzania). 


Maboresho hayo pia yalilenga katika kuzifanya taasisi za habari zijitegemee kiuchumi na hivyo kuziwezesha kuwa huru katika maamuzi ya kiuhariri.


Comrade Sungura amewahi kufanya kazi na taasisi za kimataifa kama vile shirika la umoja wa mataifa la Elimu, sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika kuboresha matangazo ya vyombo vya habari vya umma (Public Broadcasting Services) kama vile TBC na ZBC, kazi ambayo aliifanya kwa ufanisi mkubwa.


Sungura ana Digrii ya Uzamili katika usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam,  Digrii ya Kwanza katika Usimamizi wa Biashara kutoka katika Chuo hicho hicho na Diploma ya Uandishi wa Habari kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania, TSJ (sasa SJMC). 

No comments:

Post a Comment