Wednesday, August 1, 2018

Dkt. Shein akutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Jimbo la Gorontalo na Kiongozi wa Kampuni ya gesi nchini Indonesia


 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwa katika mazungumzo na Makamo wa Rais wa Indonesia Muhammad Jusuf Kalla ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao walisisitiza haja ya kuzidisha ushirikiano katika sekta za maendeleo.

 Viongozi hao walifanya mazungumzo katika Ofisi ya Makamo wa Rais wa Indonesia Muhammad Jusuf Kalla iliyopo mjini Jakarta Indonesia, ambapo mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mawaziri wa pande zote mbili. Katika mazungumzo hayo Rais Dk. Shein alimpongeza Makamo wa Rais wa nchi hiyo kwa muwaliko wake huo muhimu ambao unaimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Indonesia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla na makhsusi kwa Zanzibar. 

 Dk. Shein alimueleza Makamo huyo wa Rais wa Indonesia kuwa Tanzania inajivunia kwa kiasi kikubwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo ambao umeasisiwa na viongozi wakuu wa nchi hizo tokea miaka ya sitini na kuahidi kuwa utaendelezwa. 

 Alieleza kuwa tangu mwaka 1964 kulikuwa na uhusiano na ushirikiano mkubwa kati ya Zanzibar na Indonesia hasa katika biashara ya karafuu ambapo wakati huo zao hilo lilikuwa likizalishwa kwa wingi zaidi na bei yake kuwa juu katika soko la dunia, Indonesia ikiwa moja ya wanunuzi wakubwa. Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Indonesia imekuwa ikiunga mkono juhudi za Zanzibar kwa kusaidia maeneo mbali mbali yakiwemo ya kuwajengea uwezo wananchi hasa katika sekta ya elimu na kilimo na kusisitiza haja ya kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano. 

 Kwa upande wa sekta ya kilimo Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuongeza uzalishaji wa mpunga sambamba na kuangalia kilimo cha mwani na mazao yake. 

 Dk. Shein alieleza haja ya kuirejesha biashara ya karafuu sambamba na kuwawezesha vijana kujiajiri katika kilimo kwa kuwapatia taaluma ya teknolojia mpya kwenye kilimo cha mikarafuu. Kwa upande wa eneo la uvuvi ambapo ni eneo jipya la ushirikiano, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema na eneo hilo likaangaliwa kwa upeo mkubwa zaidi hasa katika kuimarisha uvuvi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwenye kuvua, hasa katika bahari kuu. 

 Akieleza kuhusu sekta ya utalii, Rais Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa katika kuhakikisha idadi ya watalii inaongezeka hasa ikizingatiwa kwamba sekta hiyo inachangia asilimia 80 ya mapato ya serikali kwa fedha za kigeni sambamba na kuchangia kiasi kikubwa katika pato la Taifa.

 Aliongeza kuwa katika sekta ya utalii katika kipengele cha ukarimu ni vyema yakaimarishwa mashirikiano kati ya pande mbili hizo hasa ikizingatiwa kuwa Indonesia tayari imeshapata mafanikio makubwa. Dk. Shein alieleza kuwa mbali na juhudi hizo pia, hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha utalii wa Zanzibar unatangazwa na kusisitiza kuwa ili utalii uweze kutangazwa vizuri ni vyema kukawa na njia nzuri za kuwasafirisha watalii.

 Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kueleza haja ya kuwepo na kuimarisha ushirikiano katika Nyanja ya utafiti na maendeleo ambalo ni eneo jengine la ushirikiano na kupelekea taasisi za elimu kuhusishwa ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Taasisi ya Afya pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo. 

 Alieleza kuwa taasisi hizo ni vyema zikashirikiana na zile za Indonesia, katika nyanja mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kubadilishaja taaluma na uzoefu chini ya Mpango wa ushirikiano wa Nchi za Kusini mwa Dunia hasa katika sekta ya utalii,kilimo, afya na elimu. 

 Dk. Shein alieleza kuwa tayari Zanzibar ina Vyuo vitatu vya Amali kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana wa kujiajiri, hivyo aliona haja kwa Mawaziri husika kukutana pamoja kujadili namna bora ya kushirikiana katika nyanja hiyo. Akieleza kuhusu suala zima la uchumi wa kisasa, Rais Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuwepo kwa mashirikiano katika kuimarisha uchumi wa kisasa kwa kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika miradi ya miundombinu, kwa njia ya mashikiano na sekta binafsi. Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimualika Makamo huyo wa Rais wa Indonesia kuhudhuria katika sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hapo Januari mwakani ambapo kiongozi huyo alikubali mwaliko huo. 

Nae Makamo wa Rais wa Indonesia Muhammad Jussuf Kalla kwa upande wake alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kukubali mwaliko wake huo na kumueleza kuwa Indonesia itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo ambao umewekwa na waasisi wa Mataifa hayo.

 Makamo wa Rais huyo alieleza kuwa uhusiano huo ulianza kutoka kwa Baba wa Taif Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Baba wa Taifa hilo Soekarno Hatta. Katika maelezo yake, kiongozi huyo alieleza kuwa kuna haja ya kuongeza mashirikiano hasa katika sekta ya biashara kati ya pande mbili hizo hasa kutokana na soko kubwa la biadhaa za nchi hio kwa Afrika. 

 Akieleza katika sekta ya utalii, Makamo huyo wa Rais ameleza kuwa kuwepo kwa mashirikiano kati ya pande mbili hizo kutasaidia kuimarisha sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ina vivutio vingi vya kitalii zikiwemo fukwe nzuri. 

 Alieleza kuwa kutokana na Indonesia kuwa na Chuo Maalum cha Kitalii wanaona haja ya kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya utalii katika Nyanja ya mafunzo. Kiongozi huyo pia, aliahidi kuunga mkono katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutoa mafunzo hasa katika kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga na kueleza haja ya vijana wa Kizanzibari kwenda kujifunza nchini humo kutokana na nafasi maalum watakazozitoa. 

 Makamo wa Rais, alieleza kuwa mmano Agosti 26 mwaka huu Indonesia itafanya mkutano wa Kimataifa wa Kilimo ambao utagusia kilimo cha mpunga na kutafuta njia za kuwasaidia vijana katika kuhakikisha wanajihusisha na kilimo. 

 Aidha, alitilia mkazo suala la kubadilishana uzoefu kwa vijana huku akieleza namna ya kuwasaidia vijana kwa kuwapa ufadhili katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo utalii, uvuvi, mifugo na kilimo. Aliongeza kuwa nchi yake imekuwa ikitoa mafunzo ya amali kwa vijana na kueleza kuwa mbali ya mafunzo hayo pia, wako tayari kuengeza maeneo mengine yakiwemo uvuvi, utalii, mifugo na kilimo kwa vijana wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment