Sunday, July 8, 2018

WAZIRI MKUU AKEMEA MAAFISA USHIRIKA WENYE VISINGIZIO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya kutowajibika miongoni mwa watumishi kwa kisingizio cha mgawanyo wa madaraka.

Ametoa onyo hilo jana (Jumamosi, Julai 7, 2018) wakati akizungumza na wanaushirika na mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini humo.

Amesema kuna maafisa ushirika ambao hawataki kuwajibika kwa sababu wameajiriwa TAMISEMI na wengine wako chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

"Afisa Ushirika wa Wilaya yuko mkoani ambako ni chini ya TAMISEMI, Mrajis Msaidizi wa Mkoa yuko Wizarani. Serikali ni moja, kwa hiyo wote bado mnawajibika kwa Mrajis Msaidizi wa Mkoa," alisema.

Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri (DED) wasiwapangie kazi nyingine zilizo nje na taaluma yao maafisa ushirika wa wilaya na wahakikishe wanatoa taarifa kwenye vikao vya Halmashauri zao.

"Msimpe kazi ya kufundisha Afisa Ushirika kwa sababu hakuna mtu mwingine. Afisa Ushirika aachwe afanye kazi ya ushirika na atoe taarifa kwenye vikao vyenu. Madiwani mnapokutana kwenye Baraza, mpeni nafasi Afisa Ushirika aeleze maendeleo ya ushirika yakoje katika wilaya yenu."

Alisema changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya ushirika ni wizi na ubadhirifu miongoni mwa watendaji wa vyama vya ushirika waliopewa dhamana ya kuvisimamia na kuviendesha vyama hivyo.

Alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa elimu ya kutosha ya ushirika miongoni mwa wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika; kuporomoka kwa imani ya ushirika miongoni mwa jamii na kwa baadhi ya wanachama kutokana na vyama vya ushirika kushindwa kukidhi mahitaji ya wanachama wake.

Nyingine ni uwepo wa madeni makubwa katika baadhi ya vyama vya ushirika nchini na baadhi ya viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara kuwa na mtazamo hasi kwenye ushirika kwa malengo ya upotoshaji kwa maslahi yao binafsi.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Waziri Mkuu aliitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika ihakikishe kwamba usimamizi, udhibiti, uhamasishaji wa vyama vya ushirika unafanyika kikamilifu na kwa wakati kwa kuzingatia Sheria ya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na kanuni zake za mwaka 2015.

Pia aliiagiza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika iwasaidie wanaushirika katika mchakato wa urasimishaji wa mali zao na utoaji wa hati miliki za kimila za kumiliki ardhi kwa wakulima wadogo wadogo vijijini ili waweze kuzitumia kama dhamana ya kukopa mikopo katika taasisi za kifedha kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi

Aidha alizitaka mamlaka zote zinazohusika na maendeleo ya sekta ya ushirika nchini zijiwekee malengo yanayotekelezeka ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya ushirika na kujipima kila inapohitajika.

Siku ya Ushirika Duniani huadhimishwa Jumamosi ya kwanza ya Julai kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Ushirika kwa ulaji wa uzalishaji endelevu wa bidhaa na huduma.”

No comments:

Post a Comment