Friday, July 6, 2018

WAZIRI JENISTA MHAGAMA AIPONGEZA WCF KWA KUINGIA KWENYE MFUMO WA TEHAMA KATIKA KUTOA HUDUMA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Jenista Mhagama, amefurahishwa na mwitikio wa waajiri kujisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) baada ya kuanza kushuhudia jinsi wafanyakazi wao wanavyonufaika na malipo ya Mafao ya Fidia.
Mhe. Waziri ameyasema hayo leo Julai 6, 2018 baada ya kutembelea banda la WCF kwenye maonesho ya 42 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere (Maarufu kama Sabasaba) jijini Dar es Salaam.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru waajiri wote nchini ambao wameitikia wito wa Serikali wa kujisajili na Mfuko kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi. Nimetaarifiwa kuwa mpaka sasa jumla ya waajiri 14,855 wamesajiliwa na Mfuko. Na kinachonifurahisha zaidi ni kwamba sasa waajiri wameanza kuona manufaa ya kuanzishwa kwa Mfuko baada ya kushuhudia jinsi wafanyakazi wao wanavyonufaika na mafao yanayolipwa na Mfuko” Alisema Mhe. Waziri.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, kwa mwaka wa fedha uliomalizika (2017/2018), tayari Mfuko ulikwishalipa mafao ya jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa wanufaika 812.” Alisema Bw. Mshomba.
Halikadhalika Bw. Mshomba alisema Mfuko umekuwa na faida sio tu kwa wafanyakazi na waajiri lakini pia hata kwa serikali kupitia kodi, ambapo alisema Mfuko umelipa kodi serikalini kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kama kodi kwa mwaka wa 2016/2017 na mwaka huu ulioisha Juni 2018 tunatarajia kulipa zaidi ya shilingi bilioni 5 kama kodi ya serikali.

Aidha, Mhe. Waziri Jenista Mhagama aliupongeze Mfuko na waajiri kwa kushirikiana pamoja katika kutekeleza sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, kwani mafanikio haya ni matokeo ya kufanya kazi kwa kushirikiana.

“Kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza siku zote, nia ya serikali ni kuona majukumu yote yanayohusu fidia kwa wafanyakazi yanafanywa na Mfuko huu na hivyo kuwawezesha waajiri kubakia na jukumu la kubuni mbinu za kuongeza uzalishaji na kukuza biashara zao.  Hivyo, nitoe wito kwa waajiri ambao bado hawajajisajili na ambao hawalipi michango watekeleze wajibu wao kwa hiari bila kuchelewa.” Alisema Mhe. Waziri.

Aidha, Mhe. Waziri aliuagiza Mfuko uendelee kuchukua hatua mbalimbali za kisheria kwa waajiri ambao wataendelea kutokutekeleza wajibu wao wa kujisajili na kuchangia kwa mujibu wa sheria.
Waziri Muhagama pia aliupongeza Mfuko kwa kupanua mfumo wa utoaji huduma kwa kuanzisha matumizi ya Tehama kwa kutumia Mfumo wa kielektroniki. 
“Niupongeze Mfuko kwa kuwekeza katika mfumo wa kielektoniki ambayo inasaidia sana utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao. Nimeoneshwa namna ambavyo mwajiri anaweza kujisajili, kupata hati ya usajili, kulipa michango ya kila mwezi na kupata stakabadhi kwa njia  kielektroniki. Mwajiri anaweza kupata huduma zote akiwa ofisini kwake. Haya ni mafanikio makubwa sana yaliyofikiwa na Mfuko katika kipindi kifupi cha miaka miwili ya utaoaji wa huduma. Nitoe wito kwa waajiri, kutumia mifumo hii ambayo ni rahisi kutumia na ni rafiki kwa watumiaji.” Alisema Mhe. Waziri.
Mheshimiwa Waziri aliwahimiza waajiri kuwa na taarifa sahihi za wafanyakazi wao “ili Mfuko uweze kulipa fidia bila kuchelewa, ni lazima mshirikiane katika kuhakikisha nyaraka muhimu zinazohitajika katika ulipaji wa fidia zinaufikia Mfuko kwa wakati. Nitoe rai kwa waajiri kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya matukio ya majanga yanayotokana na kazi mapema pamoja na nyaraka muhimu zinazohitajika katika ulipaji wa fidia.
  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, (wapili kushoto), Naibu Waziri wa Viwanda, Bishara na Uwekezaji, Mhe. Eng. Stella Manyanya, (wakwanza kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba wakipatiwa maelezo na wataalamu wa Mfumo wa Kielektroniki wa Mfuko huo, Bw.Uforo Henry, (wapili kulia) na Abdi Kalilo wakati Mhe. Waziri na Naibu Waziri walipotembelea banda la Mfuko huo kwenye maonesho ya 42 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Julai 6, 2018.



Waziri Mhagama akimsikilzia  Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Masha Mshomba, wakati akifafanua baadhi ya mambo kwa waandishi wa habari.
 Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, (kulia), akimuongoza Mhe. Waziri wakati akitembeela banda la Mfuko huo leo Julai 6, 2018.
 Waziri Jenista Mhagama, akimsikilzia Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Anselim Peter, wakati akifafanua kuhusu mfumo mpya wa Kielektroniki ambao WCF umeanza kuutumia katika kusajili na kupokea michango ya wananchama
 Maafisa wa WCF wakiwa wamesimama kwenye lango la kuingilia kwenye banda hilo tayari kupokea wananchi.

 Bw. Mshomba, (kulia), Bw. Anselim Peter (Kushoto), wakibadilishana mawazo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii, (SSRA), Bi. Sarah Kibonde Msika, nje ya banda la WCF.
Mhe. Waziri akipokelewa wakati akiwasili kwenye banda la WCF.
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, WCF, Bi. Laura Kunenge (kulia) na mwenzake wa SSRA, Bi. Sara Kibonde Msika, wakibadilishana mawazo kwenye banda la WCF.

 Abdi Kililo (kulia) kutoka kitengo cha Tehama cha WCF, akitoa maelezo kwa wananchi hawa waliotembeela banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Wakwanza kulia ni Afisa anayeshughulikia masuala ya Sheria wa Mfuko huo, Bi.Fransisca Kweka.
 Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, akiwa na Dkt.Damian Elias kutoka kitengo cha Huduma za Tiba na Tathmini Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
 Afisa Uhusoano Mwandamizi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Sebera Fulgence, (kushoto), akiwa na Justin Mwandumbya wa kitengo cha fedha
Maafisa wa WCF, Glady Madembwe, kutoka kitengo cha madai (Claims) (kushoto) na Afisa wa Afya na Usalama mahala pa kazi kutoka WCF, Bw. Robert Duguza (wapili kushoto), wakiwahudumia wananchi hawa waliotembelea banda la WCF.

No comments:

Post a Comment