Thursday, July 5, 2018

RC TEMEKE AWAMWAGIA SIFA WOISO ORIGINAL PRODUCTS KWA KUNYAKUA TUZO YA BIDHAA ZA NGUO NA NGOZI

Na Leandra Gabriel , Globu ya Jamii.

MKUU wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva amewataka wananchi hasa watokao katika Manispaa ya  Temeke kujitokeza kwa wingi kushuhudia maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba ili kujipatia elimu ya ujasiriamali.

Lyaniva ametembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo na kujionea kazi za wazalendo wakiwa na bidhaa tofauti zilizotengenezwa hapa nchini wakitilia mkazo kauli ya Rais wa John Pombe Magufuli ya uchumi wa viwanda.

Akizungumza na Globu ya Jamii akiwa ndani  ya banda la bidhaa za nguo na ngozi la Woiso Orginal Company Ltd Lyaniva ameeleza kuwa maonesho hayo yameboreshwa na washiriki wamekuwa wengi kutoka katika nchini mbalimbali duniani.

"Maonesho ya mwaka huu zaidi ya mataifa 50 kutoka nje ya nchi wameweza kushiriki na wameleta bidhaa bidhaa nzuri zikiwa zenye ubora wa hali ya juu,"amesema Lyaniva.

Lyaniva amewapongeza wazalishaji wa bidhaa za nguo na ngozi kutoka kampuni ya Woiso Original Products kwa kuzalisha bidhaa nzuri na zenye ubora wa hali ya juu na kwa bei nzuri ambayo unanunua kitu na utadumu nacho kwa mda mrefu na amewataka wananchi kujitokeza sasa kuona na kujifunza namna bidhaa za kitanzania hasa za ngozi zilivyoshika hatamu kwa ubora wa hali ya juu.

Aidha amewashukuru watanzania walioelewa na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika masuala ya kiuchumi na wamekuja vizuri sana na kuboresha maonesho hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yana tija kwa taifa letu.

Naye Meneja masoko wa Woiso Original Products Company Ltd bi. Teya Herman ameeleza kuwa wao kama kampuni wanajituma sana katika kuhakikisha wanatoa bidhaa bora za ngozi na nguo kama vile viatu, mikanda, pamoja na nguo na mapazia.

Kuhusu tuzo waliyokabidhiwa leo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kassim ya watayarishaji bora wa bidhaa za nguo na ngozi bi. Teya ameeleza kuwa ni mara yao ya 4 kushiriki maonesho hayo na ni mara ya 4 kushinda tuzo hiyo ambapo awali ilijikita katika bidhaa za ngozi na ila kwa sasa imejumuisha bidhaa za ngozi na nguo.

Akielezea changamoto wanazokutana nazo hasa kwenye upatikanaji wa ngozi bi. Taya amesema kuwa upatikanaji wa bidhaa hiyo hauko vizuri  kutokana na uwepo wa alama zilizowekwa na wafugaji na zile zinazotokana na kuchinjwa hali inayopelekea ugumu wakati wa kuandaa bidhaa hizo.

Na ameungana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke akiwaomba watanzania kuunga mkono juhudi za serikali katika kuelekea uchumi wa viwanda kwa kupenda vya nyumbani.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva akimuelezea mwananchi aliyefika kwenye banda la Woiso Original Products Company Ltd wanaojihusisha na uuzaji wa bidhaa za nguo na ngozi wakiwa washindi kwenye kipengele hicho kwa mara ya nne mfululizo katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba 
Meneja Masoko wa Kampuni ya Woiso Original Products Ltd Teya Herman akieleza jambo kwa mkuu wa  Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva akieleza jambo kwa Meneja Masoko wa kampuni ya Woiso Original Products Ltd Teya Herman  alipotembelea banda hilo na kujionea bidhaa zinazotengenezwa na watanzania zikiwa zenye ubora katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba
Meneja Masoko wa kampuni ya Woiso Original Products Ltd Teya Herman akizungunza na Globu ya Jamii akielezea tuzo ya ushindi waliyoipata katika kipengele cha Bidhaa za nguo na ngozi kutoka Tanzania ikiwa ni mara ya nne mfululizo wakishinda katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva akizungumza na Globu ya Jamii akiwa ndani ya banda la washindi wa bidhaa za nguo na ngozi akielezea umuhimu wa watanzania kupenda vitu vya nyumbani ikiwemo kuwaunga mkono Wazalishaji wa ndani wa Viwanda vidogo na vikubwa.

Picha na Emmanuel Massaka Globu ya jamii)

No comments:

Post a Comment