Sunday, July 1, 2018

NHC MNA JUKUMU LA KUWAFIKIA WATU WA CHINI - MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lina jukumu kubwa la kuhakikisha sekta hiyo inakua na kuwafikia watu wa kipato cha chini.

Amesema ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inahimiza uchumi wa viwanda, hivyo sekta ya nyumba ina mchango mkubwa sana katika kuchochea ukuaji wa viwanda.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 30,2018) wakati akizindua mradi wa Singidani Commecial Complex, mjini Singida. Jengo hilo la biashara na ofisi limejengwa na NHC kwa ajili ya kupangisha wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema sekta ya nyumba ni mtambuka kwa kuwa huchochea ukuaji wa uchumi, kutoa ajira na kukuza uwekezaji wa viwanda vya vifaa vya ujenzi kama saruji, mabati, nondo, marumaru na vinginevyo, ambavyo vinafungua fursa kubwa ya ukuaji wa viwanda.

Hivyo, Waziri Mkuu amesema wadau mbalimbali wanapaswa kuitazama sekta ya nyumba kama sekta mtambuka katika kuleta maendeleo endelevu ya uchumi na jamii kwa ujumla.

“Napenda kutoa pongezi kwa Shirika la Nyumba la Taifa kwa kujenga jengo hili zuri na la kisasa kabisa hapa mjini Singida. Vilevile, jengo hili limeboresha na kupendezesha mandhari ya mji wa Singida kwa kiwango kikubwa kabisa,” amesema. 

Waziri Mkuu amesema amefurahi kusikia jengo hilo limesanifiwa na ujenzi wake kusimamiwa na Watanzania wenyewe, wakandarasi washauri wakiwa ni NHC wenyewe na kwamba Watanzania zaidi ya 600 walipata ajira wakati wa ujenzi.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Felix Maagi alisema mradi wa jengo hilo la ofisi na biashara la Singidani lililogharimu sh. bilioni 3.4 ulianza Januari 26, 2015 na kukamilika Februari 17, 2018 na linatarajia kuliingizia shirika pango ya sh. milioni 420 kwa mwaka. Tayari asilimia 50 ya jengo hilo limepangishwa.

Mkurugenzi huyo alisema mbali na mradi huo wa Singidani, pia shirika limeendelea kukua na kuimarika katika utendaji wake ambapo thamani ya mali zote imeongozeka kutoka sh. trilioni 1.7 mwaka 2011 mpaka kufikia sh. trilioni 4.8 mwaka 2018.

Bw. Maagi alisema mapato ya shirika yamekua kutoka sh. bilioni 40 kwa mwaka 2011 hadi kufikia sh. bilioni 154 mwaka 2018.” Pia shirika linalipa gawio la Serikali kila mwaka na gawio hilo limekua kutoka sh. milioni 250 mwaka 2011 hadi sh. bilioni 1.2 kwa mwaka 2018,”

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, wabunge wa mkoa wa Singida, viongozi wa dini na maafisa wa Serikali.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Viongozi wa Dini wakati alipowasili kwenye viwanja vya Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida, kufungua jengo hilo Juni 30, 2018. Kulia ni Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida,  Issa Ramadhani Simba na watatu kulia ni Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Baadhi ya wananchi na wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza kabla ya kufungua Jengo la Biashara la NHC la Singidani mjini Singida Juni 30, 2018. 
 Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Felix Manyama Maagi akisoma taarifa ya Shirika hilo mbele ya mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika tukio la ufunguzi wa Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na NHC mjini Singida Juni 30, 2018. 
 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema  Nchimbi akitoa salamu za mkoa mbele ya mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika tukio la  ufunguzi wa Jengo la Biashara la Singidani lililopo Singada mjini Juni 30, 2018. 
 Kikundi cha Kwaya cha Polisi Jamii cha Mjini Singida kikiimba mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  katika uzinduzi wa Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida Juni 30, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi wakati alipofungua Jengo la Biashara la Singidani lilijengwa na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) mjini Singida Juni 30, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika  la Nyumba la Taifa  (NHC) mjini Singida Juni 30, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la  Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida Juni  30, 2018.  Watatu kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi. Watatu kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Felix Manyama Maagi na kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum Neema Mgaya.  Wanne kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida Juma Kilimba na wapili kulia ni Mbunge wa Singida Mjini Mussa Sima. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (kushoto) wakifurahia baada ya Waziri Mkuu kufungua Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) mjini Singida Juni 30, 2018. Kulia ni Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima na wapili kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida, Juma Kilimba. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakimsikiliza, Kaimu Mkurugenzi wa Ubunifu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Margaret Ezekiel wakati alipotoa Maelezo kuhusu Jengo la Biashara la Singidani lililojengwa na NHC mjini Singida na kufunguliwa na Waziri Mkuu Juni 30, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wabunge walioshiriki katika ufunguzi wa Jengo la Biashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) la SIngidani mjini Singida Juni 30, 2018. Waliokaa, watatu kushoto ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Watano kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, Wasita kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida, Juma Kilimba na  kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Felix Manyama Maagi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi baada ya kufungua Jengo la Biashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Singida, Juni 30, 2018.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

No comments:

Post a Comment