Monday, July 9, 2018

MPINA AAMURU KUUNDWA KWA IDARA YA ULINZI WA MIFUGO NA MAZAO YAKE

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akitoa maelekezo ya serikali katika kikao hicho kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Abdallah Ulega 
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji Mh Mahamoud Mgimwa na wajumbe wa kamati hiyo akisikiliza mawasilisho ya Taarifa za Operesheni Nzagamba kutoka kwa wawasilishaji leo 
 WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiwa kwenye picha ya pamoja na kikosi kazi alichokiunda cha Operesheni Nzagamba 2018 na viongozi wakuu wa wizara na mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji Mh Mahmoud Mgimwa 



Na John Mapepele,Dodoma

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameamuru kuundwa Kitengo kipya cha Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali za Mifugo katika Idara ya Uzalishaji na Masoko cha wizara hiyo ili kutoa ulinzi wa kutosha wa mifugo na mazao yake baada ya kubainika kuwepo mianya mikubwa ya utoroshaji rasilimali hizo nje ya nchi na uingizaji holela wa mazao hayo nchini.

Pia ameagiza kuandaliwa mkakati wa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato yatokanayo na sekta ya mifugo baada ya kubainika kuwepo kwa mianya mingi na mbinu haramu zinazotumiwa kukwepa kulipa mapato ya Serikali hatua inayosababisha sekta ya mifugo kutoa mchango mdogo katika Pato la Taifa.

Sambamba na hilo pia Waziri Mpina ameagiza kupitiwa upya kwa mfumo wa uagizaji, ununuzi na usambazaji wa dawa za mifugo ambapo wafugaji wengi wamelalamikia mfumo wa sasa hasa katika upatikanaji wa dawa, bei kubwa, kuuziwa dawa zilizokwisha muda wa matumizi na dawa nyingi kutokuwa na viwango vya ubora unaotakiwa.

Akizungumza jijini Dodoma jana wakati wa tathmini ya operesheni ‘Nzagamba’, iliyodumu kwa muda wa miezi mitatu katika mikoa yote ya Tanzania Bara, Waziri Mpina alisema makusanyo ya maduhuli kutokana na operesheni hiyo jumla ya Tsh bilioni 7.1 zilikusanywa kutokana na tozo, kodi na faini mbalimbali ambapo kumepelekea makusanyo ya maduhuli ya wizara kwa mwaka wa fedha 2017/18 kufikia sh bilioni 19.5 ikilinganishwa na Tsh bilioni 12 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 2016/17.

Waziri Mpina alisisitiza kuwa awali Serikali ilikuwa inakusanya mapato yatokanayo na sekta ya mifugo yaliyokuwa kati ya Bilioni 10 hadi 12 kwa mwaka licha ya idadi kubwa ya mifugo iliyoko nchini hatua ambayo iliisukuma wizara hiyo kufanya operesheni ‘Nzagamba’ ili kubaini mianya ya upotevu wa mapato yatokanayo na sekta hiyo.

“Katika kipindi cha miezi mitatu ya operesheni hiyo jumla ya Ng’ombe 37,262, Mbuzi na kondoo 125,015, Punda 2,156 zilikamatwa zikisafirishwa bila vibali wala kulipiwa tozo husika kwenda nchi jirani za Kenya, Zambia, Comoro na Burundi huku tani 10,600 za vyakula vya mifugo na uingizaji wa mazao ya mifugo bila vibali kilo 1,619 nazo zikikamatwa katika operesheni hiyo”alisema.

Waziri Mpina alisema operesheni hiyo imebaini ukwepaji wa sh bilioni 1.27 kwa kampuni 15 zinazoingiza bidhaa za nyama na maziwa nchini.Aidha Serikali inapoteza vyote yaani mapato, ajira, malighafi za viwanda na kuigeuza Tanzania kuwa soko la bidhaa na machungio ya mifugo ya nchi jirani jambo ambalo Serikali ya awamu ya tano haitaliruhusu liendelee.

Kuhusu suala la usafirishaji mifugo ndani ya nchi bila kuwa vibali, Waziri Mpina alisema kosa hilo lilihusisha jumla ya ng’ombe 28,712, mbuzi/kondoo 11,251, nguruwe 801 na tani 480 za vyakula vya mifugo pia operesheni hiyo ilibaini uwepo dawa zilizokwisha muda wake kilo 805.

Mkuu wa Operesheni Nzagamba 2018, Dk. Lovince Assimwe alisema vikosi vya operesheni hiyo viligawanyika katika makundi matatu ya minadani,viwandani na ukaguzi wa hesabu ambapo imebainika kuwepo ukiukukwaji mkubwa wa Sheria, Kanuni na taratibu za uzalishaji,biashara ya mifugo,pembejeo na mazao ya mifugo katika maeneo ya usafirishaji mifugo nje ya nchi bila kuwa na vibali wala leseni.

Pia usafirishaji wa mifugo ndani ya nchi bila ya vibali, ukiukwaji wa haki za wanyama,uingizaji wa mazao ya mifugo nchini bila kuwa na vibali pamoja na uwepo wa dawa zilizokwisha muda wa matumizi,maeneo ya uzalishaji kutokuwa na wataalamu wa fani husika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa alisema kazi inayofanywa na wizara hiyo ya kudhibiti rasilimali za Taifa ni kuliunga mkono Bunge kwa kuzisimamia sheria ilizozitunga kusimamia sekta hiyo.

“Mnatuunga mkono kwa kusimamia sheria ambazo tumezitunga wabunge na  kwa usimamizi huu wa sheria sisi wabunge tutaendelea kuunga mkono juhudi zako Mhe Waziri na wizara kwa ujumla tumeridhika sana na hii operesheni ina manufaa makubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu”alisema Mgimwa. 

Mgimwa alisema Wizara ya Mifugo ni kubwa ina umuhimu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa viwanda na kuiagiza Wizara kuhakikisha operesheni hiyo inakuwa endelevu kwani imeonesha ongezeko kubwa la mapato ya Serikali.Pia Mgimwa alizitaka Wizara nyingine zinahusika na operesheni Nzagamba kutoa ushirikiano wa kutosha bila kukwamishana kwani kazi hiyo sio ya Wizara ya Mifugo peke yake bali ni suala la Taifa zima.

Nao baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walipongeza juhudi zilizofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuokoa rasilimali za Taifa na kutaka Serikali kutengeneza mfumo rasmi wa kuhakikisha ulinzi wa rasilimali hizo za mifugo unakuwa endelevu.

Katibu Mkuu Mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mary Mashingo alisema Serikali ya awamu ya tano imetilia mkazo suala la usimamizi wa sheria katika sekta ya Mifugo na kuwa uchochea muhimu katika uchumi wa viwanda

No comments:

Post a Comment