Sunday, July 8, 2018

DKT TIZEBA NA DKT MABULA WAMALIZA MGOGORO WA ARDHI WA CHAMA CHA USHIRIKA ULIODUMU KWA MIAKA 17


Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza jambo kwa msisitizo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula, Leo 8 Julai 2018. (Picha zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza na wazee kijijini Nyamatongo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba, Naibu waziri wa ardhi, nyumba na  maendeleo ya makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa kijiji cha Nyamatongo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 Julai 2018.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza jambo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baada ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 Julai 2018.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana (Kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha ushirika Nyamatongo Ndg Willium Elikana mara baada ya kuridhia mgogoro kumalizika.


Na Mathias Canal, Sengerema-Mwanza

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula wametatua mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17.

Mgogoro huo umemalizika kwa maelewano ya pande zote mbili kuwa na kauli moja ambapo Mwenyekiti wa kijiji hicho amekubali kuketi meza moja na Uongozi wa chama hicho cha ushirika ili kukubaliana namna bora ya kuchochea Maendeleo katika kijiji na Taifa kwa ujumla badala ya kuendeleza mgogoro usiokuwa na maslahi kwa pande zote.

Alisisitiza umuhimu wa ushirika nchini ambapo aliwaeleza wananchi hao kutoendeleza vita ya kutokuwa na maelewano kwani kufanya hivyo kunarudisha nyuma shughuli za Maendeleo ya kijiji na Taifa kwa ujumla wake.

Pia, Dkt Tizeba ametangaza Kiama kwa maafisa ugani wanaokaa maofisini badala ya kuwasaidia wakulima kwenye hatua muhimu za uandaaji wa shamba na hatimaye wakati wa Kilimo.Katika mkutano huo Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angelina Mabula aliwataka wananchi hao kuwa na utamaduni wa kuketi pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili ili kuzitatua kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa migogoro kama hiyo haihitaji sintofahamu ya mashitaka ya muda mrefu kwani kufanya hivyo ni kutengeneza uhasama usio kuwa na sababu ilihali wote ni watanzania.Dkt Mabula aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kutatua changamoto zote zinazohusisha wananchi katika migogoro ya ardhi pamoja na kadhia zingine zote.

Mgogoro huo ambao ulianza tangu mwaka 2001 umekuwa na hatua za kushitakiana baina ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamatongo dhidi ya Chama cha ushirika Nyamatongo katika maeneo mbalimbali tangu mwaka 2001 ambapo awali ulitolewa maamuzi katika ngazi ya baraza la kijiji baadae baraza la kata na hatimaye Baraza la Ardhi la Wilaya ya Sengerema ambalo ndilo liliamua kuvunja maamuzi yote ya baraza la kijiji na Kata ili kuanza upya usikilizwaji wa kesi hiyo.

Mara baada ya kumalizika kwa mgogoro huo wananchi kijijini hapo wamempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angelina Mabula kwa kuzuru kijijini hapo hatimaye kutatua mgogoro huo ambao umekuwa sugu kwa miaka 17.

Aidha, katika mkutano huo wananchi wamepata nafasi ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili kijijini hapo ikiwemo ukosekanaji wa maji safi na salama, huku wengine wakieleza kusikitishwa na maafisa ugani kuketi maofisini pasina kuzuru kwa wakulima ili kuwafundisha mbinu bora za Kilimo.

No comments:

Post a Comment