Monday, July 2, 2018

BODI YA USHAURI YA HOSPITALI TEULE YA MKOA SIMIYU YAZINDULIWA

Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Hospitali Teule ya mikoa wa Simiyu, Bw. Gigi Mathias akiwaonesha wajumbe wa bodi hiyo mwongozo wa kuendesha bodi hiyo mara baada ya bodi hiyo kuzinduliwa.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Bodi ya Ushauri ya Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu imezinduliwa rasmi na kutakiwa kusimamia vema Hospitali hiyo ili kuhakikisha huduma za afya zinatolewa ipasavyo kwa wananchi.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ulifanyika katika Ukumbi wa Hospitali hiyo Mjini Bariadi, mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Utawala na Rasilimaliwatu Chele Ndaki, amesema bodi hiyo inalo jukumu kubwa la kuisimiamia hospitali teule ya mkoa na kuhakikisha huduma za afya zinatolewa katika viwango vinavyotakiwa.

"Mnalo jukumu kubwa katika kuhakikisha kwamba huduma za afya zinazotolewa zinaendana viwango vya Serikali yetu, nafikiri hata ninyi mnaona namna viongozi wetu walivyolipa kipaumbele suala afya, lengo ni kuhakikisha wananchi ambao ndiyo waajiri wetu wapewe huduma nzuri na waendelee kufanya shughuli zao za uzalishaji" alisema Ndaki.

Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Utawala na Rasilimaliwatu Chele Ndaki, akimkabidhi Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya HospitalI za mikoa, Bw. Gigi Mathias kama ishara ya kuizinda bodi hiyo.

Amesema pamoja na kushauri juu ya namna hospitali inavyotoa huduma, bodi hiyo pia itakuwa na jukumu la kushauri uongozi wa hospitali na kutoa mapendekezo juu ya mambo mbalimbali yanayolenga kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi ili waweze kutoa huduma zinazotakiwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Bw. Gigi Mathias amesema wajumbe wa bodi hiyo wamejiwekea mpango kazi utakaowazesha kutoa ushauri ili kuboresha mambo mbalimbali katika hospitali hiyo.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Chele Ndaki akiwaongoza Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali Teule ya Mkoa, kutembelea na kuona Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) linalojengwa Eneo la Nyaumata Mjini Bariadi baada ya uzinduzi wa bodi hiyo, uliofanyika katika ukumbi wa Hospitali Teule ya Mkoa mjini Bariadi.

"Kama bodi tutaishauri Menejimenti ya Hospitali iweze kuboresha huduma kwa wananchi na watumishi pia kwa sababu kama watumishi hawataboreshewa huduma zao muhimu utendaji wao utakuwa hafifu; tutasimamia rasilimali zote za hospitali, pia tuna jukumu kama bodi kusimamia kandarasi zote na kuhakikisha zinafanya kazi kwa viwango” alisema Gigi.

“Kwa kuwa bodi hii ina wajumbe wengi ambao ni watumishi wa Serikali na wengine ni wastaafu ambao ni wazoefu katika nyanja mbalimbali nina uhakika tutaishauri Menejimenti ya Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu katika masuala yote kwa lengo la kuboresha utendaji na utoaji wa huduma bora" alisisitiza.

Naye Mjumbe wa bodi hiyo Bw. Said Zongo amesema wajumbe wa bodi hiyo watafanya kazi ya kuishauri Menejimenti ya Hospitali Teule ya Mkoa kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Chele Ndaki akizungumza na Wajumbe wa bodi ya ushauri ya HospitaIi ya Mkoa, kabla ya uzinduzi wa bodi hiyo, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa HospitalI Teule ya Mkoa mjini Bariadi.
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu, Bw. Said Zongo akichangia hoja katika kikao cha uzinduzi wa bodi hiyo, kilichofanyika mjini Bariadi.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Utawala na Rasilimaliwatu Chele Ndaki, (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya HospitaIi Teule ya Mkoa, baada ya uzinduzi wa bodi hiyo, katika uliofanyika katika ukumbi wa HospitalI Teule ya Mkoa mjini Bariadi.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Chele Ndaki akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya HospitaIi Teule ya Mkoa, baada ya uzinduzi wa bodi hiyo, katika uliofanyika katika ukumbi wa HospitalI Teule ya Mkoa mjini Bariadi.

No comments:

Post a Comment