Friday, June 1, 2018

WAZIRI MKUU MGENI RASMI KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA YA KUHIFADHI QURAN YATAKAYOFANYIKA JUNI 3 ,2018 JIJINI DAR

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Fainali ya Mashindano ya Kimataifa ya kuhifadhi Quran yanayotarajiwa kufanyika Juni 3 mwaka huu jijini Dar es Salaam ambapo mataifa zaidi ya 20 yameshiriki.

Mashindano hayo yameandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania.Mbali ya kuwepo kwa Waziri Mkuu Majaliwa viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwamo wastaafu nao watakuwa miongoni mwa watakaohudhuria kushuhudia mashindano hayo yenye hadhi ya kimataifa.

Viongozi wastaafu watakaohudhuria siku hiyo ni Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne mzee Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais mstaafu Dk.Mohammed Ghalib Bilal pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mratibu wa Mashindano hayo kutoka Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania Sheikh Mohamed Nasoro amesema tayari washiriki karibu wote wamewasili chini Tanzania ambapo waliopo sasa ni washiriki kutoka mataifa 18 kati ya mataifa 20 ambayo yamealikwa.

Pia amesema mbali ya washiriki kuwapo nchini, tayari majaji wa mashindano hayo nao wapo na wamekuwa wakiendelea kuchuja washiriki ili kubaki na wale watakaoingia fainali na hatimaye washindi ukabidhiwa zawadi zao na Waziri Mkuu.

"Washiriki karibu wote wamewasili nchini na hadi jana tayari washiriki tisa wamesikilizwa na majaji wetu na leo watawasikiliza washiriki wengine tisa ili kuwachuja na kubaki wale watakaoingia hatua ya fainali na hatimaye kupewa zawadi zao ambapo kwa sasa hatuaamua kuweka hadharani mshindi atapata zawadi ya aina gani na tunafanya hivyo kwasababu maalumu.

"Majaji ambao wapo kwenye mashindano hayo wanatoka katika nchi mbalimbali duniani.Huu ni mwaka wa pili Jumuiya yetu kuandaa mashindano haya na hakika tunakwenda vema,"amesema Sheikh Nasoro.Ametaja baadhi ya nchi zinazoshiriki mashindano hayo ya kimataifa ni Uingereza, Saud Arabia, DRC Congo, Tanzania, Kenye, Uganda, Mali, Sudan, Yemen na Marekani. "Hizo ni baadhi tu ya mataifa ambayo washiriki wake tayari wamefika nchini kwa ajili ya mashindano hayo,"amesisitiza.

Kuhusu umuhimu wa vijana wa Kiislamu kuhifadhi Quran amesema Quran ndio Katiba pekee isiyobadilika na inatoa maelekezo na miongozo mbalimbali ya namna ya kuishi hapa duniani, hivyo vijana wanapohifadhi Quran faida kubwa wanaishi katika misingi ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.

"Tuishauri jamii ya Kiislamu kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya dini na hili la kuhifadhi Quran ni mojawapo.Tunaamini vijana wakiandaliwa katika misingi ya imani ni rahisi kupata viongozi wazuri na wenye hofu ya Mungu,"ameongeza.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania Mohamed Ali Hassan amesema wanamshukuru Mungu kwani maandalizi yanakwenda vizuri na mwitikio kwa walioalikwa ni mkubwa na kusisitiza majaji wapo tayari kufanya kazi ya kuchuja washiriki hao ili kubaki na wale watakaoingia hatua ya mwisho ya fainali.



No comments:

Post a Comment